1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Medvedev apongezwa na jumuiya ya kimataifa

Josephat Charo3 Machi 2008

Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Marekani zampongeza Medvedev na kutaka kuendeleza ushirikiano na Urusi

https://p.dw.com/p/DHR5
Rais mteule wa Urusi, Dmitry Medvedev (kushoto)na rais anayeondoka Vladamir Putin anatakayekuwa waziri mkuu katika serikali mpyaPicha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo amempongeza rais mteule wa Urusi, Dmitry Medvedev, kwa ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani wake lakini akaeleza masikito yake kuhusu matatizo yaliyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais nchini Urusi. Uingereza imempongeza Medvedev huku Ufaransa ikilalamika hakukuwa na mashindano katika uchaguzi wa Urusi. Wakati huo huo, waangalizi wa nchi za magharibi wanasema uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki. Josephat Charo anaarifu zaidi.◄

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempongeza Dmitry Medvedev kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Urusi na anatarajia kuendeleza ushirikiano mpana na nchi hiyo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani mjini Berlin, Thomas Steig, amesema bila shaka kulitokea hali fulani wakati wa kampeni za uchaguzi zilizodhihirisha sheria za demokrasia hazikuzingatiwa kila mara.

Aidha msemaji huyo amesema serikali ya Ujerumani iliweka wazi hali hiyo kabla uchaguzi wa jana nchini Urusi na kueleza masikitiko yake kwamba waangalizi wa kimataifa hawakuweza kufanya kazi yao kama ilivyotakiwa. Steig amesema Ujerumani inautazama ushindi mkubwa wa Medvedev kama ishara ya ari ya Warusi kutaka kuendelea mbele. Kansela Merkel ameukaribisha ukweli kwamba rais mteule wa Urusi,Dmitry Medvedev, ameashiria mara kwa mara anataka kulifanya taifa la Urusi kuwa la kisasa na kuufanya madhubuti utawala wa sheria.

Ingawa Ujerumani inasema uchaguzi wa Urusi haukuzingatia kikamilifu maadili ya demokrasia, kansela Merkel amemtakia kheri na mafanikio rais mteule Medvedev katika jukumu gumu linalomsubiri. Bi Merkel amesema anataka kukutana naye pamoja na rais anayeondoka Vladamir Putin haraka iwezekanavyo. Ripoti ya vyombo vya habari kwamba Merkel atakutana na viongozi hao Jumamosi wiki hii haijathibitishwa.

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amempongeza pia Medvedev lakini hajamualika kiongozi huyo kwa mazungumzo mjini London. Brown amemuandikia Medvedev akisisitiza matumaini kwamba Uingereza na Urusi zitaweza kuurekebisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambao umeharibika mno. Serikali ya Uingereza inatarajia ushirikiano zaidi na Urusi na imesema itaihukumu serikali mpya ya mjini Moscow kwa matendo yake na athari zake.

Huko nchini Ufaransa, rais Nicolas Sarkozy wa nchi hiyo amempongeza Medvedev kwa njia ya simu kwa ushindi wake katika uchaguzi na kumhakikishia nia yake kuuimarisha ushirikiano wa Ufaransa na Urusi.

Lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, amesema hakukuwa na mashindano ya maana katika uchaguzi wa Urusi. Kouchner amesema uchaguzi huo ulifanyika mtindo wa Urusi matokeo yakijulikana kabla na kuutaka Umoja wa Ulaya utafute njia mpya ya kuwasiliana na Urusi chini ya utawala mpya wa rais Medvedev ili kuisaidia nchi hiyo irejee mahala inapostahiki.

Katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, kiongozi wa halmashauri ya umoja huo, Jose Manuel Barroso, ameeleza matumaini yake kwamba umoja huo utaweza kuendeleza ushirikiano wake wa kimkakati na Urusi chini ya kiongozi mpya Medvedev. Hata hivyo ameitaka Urusi iheshimu demokrasia na haki za binadamu.

Rais George W Bush wa Marekani amesema anatarajia kufanya kazi pamoja na Medvedev na atawasiliana naye kwa njia ya simu wiki hii. Msemaji wa maswala ya usalama nchini Marekani, Gordon Johnroe, hakusema lolote kuhusu uchaguzi wa Urusi ulivyofanyika lakini akasema Marekani itashirikiana na Urusi katika maswala ya masilahi ya pamoja kama vile kuzuia utapakazaji wa silaza za nyuklia, vita dhidi ya ugaidi na juhudi za kupambana na uhalifu wa kimataifa.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya jamhuri ya Cheki, imesema uchaguzi wa Urusi haukuwa wa haki ikisema wagombea hawakupewa nafasi sawa. Imewalaumu viongozi wa Urusi kwa kutowaruhusu waangalizi huru wa uchaguzi nchini humo. Uhusiano kati ya Urusi na jamhuri ya Cheki umekuwa ukizorota baada ya serikali ya mjini Prague kuwa tayari kukubali Marekani ijenge sehemu ya mfumo wa ulinzi wa makombora katika ardhi yake.

Waangalizi wa bunge la baraza la Ulaya, PACE, wamesema uchaguzi wa Urusi haukuwa huru wala wa haki. Kiongozi wa baraza hilo, Andreas Gross amesema uchaguzi huo ulikuwa kama kura ya maoni juu ya rais mteule Dmitry Medvedev.

Hii leo polisi wamewakamata watu takriban watano katika maandamano ya kupinga ushindi wa Medvedev mjini Moscow. Madarzeni ya watu wamefanya maandamano ambayo hayakuidhinishwa mjini humo.