1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Medvedev: Vita Baridi vipya vimeanza

13 Februari 2016

Dunia imetumbukia kwenye "Vita Baridi Vipya" amesema Waziri Mkuu wa Urusi Jumamosi (13.02. 2016) wakati mvutano wa Urusi na mataifa ya magharibi kuhusu Ukraine na Syria ukihodhi mkutano wa usalama nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1Hv0s
Waziri Mkuu wa Urusi Dmitri Medwedew katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)
Waziri Mkuu wa Urusi Dmitri Medwedew katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)Picha: Reuters/M. Dalder

Akizungumza katika mkutano huo wa usalama mjini Munich Dmitry Medvedev amesema dunia imetumbukia katika kipindi kipya cha vita baridi wakati tafauti zikiongezeka kati ya Urusi na mataifa ya magharibi kushusiana na mizozo nchini Ukraine na Syria.

Amewaambia wajumbe katika mkutano huo mjini Munich katika jimbo la Bavaria nchini Ujerumani kwamba takriban kila siku wanashutumiwa kwa kutowa vitisho vipya aidha dhidi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO au nchi nyengine.

Hata hivyo Medvedev amesema kutokana na changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa kama vile mizozo ya kikanda, ugaidi na mzozo wa wahamiaji Urusi inatakiwa nchi hiyo ichukuliwe kama mshirika : Ameongeza kusema kwamba tafauti zilioko kati ya Urusi na nchi nyengine duniani zinaweza kutatuliwa.

Amesema "misimamo yetu inatafautiana lakini haitafautiana sana kama ilivyokuwa miaka 40 iliopita ambapo wakati kulikuwa na ukuta uliosimama barani Ulaya.".Ametaja mfano wa makubaliano kadhaa yaliyofikiwa tokea wakati huo yakiwemo masuala ya upunguzaji wa silaha mpango ya nyuklia wa Iran na uharamia.

Sera za kujitanuwa

Waziri Mkuu huyo wa Urusi ameyashutumu mataifa ya maggharibi kwa sera zake za kujitanuwa kuingia kwenye majimbo yaliokuwa yakitawaliwa na muungano wa zamani wa Kisovieti mashariki kwa Ulaya tokea kumalizika kwa vita baridi kwa kusema hatua hiyo inazidi kukuza mfarakano na Urusi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev pembezoni mwa mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kushoto) na Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev pembezoni mwa mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)Picha: Reuters/D. Astakhov

Amesema "wanasiasa wa Ulaya walidhani kuanzisha kile kinachojulikana kama ni ukanda wa marafiki pembezoni mwa Umoja wa Ulaya kunaweza kuwa hakikisho la usalama na ameuliza matokeo yake ni nini ? Sio ukanda wa marafiki bali wa mtengano."

Medvedev pia amehoji busara ya kuwekewa vikwazo Urusi na mataifa ya magharibi kutokana na kulitwaa jimbo la Crimea na kuwasaidia waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine kwa kusema vinaleta madhara kwa pande zote mbili badala ya kuwa na ushirikiano wa dunia kupambana na kile alichokitaja kuwa mzozo wa uchumi unaozidi kukua duniani.

Vikwazo dhidi ya Urusi kubakia

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameuambia mkutano huo wa usalama mjini Munich Urusi inapaswa kusita kuwashambulia waasi wa msimamo wa wastani nchini Syria na kuviondowa vikosi vyake kutoka Ukraine.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)Picha: Reuters/M. Dalder

Kerry amesema hadi sasa sehemu kubwa ya mashambulizi yake yamekuwa dhidi ya makundi halali ya upinzani.Amesema ili kuheshimu makubaliano iliyoafiki mashambulizi ya Urusi lazima yabadlike akikusudia makubaliano yaliofikiwa Ijumaa ambapo mawaziri wa mambo ya nje walikubali kutafuta usitishaji wa uhasama nchini Syria katika kipindi kisichozidi wiki moja.

Kerry pia amesisitiza kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vitaendelea kubakia hadi hapo nchi hiyo itakapotekeleza fani zote za makubaliano ya amani ya Ukraine yaliofikiwa katika mji mkuu wa Belarus Minsk mwaka jana.

Amesema Urusi ina chaguo rahisi kuamuwa : itekeleze kikamilifu makubaliano ya Minsk au iendelee kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi vyenye kuiathiri nchi hiyo.

Jopo la viongozi wa Ulaya ya mashariki walikuwa na shauku kuongezea shutuma zao dhidi ya sera ya shari ya kigeni ya Urusi.

Putin ashutumiwa

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema kila siku vikosi vya Urusi,silaha zan Urusi, risasi za Urusi zinapenyezwa nchini mwangu.

Rais Petro Poroschenko wa Ukraine katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)
Rais Petro Poroschenko wa Ukraine katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)Picha: Reuters/M. Dalder

Hotuba yake amemwelekezea rais wa Urusi ambaye hakushiriki mkutano huo akisema :Bw. Putin hivi sio vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ukraine ,huu ni uvamizi wako.Hivi sio vita vya wenyewe kwa wenye Crimea hawa ni askari wako wanaoikalia kwa mabavu nchi yangu.

Akizungumza kwa hisia nzito Poroshenko pia amesema kwamba makundi yanyaoiunga mkono Urusi yanaiyumbisha Ulaya yakiwa ndani ya bara hilo kwa kutumia mbinu mbali mbali.

"Mtengano,kutokuvumiliana, kutoheshimu haki za binaadamu,misimamo mikali ya kidini,chuki dhidi ya wageni" amesema Ulaya hiyo mbadala ina kiongozi wake ambaye ni Bw.Putin.

NATO haitaki vita vipya baridi

Katibu Mkuu wa Jumuiya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg pia ameuhutubia mkutano huo wa Munich akiahidi kuikabili Urusi kwa msimamo madhubuti wa pamoja kwa kuwa na mazungumzo zaidi na nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya Kujihami NATO Jens Stoltenberg katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)
Katibu Mkuu wa Jumuiya Kujihami NATO Jens Stoltenberg katika mkutano wa usalama Munich. (13.02.2016)Picha: picture alliance/dpa/S. Hoppe

"Tumekuwa tukishuhudia msimamo wa kimabavu wa Urusi, Urusi yenye kuyumbisha mpangilio wa usalama barani Ulaya.Amesema "NATO haitaki malumbano na hatutaki vita vipya baridi .Wakati huo huo jibu letu lazima liwe madhubuti."

Mapema wiki hii Stolteberg ametangaza kwamba mipango imeidhinishwa ya kuongeza uwepo wa NATO mashariki mwa Ulaya ambapo duru zinasema zitahusisha kati ya wanajeshi 3,000 hadi 6,000 wakizunguka katika kanda hiyo nzima.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/Reuters

Mhariri : Amina Abubakar