1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli kutoka Tanzania kuelekea Kongo yazama

8 Aprili 2024

Meli ya MV Maman Benita iliyokua na mizigo ikitokea Kigoma nchini Tanzania Jumamosi kuelekea Kalemie Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilizama usiku wa kuamkia Jumapili ambapo baadhi ya abiria hawajulikani walipo.

https://p.dw.com/p/4eXlA
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo | Boti ikiwa imebeba abiria karibu na Mbandaka huko Kongo
Boti ikiwa imebeba abiria karibu na Mbandaka huko KongoPicha: Junior Kannah/AFP/Getty Images

Hayo yakiarifiwa, watu 25 wameuwawa mashariki mwa Kongo kutokana na shambulio la waasi wa CODECO.

Meli hiyo ilikua na watu 26 wakiwemo raia 4 wa Tanzania, Mkenya mmoja, Wachina 4 na Wakongomani 17 kulingana na taarifa ya idara ya usafiri katika bandari ya kalemie.

Watu 15 wameokolewa huku maafisa wa uokoaji wakiendelea kutafuta wengine.

Upepo mkali ndio umesababisha ajali

Afisa tawala  wa tarafa ya Kalemie John Mutombo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Meli katika bandari ya Kigoma, Tanzania
Meli katika bandari ya Kigoma, TanzaniaPicha: Martin Kotthoff/dpa/picture alliance

Abdul Ally Kayanda raia wa Tanzania ambaye ndugu yake amenusurika katika ajali hiyo ameiomba idara ya usafirishaji nchini Tanzania kudhibiti swala la upakiaji mizigo katika bandari ya Kigoma.

Idara ya uchukuzi katika bandari ya Kalemie kupitia kamishna wake Jean Kyato imesema kuwa chanzo cha ajali ni upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa.

Licha ya picha za mwisho za meli hiyo kuonesha imepakia  mzigo mkubwa, afisa huyo amedai meli haikuwa imepakia zaidi ya uwezo wake.

Mili 25 imepatikana Ituri

Ajali hiyo imetokea sambamba na mauwaji ya watu 25 walio shambuliwa na waasi wa CODECO huko jimboni Ituri mashariki mwa Kongo ambapo mashirika ya kiraia pamoja na Umoja wa Mataifa wamethibitisha kutokea kwa shambulio hilo.

Mazishi ya raia waliouwawa na waasi wa Codeco huko Ituri
Mazishi ya raia waliouwawa na waasi wa CodecoPicha: Jorkim Jotham Pituwa/AFP via Getty Images

Taarifa kutoka huko zinasema  miili 10 ilipatikana Jumamosi na 15 Jumapili katika kijiji cha Galayi, kilomita 70 kaskazini magharibi mwa mji wa Bunia,

Ikumbukwe kuwa hali ya kibinaadamu huko ituri imezorota tangu mwanzo wa mwaka huu kutokana na mashambulizi ya waasi wa CODECO, Ofisi ya pamoja ya haki za kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRC) ilisema.