1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ya Ukraine yaachiliwa huru.

Eric Kalume Ponda6 Februari 2009

Meli ya Ukraine ambayo iliachiliwa jana baada ya kuzuiliwa na maharamia wa kisomali tangu mwezi Septemba mwaka uliopita katika Pwani ya Somalia ikiwa na shehena ya silaha sasa inaelekea bandari ya Mombasa nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/GoOO
Moja ya meli zinazozuliwa na maharamia katika Pwani ya Somalia.Picha: AP

Meli hiyo iliachiliwa huru baada ya maharamia hao kulipwa fidia ya kiasi cha dola milioni tatu walizodai kumaliza mzozo huo uliochukua muda mrefu zaidi.


Hata hivyo bado kuna maswali mengi kuhusiana na mmiliki wa shehena ya silaha iliyomo.


Tangazo ya kuachuliwa huru kwa meli hiyo lilitolewa na serikali ya Ukraine kwamba Meli hiyo Mv Faina iliyokuwa na jumla ya wafanyi kazi 20 sasa inaelekea katika bandari ya Mombasa baada ya kuachiliwa hapo jana.


Duru za karibu na kundi hilo la Maharamia zinasema kuwa fidia hiyo ilisafirishwa kutoka mjini Nairobi na kudondoshwa katika meli hiyo ingawa bado haijabainika wazi ni nani aliyelipa kiasi hicho cha fedha.


Wafanyi kazi wa meli hiyo ambao ni raia wawili wa Urusi, 17 wa Ukraine na Mmoja wa Latvia wanasema kama wako katika hali nzuri ya afya baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabi ndani ya meli hiyo kwa mjibu wa mwenyekiti wa chama cha Mabaharia nchini Kenya Andrew Mwangura.


Meli hiyo ambayo imekuwa ikizuiliwa katika mji wa bandari wa Harardhare katika pwani ya Somalia, ilizua mvutano kuhusiana na shehena iliyoko kwenye Meli hiyo baada ya madai kutolewa kwamba ilikuwa ikisafirisha shehena ya silaha hadi eneo la Kusini mwa Sudan.


Meli hiyo ina shehena ya vifaru aina ya T-7 na aina nyingine mbali mbali ya silaha. Serikali ya Kenya ilikanusha madai hayo ikisema kuwa shehena iliyoko katika meli hiyo ni yake.


Maafisa wa serikalini nchini Kenya hata hivyo wamekataa kuzungumzia suala hilo wakitaja sababu za kiusalama


Msemaji wa kundi hilo la maharamia Sugule Ali alisema kuwa mashua ya vikosi vya usalama dhidi ya uharamia katika pwani hiyo ya Somalia ilielekea katika meli hiyo punde tu baada ya maharamia hao kuichilia huru, ingawa shughuli hiyo ilicheleweshwa kwa muda wa saa moja kwa sababu maharamia watatu bado walikuwa wamekwama ndani ya meli hiyo. Meli hiyo imekuwa ikizuiliwa tangu Septemba 25 na zaidi ya maharamia 50 .


Maharamia hao walikuwa wamedai fidia ya kiasi cha Dala milioni 35 lakini baada ya mazungumzo ya muda mrefu hatimaye walikubali kiasi cha Dola milioni 3.5. Wamiliki wa meli hiyo walikuwa wanataka kulipa kiasi cha dola milioni moja kilichokataliwa na kundi hilo la maharamia.


Ponda/Afp