1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meneja wa Kampuni ya Hisa ya Wall Street ya Marekani, akumbwa na kashfa ya wizi.

Halima Nyanza18 Desemba 2008

Meneja wa Vitega Uchumi wa Kampuni ya Hisa iliyoporomoka ya Wall Street ya Marekani, Bernard Madoff ambaye anatuhumiwa kwa wizi wa dola bilioni 50, amekamatwa jana na kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani.

https://p.dw.com/p/GIZb
Meneja wa Uwekezaji katika Kampuni ya Wall Street ya Marekani Bernard Madoff akirudi nyumbani kwake Manhattan, akitokea mahakamani kusikiliza kesi yake.Picha: AP

Jaji nchini Marekani aliamuru Bernard madoff mwenye umri wa miaka 70 kuzuiliwa katika nyumba yake ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 7 iliyoko katika kitongoji cha Manhattan mjini New York.

Aidha Mtuhumiwa huyo ametakiwa kuvaa kifaa maalum cha umeme, ambacho kitamfanya kuweza kufatiliwa nyendo zake na kwamba ataruhusiwa kuondoka nyumbani kwake kwa ruhusa maalumu.

Aidha Mke wa Madoff ametakiwa kukabidha pasi yake ya kusafiria mchana wa leo kama sehemu ya masharti ya dhamana.

Mke wa mtuhumiwa huyo naye pia anachunguzwa na Tume maalum inayochunguza kashfa hiyo, iwapo aliweza kusaidia kuficha kumbukumbu za zilizotumika katika madai hayo ya wizi.

Jana Mchana mtuhumiwa huyo Bernard Madoff alisaini makubaliano ya kutaifisha nyumba yake ya kifahari iliyoko Manhattan na mali zake nyingine zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini humo, iwapo atashindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Bernad Madoff amefanikiwa kupata sahihi za watu wawili waliojitokeza kumdhamini mahakamani kati ya watu wanne waliohitajika licha ya kuwa na marafiki wengi katika sekta hiyo ya uwekezaji.

Alhamisi iliyopita Bernard Madoff alishtakiwa kwa kuiba kiasi hicho cha fedha kupitia wawekezaji, katika mradi ambao wawekezaji wa baadaye hulipa faida zao kwa wawekezaji wa mwanzo.

Imearifiwa kwamba Benki ya BNP Paribas ni miongoni mwa benki za Ulaya iliyoelezwa kukumbwa na kashfa hiyo na kwamba ndiyo iliyopoteza hisa nyingi miongoni mwa benki za Ulaya katika kashfa hiyo.

Hayo yalifahamika wakati Mwenyekiti wa Tume maalum inayochunguza kashfa hiyo Christopher Cox alipokuwa akijibu maswali kuwa, ilikuaje udanganyifu huo uliendelea kwa muongo mzima bila ya kujulikana.

Iwapo atakutwa na hatia mtuhumiwa huyo, atakabiliwa na kifungo hadi cha miaka 20 gerezani na kulipa faini ya dola milioni 5.

Kwa upande wake Mbunge mmoja wa Marekani kupitia chama cha Republican Paul Kanjorski ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusiana na masoko ya hisa, amesema Bunge la nchi hiyo litahitaji kuchunguza upya sheria za kuwalinda wawekezaji ili kuepukana na kutokea tena kwa kashfa kama hiyo.

Mbunge huyo amesema mwakani mwezi Januari, ataitisha kikao cha kamati hiyo kuchunguza suala hilo.

Katika hatua nyingine Mwanasheria mkuu wa Marekani Michael Mukasey amejiondoa katika uchunguzi wa kashfa hiyo kwa sababu za kibinafsi.

Mwakani mwezi Januari Mwanasheria huyo anamaliza muda wake wa kazi hiyo.