1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aahidi msaada kwa Ugiriki kabla kura muhimu bungeni

28 Septemba 2011

Masoko ya hisa barani Ulaya yameimarika kufuatia matumaini mapya yaliyojitokeza kuhusiana na tatizo la madeni linaloikabili Ugiriki, huku thamani ya hisa za Ujerumani na Ufaransa ikipanda kwa asilimia tano.

https://p.dw.com/p/12i8s
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kushoto, na waziri mkuu wa Ugiriki, George PapandreouPicha: dapd

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ameahidi kuisaidia Ugiriki kwa kila hali kukabiliana na tatizo kubwa la madeni linaloikabili. Bi Merkel alikutana jana na waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou mjini Berlin, kuzungumzia mzozo huo unaoyumbisha Ugiriki kiuchumi.

Mkutano kati ya viongozi hao umeongeza matumaini ya kuidhinishwa mfuko maalumu kwa ajili ya kuziokoa nchi zinazokabiliwa na madeni katika eneo linalotumia sarafu ya euro. Papandreaou alizuru Berlin siku mbili kabla bunge la Ujerumani, Bundestag, kuupigia kura mfuko huo wa thamani ya euro bilioni 440. Akiwahutubia viongozi wa kibiashara kwenye mkutano wa shirikisho la viwanda la Ujerumani, Papandreou amehakikisha kwamba Ugiriki itaweza kulipa madeni yake.