1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akamilisha ziara yake katika vinu vya kinuklia

Sekione Kitojo27 Agosti 2010

Serikali ya Ujerumani inafikiria upya lengo lake la kuweka kodi zaidi kwa viwanda vinne vikubwa vya kuzalisha nishati ya kinuklia, siku chache baada ya maafisa wa serikali ´kusema hivyo.

https://p.dw.com/p/Oy8a
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anafikiria kubadilisha msimamo kuhusu kodi ya vinu vya kinuklia.Picha: AP

Serikali ya Ujerumani inafikiria upya lengo lake la kuweka kodi zaidi kwa viwanda vinne vikubwa vya kuzalisha nishati ya kinuklia , siku chache baada ya maafisa wa ngazi ya juu kusema kuwa makampuni hayo yatalazimika kulipa fedha zaidi ili kuweza kupatikana kwa nishati mbadala isiyoharibu mazingira.

Ripoti iliyochapishwa katika gazeti la kila siku la Süddeutsche Zeitung leo Ijumaa imesema kuwa serikali ya kansela Angela Merkel badala yake inaelekea katika kuyaruhusu makampuni ya Eon, RWE, EnBW na Vattenfall kulipa fedha za mchango wa hiyari.

Siku ya Jumatatu katibu mkuu wa chama tawala cha Christian Democratic , CDU Hermann Groehe amesema kuwa mapampuni hayo yatalipa kodi ya ziada pamoja na kodi ya kila mwaka ya euro bilioni 2.3 ya fito za mafuta ya kinuklia.

Serikali inataka kurefusha kwa muda wa kisheria wa kutumika vinu hivyo 17 vya kinuklia nchini Ujerumani .

Hata hivyo , ikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa makundi ya walinzi wa mazingira , chama cha Social Democratic, SPD na baadhi ya wanachama wa chama chake , Merkel amesema kuwa makampuni hayo yanapaswa kutoa faida ya ziada inazopata.

Katika ziara aliyoifanya katika kinu cha kinuklia kinachoendeshwa na kampuni ya RWE jana Alhamis , Merkel na mwenyekiti wa kampuni hiyo Jurgen Grossman walitumia neno mchango kuelezea malipo hayo mapya yanayozungumzwa.

Msemaji wa serikali Christoph Steegmans amesema leo kuwa neno hilo limeteuliwa mahsusi , lakini hakuthibitisha iwapo malipo hayo mapya yatakuwa ya hiari. Serikali kwa sasa inatayarisha mpango ambao unasubiriwa kwa hamu , ambao una lengo la kuimarisha mkakati wa matumizi ya mafuta ya kinuklia na kuweka mizani ahadi za upunguzaji wa gesi zinazoharibu mazingira za carbon huku kukiwa na usalama katika ugavi wa nishati.

Makampuni ya kinuklia yamejibu taarifa hizo kwa upinzani mkubwa dhidi ya kodi hiyo ya fito za mafuta ya kinuklia , ambayo ilikuwa ni mpango wa serikali wa kuimarisha bajeti iliyoidhinishwa mwezi wa Julai.

Makampuni hayo yanadai kuwa kodi hiyo itafanya makampuni hayo yasiweze kujiendesha kibiashara, yametishia kuacha kuzalisha nishati na kuuza nchi za nje nishati hiyo inayotokana na vinu vya kinuklia.

Mwandishi: Sekione Kitojo / DPAE

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman