1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya Uingereza haitapata upendeleo maalum Brexit

Sekione Kitojo
27 Aprili 2017

Kansela wa Ujerumani  Angela Merkel amesema leo bungeni,(27.04.2017) kuwa Uingereza isiishi katika mawazo ya kufikirika, kwamba itakuwa na haki zilezile kama wanachama wa Umoja wa Ulaya baada ya kujitoa katika Umoja huo.

https://p.dw.com/p/2c04r
Berlin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani akihutubia bunge kuhusu msimamo wa EU kuhusu BrexitPicha: Reuters/H.Hanschke

Bi Merkel ameyasema  hayo  katika bunge  la  Ujerumani  , na  kuongeza  kwamba  taifa  ambalo  ni mshirika  tu  halitakuwa  na  haki kama taifa mwanachama, amesema Merkel kabla  ya  mkutano  mjini  Brussels  kuhusiana  na  Brexit siku  ya  Jumamosi. 

"Hii inawezekana  kuonekana  kama  kujipendelea, lakini  ni  lazima niseme wazi kwasababu  baadhi  ya  watu  nchini  Uingereza wanaonekana  kuwa  na  ndoto  za  mchana  kuhusiana  na  suala hili," Merkel  amesema  bungeni  leo...

Berlin Vereidigung von Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier
Bunge la Ujerumani , BundestagPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

"Wapenzi ndugu  zangu, huenda  mnaweza  kufikiria  kwamba  hili  ni jambo  la  kawaida tu. Lakini  kwa  bahati  mbaya  naweza  kusema wazi  kwamba  napata  hisia  baadhi  ya  watu  nchini  Uingereza wana mawazo  ya  kufikirika. Hii  ni  kupoteza  wakati."

Großbritannien Premierministerin Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/AA/K. Green

Merkel  amesema  mazungumzo  kuanzia  mwanzo  kabisa  ni  lazima yajumuishe  majukumu  ya  kifedha  ya  Uingereza, ikiwa  ni  pamoja na baada  ya  kujitoa  kutoka  Umoja  huo. Pia  amesema masharti ya  kujitoa  kwa  Uingereza   kutoka  Umoja  wa Ulaya  ni  lazima yafikiwe  katika  njia  inayoridhisha  kabla  ya  majadiliano  kuingia katika  uhusiano  wa  hapo  baadaye  na  Umoja  huo, mtiririko ambao Merkel  ameuita , usioweza  kubadilishwa  tena.

Mpango wa majadiliano

"Mpango wa mtiririko  wa  jinsi tutakavyolishughulikia  suala  hili  uko wazi na  hautakuwa  hata  hivyo kila  mara  rahisi  kuufuata, tunaweza  tu  kufikia makubaliano  juu  ya  uhusiano wa  hapo  baadaye  na  Uingereza mara  masuala  yote  ya  kujitoa  yatakapotatuliwa kwa njia inayoridhisha. Hii  ina  maana  kwamba  ni  haraka  kiasi  gani Uingereza  inaweza  kufikia  suluhisho  sahihi, ndipo tutakapoyaangalia  matakwa  yao  ya  kuzungumzia  suala  la uhisiano  wa  hapo  baadaye  katika  yao  na  Umoja  wa Ulaya katika  majadiliano  ya  kujitoa. Lakini  kwanza  tunalazimika  kufamu ni  vipi  Uingereza  inauona  uhusiano wake  nasi."

Viongozi  wa mataifa  mengine  27  wanachama  wa  Umoja  wa Ulaya  watakutana  Aprili 29 kuweka  misingi  ya  Umoja  huo , licha ya  kwamba  mazungumzo  hayo  yataanza  rasmi mwezi  wa  Juni mwaka  huu. Umoja  wa  ulaya  umeimarisha  mkakati  wake , ukitoa madai  mapya  kuhusiana  na  huduma  za  kifedha, uhamiaji  na fedha  ambazo  Uingereza  inapaswa  kulipa  kabla  ya  kufikisha mwisho  uanachama  wake  katika  Umoja  huo  uliodumu  kwa miaka  44.

"Majadiliano  ya  kujitoa bila  shaka  yatahitajika kufikiwa  kwa makubaliano  makubwa  baina  ya Umoja  wa  Ulaya  pamoja  na Uingereza  binafsi  katika  miaka  miwili  ijayo. Nafikiri  hilo  halina shaka  kabisa."

Belgium EU Brexit
Viongozi wa chama cha UK Independence UKIP cha Uingereza wakisherehekea kuzinduliwa kwa kifungu 50 cha majadiliano ya kujitoa katika Umoja wa UlayaPicha: picture alliance/AP Photo/T.Monasse

Uturuki pia yaonywa

Kuhusiana  na  suala  la  uhisiano  kati  ya  Umoja  wa  ulaya  na Uturuki , Merkel  amesema , uhusiano  huo umedhoofika  pakubwa kutokana  na  hatua  zilizochukuliwa  na  serikali  ya  rais Recep Tayyip Erdogan. Merkel  ameeleza  wasi  wasi  wake  kwamba  kura ya  maoni  iliyofanyika  nchini  Uturuki Aprili 16  haikufanywa  katika mazingira ya usawa. Ameionya  Uturuki kuheshimu  haki  za  raia kwa  misingi  ya  taifa  linaloheshimu  katiba. Pia  amesema atatumia  mkutano  pamoja  na  viongozi  wenzake  wa  Umoja  wa ulaya  mjini  Brussels  siku  ya  Jumamosi  kujadili  hatua  za kuchukua  kuelekea  Uturuki.

Mwandishi: Sekione  Kitojo /afpe /dpae

Mhariri: Yusuf , Saumu