1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel apanga mkutano maalum wa EU kujadili uhamiaji

Iddi Ssessanga
17 Juni 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapanga kuitisha mkutano maalumu na mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya yanayoathiriwa na mgogoro wa uhamiaji wakati kukiwa na mvutano kati yake na waziri wamambo ya ndani Horst Seehofer.

https://p.dw.com/p/2zi0n
Deutschland Angela Merkel
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Schreiber

Mkutano huo huneda ukafanyika kabla ya mkutano wa kawaida wa kilele wa viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya uliopangiwa Juni 28 na 29. Merkel anapanga kujadili suala hilo pamoja na viongozi wa mataifa yakiwemo Ugiriki, Italia na Austria, limeripoti gazeti linaloongoza kwa mauzo nchini Ujerumani la Bild, likinukuu vyanzo kutoka mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya.

"Hadi sasa hakuna kilichoamuliwa - tuko katika awamu ya mipango," chanzo kutoka serikali ya Italia kililiambia gazeti la Bild. "Pia bado haijajulikana wazi ni lini mkutano huo maalumu wa kilele utakapofanyika." Haikujulikana mara moja iwapo Uhispania na mataifa ya kanda ya Balkan yatashiriki katika mkutano huo. Msemaji wa serikali ya Ujerumani hakupatikana mara moja kuzungumzia ripoti hiyo.

Msimamo wa Merkel umekuwa kutafuta suluhisho la ngazi ya Umoja wa Ulaya kuhusu uhamiaji haramu wakati wa mkutano wa kilele mjini Brussels mwishoni mwa mwezi, na ameomba kuwepo na uvumilivu.

Berlin, Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) spricht mit Horst Seehofer (CSU)
Kansela Merkel na waziri wake wa mambo wa ndani Horst Seehofer.Picha: picture-alliance/dpa/M.Kappeler

Mwiba kwa Merkel

Kwa muda mrefu, Seehorfer, veterani wa chama cha Christian Social Unioni (CSU) - ambacho ni chama ndugu na chama cha Merkel cha Christian Democratic Union (CDU) - amekuwa mwiba kwa upande wa Merkel na ametishia kumkaidi kansela na kuendelea na utekelezaji wa mipango yake siku ya Jumatatu, kuwarejeshea wahamiaji haramu mpakani mwa Ujerumani.

Katika ripoti tofauti ya Bild, alikanusha kuwa alikuwa anajaribu kuuvunja muungano wa kihafidhina. " Hakuna yeyote ndani ya CSU anataka kumpindua kansela, kuvunja ushirika wa CDU/CSU au kuvunja serikali ya muungano kati ya CDU/CSU na chama cha Social Democratic SPD," alisema Seehorfer.

"Tunataka hatimaye tupate suluhisho endelevu kwa wahamiaji waliokataliwa kutoka mipaka yetu," aliongeza.

Lengo la Seehorfer la kuzifanyia mabadiliko na kuziimarisha sheria za uhamiaji za Ujerumani linahusisha kuwakataa wahamiaji ambao tayari wamesajiliwa katika taifa lingine la Umoja wa Ulaya, wale wasio na nyaraka au wale wanaotaka kuruhusiwa kungia tena baada ya kufukuzwa.

Deutschland Sebastian Kurz, Bundeskanzler Österreich & Horst Seehofer in Berlin
Kansela wa Austria Sebastian Kurz akiwa na waziri Horst Seehofer. Wawili hao wana maono sawa kuhusu uhamiaji barani Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Changamoto inayohitaji jibu la Ulaya

Merkel anapinga mipango hiyo, akisema itawatwika mzigo wa wakimbizi majirani za Ujerumani na kudhoofisha mshikamano wa Umoja wa Ulaya. Katika ujumbe wa kila wiki kwa njia ya vidio siku ya Jumamosi, Merkel aliuelezea uhamiaji kama "changamoto ambayo pia inahitaji jibu la  Ulaya."

"Na naichukulia mada hii kuwa mojawapo ya masuala muhimu kwa mshikamano wa Ulaya," aliongeza.

Seehorfer ni mkosoaji mkubwa wa uamuzi wa Merkel kufungua mipaka ya Ujerumani kwa mamia ya maelfu ya watafuta hifadhi mwaka 2015. Kutoridhika na uamuzi huo kulisababisha kupungua kwa uungwaji mkono kwa vyama vya kihafidhina vya jadi na kuongezeka kwa umaarufu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD), ambacho kilishinda viti 94 kati ya jumla ya viti 709 vya ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, rtre

Mhariri: John Juma