1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel apiga hatua ya muhimu katika mkutano wa G20

20 Juni 2012

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyapuuza maoni yaliyotolewa na wakosoaji juu ya mpango wake wa kuimarisha sarafu ya Euro. Merkel ameonyesha kuushikilia msimamo wake katika mkutano wa G20.

https://p.dw.com/p/15Icd
Kansela Angela Merkel akizungumza katika mkutano wa G20
Kansela Angela Merkel akizungumza katika mkutano wa G20Picha: picture-alliance/dpa

Angela Merkel sasa anaweza kusema kwamba amemalizana na mkutano wa G20. Merkel alisimama kidedea na hakubabaishwa na maoni yaliyotolewa na Marekani na hasa nchi zinazoendelea. Inaelekea kwamba Merkel anaushikilia msimamo wake na hayuko tayari kushinikizwa ili atoe ahadi zaidi kwa Ugiriki.

Badala yake Merkel alipokuwa Los Cabos, Mexico, kwa mara nyingine alisema wazi kwamba anataka Ugiriki ifuate makubaliano yaliyofikiwa mara moja. Ingawa suluhu ya mzozo wa fedha unaoikumba kanda ya Euro bado haijaweza kupatikana, nchi za Ulaya zimeweza kuonyesha kwamba zina msimamo wa pamoja. Bila shaka, matokeo ya uchaguzi wa Ugiriki yalikuwa miongoni mwa sababu zilizofanya nchi hizo ziungane.

Nchi za Ulaya zaungana kupambana na mgogoro wa kiuchumi

Ni mafanikio machache tu yaliyopatikana katika mkutano wa uchumi uliofanyika Los Cabos. Mataifa yanayotumia sarafu ya Euro yameafiki kufanya juhudi zaidi ili kuimarasha sarafu hiyo ili yaweze kupata imani katika masoko ya hisa.

Kwa upande wake, nchi zinazounda kundi la G20 zimekiri kwamba nchi za Ulaya tayari zimeshapiga hatua katika kuutatua mgogoro wa sarafu ya Euro. Rais Barack Obama wa Marekani, ambaye yuko mstari wa mbele katika kuukosoa mpango wa Merkel wa kubana matumizi, ameeleza kuwa ameona kwamba kuna mabadiliko ya fikra miongoni mwa raia wa Ulaya na hivyo amesema kuwa sasa anakubaliana na njia ambayo Ulaya imeamua kuifuata ili kujiondoa katika mgogoro wa kiuchumi.

Rais Barack Obama akizungumza katika mkutano wa G20
Rais Barack Obama akizungumza katika mkutano wa G20Picha: AP

Ujumbe mkubwa kutoka Los Cabos ni kwamba kwa sasa nchi za Ulaya pamoja na Marekani zitashirikiana katika kukuza uchumi na kupunguza mvutano kati ya masoko ya kimataifa ya fedha.

Mada muhimu kuzungumziwa mwakani?

Ujumbe wa namna hii ndio ambao watu wanatarajia kuusikia kutoka kwa nchi za G20. Kundi hili linaloundwa na nchi 20 zilizoendelea zaidi kiviwanda linatengeneza asilimia 80 ya pato jumla la uchumi wa dunia. Nchi hizo pia zinaendesha robo tatu ya biashara ya dunia huku raia wake wakiwa theluthi mbili ya idadi ya watu waishio duniani. Lakini katika kulinganisha umuhimu wa kundi la nchi hizi 20 na shughuli zinazofanywa na kundi hilo, inaonekana kwamba kundi la G20 ni kama mamba asiyekuwa na meno. Kazi kubwa iliyoko mbele ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro kwa sasa ni kuuokoa uchumi wa Uhispania ambao nao unasuasua. Hilo likifanikiwa, basi huenda mkutano ujao wa G20, ambao utafanyika mwakani nchini Urusi, ukazungumzia mada muhimu ambazo mara hii zilizungumziwa kwa juu juu tu. Mada hizo ni kama vile ukuaji wa kiuchumi unaojali mazingira pamoja na usalama wa chakula.

Mkutano wa G20 mwaka huu haukujadili mada nyingine muhimu
Mkutano wa G20 mwaka huu haukujadili mada nyingine muhimuPicha: AP

Mwandishi: Mirjam Gehrke/ZPR

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Khelef