1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aunga mkono sheria ya kurejeshwa makwao wakimbizi

9 Januari 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana Ijumaa (08.01.2016)amesema anaunga mkono mabadiliko ya sheria ili kufanya rahisi kuwarejesha makwao wahamiaji ambao watahusika katika uhalifu.

https://p.dw.com/p/1Haav
Mainz - Klausurtagung des CDU-Bundesvorstandes
Kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/F. Erichsen

Hii ni baada ya maafisa kusema wengi wa washukiwa wa ghasia za wakati wa mkesha wa mwaka mpya zilizowashitua wengi ni watu wanaoomba hifadhi.

Chini ya sheria za sasa, waombaji hifadhi wanaweza tu kulazimishwa kurejeshwa makwao iwapo watahukumiwa kifungo jela kwa takriban miaka mitatu, na iwapo maisha yao hayatakuwa hatarini katika nchi zao za asili.

Deutschland Neuhjarsempfang des Bundespräsidenten Gruppenfoto
Kansela Merkel katika mkutano na maafisa wa chama chake mjini MainzPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Wahamiaji kupoteza haki ya kukaa nchini

Baada ya wanawake kadhaa mjini Cologne kushambuliwa kwa kunyanyaswa kingono katika mkesha wa mwaka mpya na kundi la wanaume, walioelezwa na watu walioshuhudia kuwa wengi wao ni Waarabu wanaoonekana kuwa wana asili ya Afrika kaskazini --Merkel amesema muda umewadia sasa kujiuliza "Ni wakati gani unaweza kupoteza haki yako ya kukaa nasi?"

"Tunapaswa kujiuliza iwapo ni muhimu kuwaondoa mapema, kuliko ilivyo hivi sasa, na naweza kusema kwamba kwangu mimi, tunapaswa kuwaondoa mapema," kansela amesema.

Deutschland Hauptbahnhof Vorplatz in Köln
Eneo la tukio katika kituo kikuu cha treni mjini ColognePicha: Reuters/W. Rattay

"Tunapaswa kufanya hivyo kwa ajili yetu, na kwa wakimbizi wengi ambao hawakuwapo wakati wa tukio hilo mjini Cologne," ameuambia mkutano wa maafisa wa chama chake katika mji wa kusini magharibi nchini Ujerumani wa Mainz.

Merkel tayari alikwisha toa wito wa kuwapo majadiliano juu ya iwapo kuimarisha sheria ya kuwarejesha watu makwao, lakini hii ni mara ya kwanza amekuwa wazi kwa kuunga mkono mabadiliko katika sheria kama hiyo.

Katika hali ya kujitokeza kwa taarifa ambazo zimewashitua Wajerumani na kusababisha kujiuzulu kwa mkuu wa polisi wa mji wa Cologne, wanawake walionekana katika mkesha wa mwaka mpya wakilazimika kulikimbia kundi la wanaume wapatao 1,000 waliokuwa wakiwatomasa, kuwatukana na wizi katika tukio la ghasia zilizoambatana na ulevi.

Mkuu wa polisi asimamishwa kazi

Hadi jana Ijumaa (08.01.2016), polisi ya mjini Cologne ilipokea zaidi ya malalamiko ya kihalifu 200, mengi yao kuhusiana na uhalifu wa kingono kuanzia kushikwa shika hadi matukio mawili ya ubakaji , limeripoti gazeti la Spiegel la mtandaoni.

Maafisa kutoka chama cha kihafidhina cha kansela Merkel cha Christian Democratic, wanaokutana mjini Mainz mwishoni mwa juma hili, wanatarajiwa kupendekeza kwamba wahamiaji watakaofungwa kwa kipindi cha miaka mitatu nchini Ujerumani wanapaswa kurejeshwa walikotoka.

Deutschland Köln Proteste nach sexuellen Übergriffen
Wanawake waliandamana kupinga unyanyasaji huo kingono mjini ColognePicha: Reuters/W. Rattay

Mkuu wa polisi ya mjini Cologne Wolfgang Albers , mwenye umri wa miaka 60, alisimamishwa kazi kwa kushindwa kuzuwia ghasia zilizofanywa na kundi la wanaume katika sherehe za mkesha wa mwaka mpya.

Mkuu huyo wa polisi amesimamishwa kazi ili kurejesha imani ya wananchi katika jeshi hilo, amesema Ralf Jaeger, waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine-Westphalia.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid