1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel autaka Umoja wa Ulaya kuziimarisha benki

6 Oktoba 2011

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuimarisha sekta ya benki ili kusaidia kuepusha mzozo wa madeni katika eneo linalotumia sarafu ya euro.

https://p.dw.com/p/12mu7
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: AP

Kansela Merkel alisema kuzisaidia benki ni hatua halali kama viongozi wote wa kanda ya euro watakuwa na mtizamo mmoja. Alikuwa akizungumza katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels baada ya kukutana na rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.

Kauli ya Merkel imekuja baada ya Ufaransa na Ubelgiji kukubali kuisaidia kifedha benki ya Dexia, benki ya kwanza ya Ulaya kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na mzozo wa madeni katika eneo linalotumia sarafu ya euro, na ambayo ililazimika kupewa fedha mnamo mwaka 2008 ili isifilisike.

Mapema leo Barroso amewasilisha pendekezo la hatua ya pamoja itakayochukuliwa na nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuiimarisha kifedha sekta ya benki.

Ugiriki yahitaji kusaidiwa

Mzozo wa madeni ulioanzia nchini Ugiriki, umeziathiri pia Ireland na Ureno na kuziweka katika hali ngumu Italia na Uhispania. Mzozo huo pia unatishia kuizamisha kanda nzima ya euro huku benki zinazoguswa moja kwa moja na tatizo hilo zikishindwa kupata fedha za kuendeshea shughuli zao. Bi Merkel ameitaka Italia iendelee kutekeleza hatua kali za kufunga mikaja baada ya wakala wa Moody's unaotathimini uwezo wa nchi kulipa madeni, kushusha uwezo wa Italia wa kulipa madeni yake.

Kuhusu tatizo la madeni la Ugiriki kansela Merkel alisema, "Ujerumani imeridhia kuupanua mfuko wa uokozi. Sharti sasa tutathimini kama Ugiriki inastahili kupewa kiwango kikingine cha mkopo wakati huu. Hilo lazima lizingatiwe kukiwa na haja. Naona umuhimu mkubwa wa Ugiriki kubakia sehemu ya kanda ya euro na lazima ipewe nafasi ya kujikwamua na kujisimamia yenyewe."

Mfuko wa uokozi uungwe mkono

Kansela Merkel pamoja na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, wamezihimiza Slovakia na Uholanzi ziuunge mkono mfuko maalum wa fedha wa kuziokoa nchi zinazokabiliwa na madeni katika eneo linalotumia sarafu ya euro.

Merkel Barroso EU Finanzkrise Krise Schuldenkrise Brüssel Bankenkrise
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kushoto, na kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel BarrosoPicha: dapd

Barroso alisema, "Ni kwa kupitia tu Ulaya mpya, Ulaya iliyopanuka na uongozi wa Umoja wa Ulaya uliojitolea kwa dhati, ndipo tutakapojenga uaminifu katika uwezo wetu wa kuchukua hatua. Tunaweza kuhakikisha Ulaya ina umuhimu duniani na inaweza kuyalinda masilahi na maadili yake; soko huru la kiuchumi linalotilia maanani ustawi wa kijamii."

Mkutano wa Berlin

Hii leo kansela Merkel anakutana na Mkuu wa benki kuu ya Ulaya, Jean-Claude Trichet, wakuu wa shirika la fedha la kimataifa, IMF, benki ya dunia, shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, na shirika la kazi ulimwenguni, ILO, mjini Berlin kujadili mageuzi katika mfumo mzima wa fedha wa kimataifa. Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, na mwenzeke wa Ufaransa, Francois Baroin, watashiriki pia kwenye kikao hicho.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman