1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel awasihi wabunge kuunga mkono uokozi wa Ugiriki

Admin.WagnerD17 Julai 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameliambia bunge kuwa mpango wa tatu wa uokozi kwa Ugiriki ulikuwa mgumu kwa pande zote lakini ndiyo ulikuwa fursa bora na ya mwisho kutatua mgogoro wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1G0W4
Deutschland Bundestag Sondersitzung Griechenland
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Kansela Merkel amesema hakuna shaka kwamba makubaliano hayo yaliyofikiwa siku ya Jumatatu asubuhi yalikuwa magumu, lakini amewasihi wabunge kuunga mkono majadiliano aliyoyaitia jaribio la mwisho kutatua mgogoro wa madeni ya Ugirki. Amesema kutoisaidia Ugiriki utakuwa uzembe, kutakuwa kukosa uwajibikaji, na kunaweka hatari ya kusababisha machafuko.

Baada ya makubaliano ya awali siku ya Jumatatu, serikali ya Ujerumani laazima ipate idhini ya bunge ili kuendelea na mazungumzo yanayotazamiwa kuwa magumu kujadili kwa kina mpango huo wa uokozi wa miaka mitatu wenye thamani ya euro bilioni 85. Merkel amekiambia kikao cha bunge kinachoendelea mjini Berlin kuwa wabunge wanakabiliwa na uamuzi juu ya Ulaya imara na kanda ya sarafu ya euro iliyo imara.

Kansela Merkel akilihutubia bunge siku ya Ijumaa.
Kansela Merkel akilihutubia bunge siku ya Ijumaa.Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Matukio ya kusisimuwa

"Matukio ya kusisimua yaliyotokea Ulaya katika siku zilizopita hayawezi kupuuzwa. Siyo tu kwa sababu ya mashauriano yasiyokoma katika kundi la Euro la mawaziri wa fedha na wakati wa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na serikali mwishoni mwa wiki, jambo ambalo sijawahi kulishuhudia namna hii kabla, lakini siku hizi zilisisimuwa kwanza kutokana na nchi ambayo ndiyo ilikuwa mada ya fikira zetu na mashauriano: Ugiriki.

Hebu tutafakari kwa muda ingekuwaje, ikiwa wastaafu wa Ujerumani wangekuwa wanahangaika kwenye foreni mbele ya mabenki yaliyofungwa kusubiri pensheni yao ya kila wiki ya euro 120. Hili linatupa wazo na jinsi gani hali ilikuwa inasisimuwa nchini Ugiriki na hatari kiasi gani ilikuwa inaikabili nchi hiyo pamoja na Ulaya, wakati wakuu wa nchi na serikali walipokutana siku ya Jumapili," amesema Merkel wakati akifungua mjadala bungeni.

Ni uzembe na kutowajibika kuiacha Ugiriki

Uokozi wa Ugiriki siyo jambo linalopendelewa sana miongoni wa wahafidhina wa Merkel na kansela huyo anatambuwa wasiwasi juu ya ufanisi wa mpango huo. Lakini amesema "utakuwa uzembe mkubwa na hata kukosa uwajibikaji ikiwa hawatajaribu njia hiyo. Ameongeza kuwa Ugiriki ingekabiliwa na machafuko makubwa iwapo ingelazimishwa kuondoka katika kanda ya euro, na kumlaumu waziri mkuu wa nchi hiyo Alexis tsipras kwa kuharibu imani katika uchumi wa taifa lake.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble ameelezea mashaka juu ya iwapo mpango huu wa tatu kweli utakuwa na ufanisi, ingawa alisema ataupigia kura ya ndiyo na kuwasihi wahafidhina wenzake kuunga mkono. Wabunge kutoka muungano wa wahafidhina tayari na washirika wao serikali, chama cha Social Democrat SPD, waliunga mkono kwa wingi hatua ya kuanzisha mazungumzo na Athen katika kura za majaribio jana Alhamisi.

Kansela Merkel na naibu wake Sigmar Gabriel wakifuatilia mjadala bungeni.
Kansela Merkel na naibu wake Sigmar Gabriel wakifuatilia mjadala bungeni.Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Matokeo hayo yanaashiria kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa Merkel kupata idhini ya bunge huku baadhi ya wabunge wa upinzani pia wakitarajiwa kuunga mkono. Lakini mtazamo hauko sawa nchini kote. Gazeti linaloongozwa kwa mauzo la Bild, limetoka na kichwa cha habari cha "Sababu saba kwa nini Bunge linapaswa kupiga kura ya hapana, na kuanisha kuwa kujiondoa kwa Ugiriki ndiyo suluhisho bora, na "wajukuu zetu watalipa" miongoni mwa sababu hizo.

Bunge la Ugiriki liliidhinisha mpango huo mpya mapema siku ya Alhamisi, na baadaye benki kuu ya Ulaya iliongeza ufadhili wa dharura kuepusha kuporomoka kwa mfumo wa benki wa nchi hiyo. Mawaziri wa fedha wa kanda euro pia waliidhinisha mkopo wa dharura wa euro bilioni 7, na kuiepushia Ugiriki kushindwa kulipa deni lake kwa ECB hapo Jumatatu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman