1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azuru kambi ya wakimbizi Uturuki

23 Aprili 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumamosi (23.04.2016) ametembelea kambi ya wakimbizi mpakani mwa Uturuki na Syria kwa lengo la kuimarisha makubaliano ya wahamiaji yaliotingwa na wasi wasi wakimadili na kisheria

https://p.dw.com/p/1IbTJ
Kansela Angela Merkel wakati alipowasili Gaziantep Uturuki akiwa pamoja na Makamo wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Frans Timmermans (kushoto) Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk (katikati) na kupokelewa na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu. (23.04.2016)
Kansela Angela Merkel wakati alipowasili Gaziantep Uturuki akiwa pamoja na Makamo wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Frans Timmermans (kushoto) Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk (katikati) na kupokelewa na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu. (23.04.2016)Picha: picture alliance/dpa/S. Kugler/Bundesregierung

Merkel ambaye ameandamana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na Makamo wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Frans Timmermans amekwenda kwenye kambi ya Nizin nambari mbili karibu na Gaziantep mara baada ya kuwasili kusini mashariki mwa Uturuki.

Bango kubwa lililowekwa kwenye mlango wa kuingia kwenye kambi hiyo yenye kuhifadhi wakimbizi 5,000 lilikuwa linasomeka "Karibu Uturuki nchi ambayo inajivunia kuwa mwenyeji wa wakimbizi wengi kabisa duniani"

Lengo la ziara hiyo ni kupigia upatu makubaliano yenye thamani ya euro bilini sita ya kuwarudisha Uturuki wahamiaji wanaowasili Ugiriki bila ya vigezo vinavyostahiki makubaliano ambayo yanashutumiwa na mashirika ya haki za binaadamu,shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Umuhimu wa kutekelezwa makubaliano

Fedha hizo zinatarajiwa kuisaidia Uturuki kuboresha mazingira ya wakimbizi milioni 2.7 inaowapa hifadhi.

Kansela Angela Merkel wakati alipopokelewa katika kambi ya wakimbizi ya Nizip. (23.04.2016)
Kansela Angela Merkel wakati alipopokelewa katika kambi ya wakimbizi ya Nizip. (23.04.2016)Picha: picture alliance/dpa/S. Suna

Uhusiano wa kidiplomasia uko kwenye mvutano kufuatia onyo la Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwamba makubaliano hayo ya kudhibiti wimbi la wakimbizi kuingia Ulaya yatasambaratika iwapo Umoja wa Ulaya haitotekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo ya kuruhusu raia wa Uturuki kusafiri bila ya visa katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya umeahidi kuwasilisha pendekezo hilo la Uturuki hapo Mei nne iwapo Uturuki itatimiza wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano hayo lakini mashaka yamekuwa yakiongezeka kuhusiana na suala la usalama kwamba limekuwa likiwekwa kando ili kuharakisha ombi hilo la Uturuki.

Merkel apongezwa na kushutumiwa

Hapo Jumamosi Rais Barack Obama wa Marekani amepongeza uongozi wa "kishujaa" wa Merkel katika kushughulikia mzozo wa wakimbizi wa Syria.

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Navutoglu katika kambi ya wakimbizi ya Nizip. (23.04.2016)
Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Navutoglu katika kambi ya wakimbizi ya Nizip. (23.04.2016)Picha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/S.Kugler

Lakini Waziri Mkuu wa Hungary Victor Orban amesema "umoja wa Ulaya imeuzwa kwa Uturuki " na kwamba athari zake " ni vigumu kuzitabiri" na kuongeza kwamba "Usalama wa Umoja wa Ulaya hauwezi kuwa katika mikono ya mataifa yalioko nje ya Ulaya."

Merkel amesema ziara hiyo ya Uturuki ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa makubaliano hayo ya wahamiaji na kujadili hatua zinazofuatia halikadhalika kutathmini mazingira yanayowakabili wale waliokimbia vita vya miaka mitano nchini Syria.

Haki za binaadamu zisifumbiwe macho

Judith Sunderland naibu mkurugenzi wa shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch kwa Ulaya amesema badala ya kutembelea kambi ya wakimbizi iliosafishwa ujumbe huo ulikuwa unapaswa kwenda kituo cha mahabusu chenye watu waliorudishwa kwa maonevu kutoka Ugiriki.

Wakimbizi katika kambi ya Gaziantep wakisubiri kuwasili kwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.(23.04.2016)
Wakimbizi katika kambi ya Gaziantep wakisubiri kuwasili kwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.(23.04.2016)Picha: picture alliance/dpa/S. Suna

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International hapo Ijumaa pia limeuhimiza ujumbe huo wa Ulaya "kutofunga macho yao kwa orodha ya ukiukaji wa haki za binaadmu wanaokabiliana nao wakimbizi" nchini Uturuki na kurudia malalamiko iliyoorodhesha ya Wasyria waliopigwa risasi na askari wa Syria.

Viongozi hao wa Umoja wa Ulaya watetembelea pia kituo cha kuhifadhi watoto kabla ya kuwa na mazungumzo na kukamilisha ziara yao hiyo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP

Mhariri : Iddi Ssessanga