1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azuru Mali

10 Oktoba 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameanza ziara yake Barani Afrika kwa kutua nchini Mali, na kutaka uungwaji mkono zaidi katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya na wafanyabiashara wa madawa hayo waliomo nchini humo.

https://p.dw.com/p/2R4ek
Kanzlerin Merkel in Afrika Mali
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Ziara ya Merkel barani Afrika inaangazia namna ya kukabiliana na wimbi la uhamiaji wanaoingia barani Ulaya huku ikilenga pia kurejesha sifa yake nyumbani Ujerumani. 

Ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusiana na kile anachotaka kitiliwe maanani zaidi katika vita hivyo, lakini Kansela Merkel amesema nchi yake itaimarisha mahusiano na Mali, hususan kwenye masuala ya usalama kwenye eneo lake la Kaskazini kwa kukabiliana na kundi la wapiganaji wa itikadi kali. 

Merkel, ambaye bado hajaweka wazi iwapo atagombea tena ukansela kwa mara ya nne kwenye uchaguzi utaofanyika mwakani, ameshuhudia kushuka kwa umaarufu wake kutokana na sera kuelekea wakimbizi na waomba hifadhi, kutokana na hatua yake ya mwaka jana ya kuruhusu kiasi cha wahamiaji milioni moja, wengi wao wakiwa kutoka Mashariki ya Kati, kuingia Ujerumani.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM, Mali ni moja ya nchi zinazoshika nafasi kumi za juu katika kutoa wahamiaji wanaoingia Ulaya kupitia Italia kwa mwaka huu, huku njia nyingine za uuzwaji haramu wa wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika ya Magharibi zinazotumika zikipitia maeneo ya jangwani. 

Ujerumani ina zaidi ya askari 500 nchini humo, na baada ya mazungumzo yake na mwenyeji wake, Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali, Kansela Merkel amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Tuna nia ya dhati ya kuirejesha nchi kwene utangamano". 

Mali UN Blauhelmsoldaten
Askari wa kulinda usalama wa umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA kwa kiasi kikubwa ndio wanakabiliana na makundi ya itikadi kaliPicha: Getty Images/AFP/H. Kouyate

Merkel ambaye leo hii anazuru Niger na Ethiopia mnamo siku ya Jumanne, hakusema iwapo Ujerumani itatoa helikopta zaidi kama moja ya mikakati yake wa kuyasaidia majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliyomo nchini Mali, MINUSMA. Merkel amesema Ujerumani itaimarisha uungwaji mkono wake kwenye eneo la kilimo, pamoja na usalama kwenye eneo la Kaskazini la nchi hiyo, ambako kunadhaniwa kuwepo kwa makundi ya Kiislamu yanayoendelea kuibua wasiwasi kwenye eneo hilo.

Jeshi la Mali kwa kiasi kikubwa bado halipo kwenye eneo la jangwa lililopo nchini humo, pamoja na makubaliano yaliyosainiwa mwaka ajana yaliyolenga kuhakikisha kuwa linarejea kwa haraka, hatua inayoongeza shinikizo la vikosi vya Umoja wa Mataifa, MINUSMA kuendelea kuyazungukia maeneo ya ghuba yanayokabiliwa na wanamgambo na wapiganaji wa kundi la Kiislamu.

Merkel ameielezea Afrika yenye idadi ya watu ipatayo Bilioni 1.2 kama ndio tatizo la msingi katika suala la uhamiaji. Mwezi uliopita, alisema Umoja wa Ulaya ulitaka kuanzisha makubaliano yanayohusina na wahamiaji kwa kuzishirikisha nchi zilizopo Afrika ya Kaskazini, pamoja na Uturuki.   

Chini ya makubaliano hayo na Umoja wa Ulaya, Ankara ilikubali kuwarejesha wahamiaji na wakimbizi waliopitia bahari ya Aegean, kuingia nchini Ugiriki kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na raia wa Syria.

Ujerumani, Ufaransa na Italia kwa pamoja wamesema wanataka kuendeleza mahusiano ya karibu zaidi na Niger na Mali, ambazo wanaona kama ni washirika muhimu katika kukabiliana na suala la wahamiaji. 

Mwandishi: Lilian Mtono/AP/Rtre/AFPE.
Mhariri: Mohammed Khelef