1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel hakubadili sera ya wahamiaji

1 Oktoba 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza Jumamosi (01.10.2016) hakubadili mwelekeo wa sera yake ya wahamiaji kwa kuitetea kuwa ni fasaha na kuwaonya Wajerumani kutosahao historia yao.

https://p.dw.com/p/2QnVn
Deutschland Angela Merkel Bundeskanzlerin Flüchtling Selfie
Kansela Merkel akipiga picha na mhamiaji.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Merkel amesema hatua kubwa imepigwa katika suala la kushughulikia hali ya wakimbizi nchini na ametetea sera yake ya wakimbizi kuwa ina "ufasaha".Katika matamshi yaliochapishwa na gazeti la Ujerumani la "Sächsische Zeitung" amesema hakuna haja ya kubadili mwelekeo na kwamba hakufanya hivyo.Ameliambia gazeti hilo "Sikubadili sera yangu bali natengeneza sera.Sioni mabadiliko ya mwelekeo bali kazi inayahotajika kutekelezwa kwa ufasaha kwa miezi mingi inayokuja."

Chama cha Christian Demokrat (CDU) cha Merkel kimepata vipigo vya uchaguzi katika chaguzi mbili za majimbo mwezi uliopita wakati wapiga kura wakionyesha kuikataa sera yake ya kufungilia milango wahamiaji ukiwa umebakia mwaka mmoja tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Ujerumani.

Merkel ameliambia gazeti hilo amekuwa akifanya kazi tokea kipindi cha majira ya kiangazi kilichopita kutafuta "ufumbuzi ambao utakuwa na manufaa kwa Ujerumani na kwa Ulaya.".Hilo ikiwa ni pamoja na kulinda mipaka ya nje ya Ulaya na kupambana na sababu za kukimbia kwa wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati,Asia na Afrika.

Amesema "daima nimekuwa na wasi wasi na kutaka kuboresha ulinzi wa mipaka ya Umoja wa Ulaya na kushughulikia sababu zinazopelekea watu kukimbia ili kwamba kupunguza idadi ya wakimbizi."

Kulinda mipaka ya nje ya Ulaya


Merkel amekiri kwamba ilikuwa ni muhimu kujifunza kwamba mipaka ya nje ya Ulaya inapaswa kulindwa ili mtu aweze kuwa mliberali yaani huru kujiamulia kufanya akipendacho ndani ya Ulaya.Pia amesema kwamba Ujerumani inabidi ishighulikie kuratibu mchakato wa kukabiliana na kuwasili kwa wakimbizi nchini.Amesema "Lengo letu ni kuepuka kurudiwa kwa hali kama ile iliyotokea mwaka jana na kwa kweli tumepiga hatua kubwa katika kipindi cha miezi 12 iliopita."

Türkei Angela Merkel zu Besuch im Flüchtlingslager Nizip I
Kansela Angela Merkel baada ya kuwatembelea wakimbiziPicha: picture-alliance/dpa/Bundesregierung/S.Kugler

Merkel mara kwa mara amekuwa akishutumiwa kutokana na sera yake hiyo ya wakimbizi wakiwemo wanachama wenzake wa CDU kwa kuwa ni ya kiliberali mno.Shutuma hizo zimekuwa zikiendelea licha ya ukweli kwamba idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini imepunguwa sana mwaka huu kutokana pamoja na mambo mengine mkataba kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ambao unawarudisha wahamiaji wengi nchini Uturuki ili badala yake nchi hiyo ipatiwe msaada wa kifedha na kuridhiwa katika mambo mengine kadhaa.

Kansela amesema sasa ni muhimu kuharakishwa kurudisha nyumbani raia wasio wa Ujerumani ambao hawana vibali vya kuishi nchini.Amesema mkazo zaidi unapaswa kuwekwa katika utekelezaji wake na kutokana na kwamba wana wajibu wa kibinaadamu kwa wale wanaotaka hifadhi Ulaya baada ya kuvikimbia vita na ugaidi lazima wakubaliane kisheria mgao wao katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.Kauli ya Merkel inakuja wakati Hungary ikijiandaa kupiga kura katika kura ya maoni iwapo iruhusu Umoja wa Ulaya kuweka mgao huo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Wajerumani waielewe historia yao


Kansela huyo wa Ujerumani pia amesema Wajerumani wanatakiwa kuielewa vizuri zaidi historia yao wenyewe ili kuweka misingi sahihi kwa mustakbali wa nchi hiyo.Amesema ni muhimu kuifahamu historia kuhusu kuungana upya kwa Ujerumani katika miaka ya 1990 na kipindi cha kiza cha utawala wa Manazi.

Dresden
Mandhari ya mji wa Dresden.Picha: Fotolia/SeanPavonePhoto

Amewashutumu waandamanaji wa sera kali za mrengo wa kulia wanaoimba kauli mbiu ya uasi ya iliokuwa Ujerumani ya Mashariki "Sisi ndio wananchi " yaani ndio wenye maamuzi lakini pia amesema ni muhimu kuwasaidia wale wanaohisi wameachwa nyuma.

Siku hizi kauli mbiu hiyo mara nyingi husikika wakati wa maandamano ya kupinga wahamiaji.

Serikali ya Ujerumani iko katika hali kubwa ya tahadhari kabla ya kufanyika maadhimisho ya miaka 26 ya kuungana upya hapo Jumatatu katika mji wa mashariki wa Dresden.Mji huo ni maskani ya kundi linalopinga Uislamu la PEGIDA na umetingishwa na mashambulizi mawili ya mabomu moja likilenga msikiti wiki iliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuers/AP/DW

Mhariri : Bruce Amani