1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel : Jumamosi ni siku ya maamuzi ya mzozo wa Ugiriki

Admin.WagnerD26 Juni 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro barani Ulaya hapo Jumamosi ni muhimu sana na ndio utakaoamuwa suala la kufikiwa makubaliano ya kuinusuru Ugiriki.

https://p.dw.com/p/1FnlM
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipris katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. ( 25.06.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipris katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. ( 25.06.2015)Picha: Reuters/Y. Herman

Kufuatia siku ya kwanza ya Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya unaoendelea mjini Brussels Ubelgiji Merkel amesema mapema leo hii kwamba mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya inabidi waendelee na juhudi zao siku zinazokuja kwa sababu muda ndio huo unayoyoma.

Amesema viongozi wote wanaunga mkono wazo kwamba inapaswa kufanyika juhudi zote za kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Ugiriki kufikia Jumamosi.

Merkel amekaririwa akisema "Kuhusiana na mazungumzo na Ugiriki tumekubaliana kwamba kazi inabidi iendelee na taasisi tatu za mikopo na kwamba mkutano wa kundi la sarafu ya euro hapo Jumamosi utakuwa na umuhimu mkubwa sana wa kuamuwa kwa sababu muda unayoyoma.Tungelipenda mawaziri wa fedha na kundi la sarafu ya euro pamoja na taasisi hizo tatu na Ugiriki wafikie makubaliano na shauku hiyo imeelezwa bayana leo hii."

Kauli hiyo ya Merkel inakuja baada ya kushindwa tena kwa duru ya mazungumzo ya kanda ya sarafu ya euro hapo Ahamisi. Nchi 19 zinazotumia sarafu hiyo ya pamoja zimeshindwa tena kufikia makubaliano ya kunusuru Ugiriki kufilisika na madeni ambapo nchi hiyo ilikuwa inataraji ingelipatiwa mkupuo mwengine wa mkopo uliobakia wa euro bilioni 7.2 na Shirika la Fedha la Kimataifa.

Kutoka kwa Ugiriki Umoja wa Ulaya

Ugiriki inahitaji mikopo ya kulipa deni lake la euro bilioni 1.7 kwa IMF kufikia Juni 30.Kushindwa kufanya hivyo kutapelekea kufilisika kwa nchi hiyo jambo ambalo wachambuzi wanahofia kutailazimisha nchi hiyo kutoka kwenye kanda ya sarafu ya euro na pengine hata Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipris (kulia) na Rais wa Halmashauri Kuu yaUmoja wa Ulaya Jean Claude Juncker katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. ( 25.06.2015)
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipris (kulia) na Rais wa Halmashauri Kuu yaUmoja wa Ulaya Jean Claude Juncker katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. ( 25.06.2015)Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Kutoka kwa Ugiriki kwenye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya kutakuwa hakuepukiki iwapo serikali ya nchi hiyo na wakopeshaji wake watashindwa kupata ufumbuzi wa mzozo wa madeni wa Ugiriki katika kipindi cha siku tano.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Ujerumani Guenther Ottinger amesema watafanya kila wawezalo hadi hapo tarehe 30 Juni ili kwamba Wagiriki waonyeshe kuwa wako tayari kufanya mageuzi.

Madai ya ajabu

Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varaoufakis amesema nchi yake imefanya kila iwezalo kutimiza kile alichokiita "madai ya ajabu" yaliyotolewa na wakopeshaji wake na kwamba imeazimia kuendela kubakia kuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis katika mkutano wa mawaziri wa fedha kanda ya sarafu ya euro mjini Brussels. (25.06.2015)
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis katika mkutano wa mawaziri wa fedha kanda ya sarafu ya euro mjini Brussels. (25.06.2015)Picha: Reuters/Philippe Wojazer

Lakini amesema Ugiriki haitokubali ufumbuzi wa mzozo wake wa madeni ambao inauona kuwa hauna manufaa.

Akiandika kwenye mtandao wa Twitter mapema Ijumaa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Donald Tusk amefuta uwezekano wa kufanyika kwa mkutano maalum wa kilele wa viongozi wa kanda ya sarafu ya euro kama ule aliouitisha Jumatatu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/DW

Mhariri : Iddi Ssessanga