1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kugombea tena kiti cha kansela kwa tikiti ya CDU/CSU

Oumilkheir Hamidou
3 Aprili 2017

Angela Merkel ateuliwa rasmi kugombea kiti cha kansela kwa tiketi ya vyama ndugu vya CDU/CSU, maandamano ya umma nchini Rumania na miaka 25 tangu yalipotiwa saini makubaliano ya Maastricht ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2X642
Angela Merkel und Horst Seehofer
Picha: Getty Images/J. Simon

Tunaanzia lakini Munich ulikofanyika mkutano wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU. Wakuu wa vyama hivyo ndugu wamemteuwa rasmi Angela Merkel agombee wadhifa wa kansela kwa mara ya nne. Gazeti la "Mittelbayerische" linaandika; "Wakuu wa vyama ndugu vya CDU/CSU wameingiwa na wahka kutokana na kuzidi imani ya wapiga kura kwa chama cha Social Democrat tangu Martin Schulz alipoteuliwa kugombea kiti cha kansela. Kwamba SPD wanazidi kupanda ni sehemu tu ya tatizo.

Kishindo kikubwa zaidi ni ile hali kwamba Martin Schulz pia amempita Angela Merkel. Umashuhuri wa mgombea huyo wa SPD ndio unaogubika udhaifu wa kansela. Umashuhuri wa kansela umefifia kufuatia mzozo wa wakimbizi. Seehofer daima alikuwa akimuonya kansela kuhusu hilo, bila ya kufanikiwa. Matamshi  yake makali nayo pia yamechangia katika kupungua umashuhuri wa kansela."

Seehofer afuata njia hatari

Gazeti la "Der neue Tag" linauchambua mkutano wa Munich kama ifuatavyo: "Mkutano huo kubuni mbinu ulioitishwa na viongozi wa CDU/CSU ili kujiandaa kwaajili ya uchaguzi mkuu mtu anaweza kuutaja kwa muhtasar kuwa ni mkutano wa " kupatana, kufurahishana na kuwekeana kikomo. Mara nyingi CSU wameingia katika kampeni za uchaguzi pamoja na CDU wakitanguliza mbele madai yao wenyewe-mara ya mwisho yalihusu "kulipishwa ushuru wageni."Lakini mzozo huu wa sasa wa kikomo ni wa kipeo cha aina nyengine kabisa.

Kwasababu bila ya kikomo Seehofer hatotia saini makubaliano ya kuundwa serikali ya muungano. Lakini ndo kusema atakiachia chama chake cha CSU kikalie viti vya upande wa upinzani bungeni? Wapiga kura wanahisi mwisho wa mchezo huo haukadiriki. Anaetaka kwenda upande wa upinzani kwasababu ya Merkel anaweza pia kuamua kukipigia kura chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD. Seehofer anaelekea kufuata njia hatari hapo.

Kilio cha wananchi wa Rumania

Mada yetu ya pili magazetini inahusina na kilio cha wananchi nchini Rumania. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Warumania wamechoshwa na rushwa na wanataka sasa kudhibiti wenyewe mustakbali wao. Maandamano yao yamelengwa dhidi ya serikali ambayo ndio kwanza imeingia madarakani. Lakini idadi ya walioteremka vituoni kupiga kura ilikuwa ndogo kupita kiasi. Kwa hivyo wananchi wanataka serikali hiyo ijiuzulu na ichaguliwe nyengine itakayokubalika. Rais Klaus Iohannis anakubaliana nao. Wengi wa waandamanaji ni vijana, wasomi na licha ya yote hayo wameamua kusalia nchini. Hawataki chochote kutoka Ulaya. Ila waonekane tu. Na sio kama waandamanaji katika nchi ndogo ya Balkan. Bali kama wazungu wanaopigania kuwepo nchi inayoheshimu sheria.

Miaka 25 ya Maastricht

Mada yetu ya mwisho inahusu makubaliano ya Maastricht. Gazeti la "Neue Westfälische" linaandika: "Mjini Maastricht, Umoja wa Ulaya unatathmini lengo la umoja wao. Wameshindwa lakini katika juhudi zao kuwajumuisha raia na kufanya kile kinachohitajika. Maastricht linasalia kuwa jina la mji wa kiuhistoria usiokuwa na faida yoyote. Na madhara yake mpaka leo yanausumbua umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman