1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kuwania muhula wa nne

20 Novemba 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumapili (21.11.2016) amethibitisha kwamba atagombania tena ukansela katika uchaguzi wa mwaka 2017.

https://p.dw.com/p/2SyDr
Deustchland Angela Merkel
Picha: Getty Images/S. Gallup

Wajerumani wamekuwa wakisubiri kwa hamu kwa miezi kadhaa sasa kutaka kujuwa iwapo Kansela Merkel ambaye amekuwepo madarakani tokea mwaka 2005 atawania muhula wa nne au la wakati wa uchaguzi iliopangwa kufanyika mwezi wa Septemba mwaka 2017.

Baada ya miezi kadhaa ya tetesi inanaripotiwa kansela huyo amewaambia wanachama wenzake wa chama cha  CDU mjini Berlin kwamba yuko tayari kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi huo wa mwakani.

Kiongozi huyo wa chama cha CDU mwenye umri wa miaka 62 amekuwa akikabiliwa na matatizo kadhaa katika miezi ya hivi karibuni zikiwemo shutuma juu ya jinsi alivyoushughulikia mzozo wa wahamiaji uliosababisha kushuka kwa umashuhuri wake na kuja juu kwa siasa za sera kali za mrengo wa kulia.Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani dpa wakati akitangaza ugombea wake kwa wanachama wakuu wa CDU pia amesema kwamba atawania tena kukiongoza chama hicho cha sera za mrengo wa kulia wa wastani.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa taasisi ya Emnid uliochapishwa katika gazeti la Ujerumani la "Bild am Sonntag" asilimia 55 ya Wajerumani wanataka Merkel aendelee kuiongoza serikali ya Ujerumani kwa miaka mengine minne wakati asilimia 39 ilipinga aendelee kuingoza nchi.

 

Ajipatia heshima ya kimataifa

Angela Merkel
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture alliance/dpa/C.Rehder

Merkel ameiongoza taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya kupitia msukukosuko wa wa kifedha mzozo wa madeni wa nchi zinazotumia sarafu ya euro amekuja kupata heshima ya kimataifa ambapo hapo Alhamisi wakati Rais Barack Obama wa Marekani alipokuwa ziarani nchini Ujerumani amemuelezea kuwa ni "mshirika wa kupigiwa mfano."

Kutokana na ushindi wa Trump nchini Marekani kuongezeka kuungwa mkono kwa vyama vya sera kali za mrengo wa kulia barani Ulaya baadhi ya wachambuzi wanamuona Merkel kuwa ngome ya maadili ya kiliberali.

Hata hivyo uamuzi wake wa mwaka jana kuwacha wazi mipaka ya Ujerumani kwa takriban wahamiaji 900,000 wengi wao kutoka maeneo ya vita huko Mashariki ya Kati kumewakasirisha wapiga kura wengi nyumbani na kuathiri mashuhuri wake.
Chama chake kilipoteza katika uchaguzi wa majimbo mwaka jana wakati uungaji mkono wa chama Mbadala kwa Ujerumani AfD umeongezeka.

Aliishangaza nchi

Angela Merkel Raute Merkel-Raute
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/M.Kappeler

Hapo mwezi wa Septemba baada ya kushindwa vibaya kwa chama chake cha CDU katika uchaguzi wa jimbo mjini Berlin Merkel akiwa mnyenyekevu aliishangaza nchi kwa kusema angelitamani kuurudisha nyuma wakati kwa suala la wahamiaji lakini alisita kusema sera yake ilikuwa na makosa.Bado anahitaji kuungwa mkono na chama ndugu cha CSU washirika wake wa jimbo la Bavaria ambao walimshutumu vikali kwa sera yake ya kufunguwa mipaka kwa wahamiaji.


Takriban uchunguzi mwingi wa maoni unadokeza kwamba serikali ya muungano mkuu na chama cha SPD yumkini ikawa ndio chaguo baada ya uchaguzi wa mwezi wa Septemba juu ya kwamba kupata nguvu kwa chama cha AfD kunafanya mahesabu ya kuunda serikali ya mseto kuwa magumu zaidi.

Haijulikani iwapo iwapo atashinda muhula huo wa nne atatumikia kipindi chote cha miaka minne. Huko nyuma alisema anatafuta wakati muafaka kuachana na siasa  na sio kuzin'gan'gania kwa muda mrefu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa /DW
Mhariri : Zainab Aziz