1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Hollande kukutana na Putin

6 Februari 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa Ijumaa (06.02.2015) wanatarajiwa kujadili na Rais Vladimir Putin wa Urusi pendekezo lao la kukomesha mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1EWRb
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wakiwa mjini Kiev. (05.02.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wakiwa mjini Kiev. (05.02.2015)Picha: S. Supinsky/AFP/Getty Images

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine amesema mazungumzo ya Alhamisi usiku kati yake na Merkel na Hollande yamekuza matumaini baada ya viongozi hao wawili wa Ujerumani na Ufaransa kuwasili katika mji mkuu wa Ukraine Kiev katika juhudi kubwa kabisa kuwahi kufanyika za kuutatuwa mzozo huo wa Ukraine uliodumu kwa miezi kumi sasa.

Viongozi hao wawili wa Ulaya watakutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow Ijumaa ambaye mataifa ya magharibi yanamuona kuwa ndiye mpangaji mkuu wa uasi wa Ukraine unaoegemea upande wa Urusi na kujaribu kumshawishi asaini mpango wao wa amani wanaoupendekeza.

Kabla ya kuanza kwa safari yao hiyo ya kuendeleza juhudi za kidiplomasia kuutatuwa mzozo wa Ukraine Rais Hollande amesema mjini Paris kwamba yeye na Merkel watapendekeza ufumbuzi mpya kwa mzozo huo kwa kuzingatia haki ya Ukraine kudhibiti mipaka ya ardhi yake.

Mpango wa Minsk wasisitizwa

Wakati wa mkutano wake na viongozi hao wa Ufaransa na Ujerumani mjini Kiev Rais Poroshenko amesisitiza umuhimu wa kuendelea pia kuzingatiwa kwa mpango wa amani wa Minsk ambao tayari ulikuwa umekubaliwa.

Amekaririwa akisema "Mpango wa Minsk uko rahisi tu kutekelezeka: unataka usitishaji wa mapigano wa mara moja,kuwaachilia watu wote wanaoshikiliwa mateka, kufunga mipaka au kurudi tena kwenye mipaka inayotambuliwa kimataifa kwa upande wa Ukraine. Kuondolewa kwa vikosi vyote vya kigeni kutoka katika ardhi ya Ukraine,kuanzisha mchakato muhimu wa utaratibu wa kisiasa kwa uchaguzi wa serikali za majimbo kwa kuzingatia sheria ya Ukraine katika eneo la Donetsk na Luhansk."

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani(kushoto), Rais <petro Poroshenko wa Ukraine (katikati)na Rais Francois Hollande wa Ufaransa (kulia)wakiwa mjini Kiev. (05.02.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani(kushoto), Rais Picha: Reuters/Valentyn Ogirenko

Mpango unaopendekezwa na viongozi wa Ujerumani na Ufaransa inaonekana kwamba umefuatia mawasiliano ya kwenda na kurudi kati ya Merkel, Hollande na Putin na kwa mujibu wa repoti ya gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung utawapa waasi mamlaka makubwa zaidi na ardhi waliyoiteka katika mapigano ya hivi karibuni juu ya kwamba maafisa wa serikali ya Ujerumani wamekanusha.

Telekezo la mpango wa Minsk ni mtego

Licha ya juhudi hizo za kidiplomasia katika mpango huo mpya Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk amesisitiza kwamba Urusi lazima iheshimu mpango wa amani uliosainia Minsk mwezi wa Septemba mwaka jana. Amewaambia waandishi wa habari kuwa na mpango mpya na kutotekeleza ule uliopita kwake yeye anaona huo ni mtego.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Jatsenyu (kulia) mjini Kiev.(06.02.2015)
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Jatsenyu (kulia) mjini Kiev.(06.02.2015)Picha: Jim Watson/AFP/Getty Images

Marekani inaelekea kupitisha uamuzi wa kuipatia silaha Ukraine ambapo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia alikutana na Rais Poroshenko mjini Kiev hapo Alhamisi lakini hahusiki na mpango huo wa Merkel na Hollande juu ya kwamba anauunga mkono.

Mataifa ya magharibi yamegawika juu ya suala la kutowa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.Ujerumani imekuwa ikiongoza juhudi za kidiplomasia kuutatuwa mzozo huo lakini inapinga vikali kupatiwa silaha kwa serikali ya Ukraine kupambana na waasi.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ameonya kwamba kupatiwa silaha kwa Ukraine kutaipa kisingizio Urusi cha kuingilia kati moja kwa moja katika mzozo huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Josephat Charo