1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Hollande wana wasiwasi kuhusu Ukraine

Josephat Nyiro Charo15 Juni 2014

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francoise Hollande siku ya Jumamosi (14.06.2014) wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Ukraine na kutaka mapigano yakome.

https://p.dw.com/p/1CIdP
Francois Hollande und Angela Merkel Disharmonie
Picha: JANEK SKARZYNSKI/AFP/Getty Images

Katika mazungumzo ya simu na rais wa Urusi siku ya Jumamosi rais wa Ufaransa Francoise Hollande na kansela wa Ujerumani Angela Merkel walielezea wasiwasi wao mkubwa juu ya mapigano yanayoendelea nchini Ukraine. Kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Ufaransa, Hollande na Merkel walisisitiza umuhimu wa kufikiwa haraka makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.

"Inahusu kuweka mazingira ya kutuliza hali ya mambo katika uwanja wa mapambano, hususan kwa kuwazuia wapiganaji na silaha kuvuka mpaka na Urusi na kuwataka wanamgambo wanaotaka kujitenga kukomesha mapigano yao," ikaongeza kusema taarifa iliyotolewa.

Matamshi ya Merkel na Hollande yanakuja saa kadhaa baada ya wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi kuidungua ndege ya jeshi la Ukraine na kuwauwa watu wote 49 waliokuwemo. Kwa mujibu wa jeshi la Ukraine, waasi waliifyetulia kombora na risasi kutumia bunduki za rashasha wakati ilipokuwa ikijiandaa kutua katika mji wa mashariki wa Luhansk mapema Jumamosi. Ndege hiyo ilikuwa imewabeba wanajeshi, mashine, vifaa na mahitaji. Ukraine inaudhibiti uwanja wa ndege wa Luhansk, lakini mji wenyewe uko mikononi mwa waasi wanaoiunga mkono Urusi.

Tukio baya zaidi la umwagaji damu

Shambulizi hilo linaelezwa kuwa baya kabisa miongoni mwa matukio ya umwagaji damu katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili ya makabiliano kati ya waasi wanaoegemea Urusi na vikosi vya jeshi la Ukraine mashariki mwa nchi hiyo.

Ukraine Flugzeugabschuss 14.6.2014
Mahala ilipoanguka ndege ya jeshi la UkrainePicha: REUTERS

Katika hatua ya kukabiliana shambulizi hilo dhidi ya ndege ya jeshi, rais wa Ukraine, Petro Poroshenko, alikutana na wakuu wa ulinzi na usalama kujadili njia ya kujibu kudunguliwa kwa ndege hiyo ya kijeshi Jumamosi alfajiri. "Wote wanaohusika na vitendo vya ugaidi wa kiwango hiki lazima waadhibiwe," alisema Poroshenko katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. "Ukraine inahitaji amani. Hata hivyo magaidi watakabiliwa na hatua zifaazo."

Urusi yalalamika kuhusu bendera

Urusi baadaye iliishutumu Ukraine kwa kushindwa kuulinda ubalozi wake mjini Kiev. Muda mfupi baada ya ndege ya kijeshi kuangushwa, kundi la mamia kadhaa ya watu, wengi wao wakiwa vijana, waliyavunja madirisha ya ubalozi na kuiteremsha bendera ya Urusi. Waandamanaji hao pia walizipindua motokaa kadhaa zinazomilikiwa na wafanyakazi wa ubalozi huo.

"Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imeishutumu polisi ya Ukraine kwa kutochukua hatua na kusema hatua hiyo inayakiuka majukumu ya kimataifa ya Ukraine."

Ukraine Kiew Russische Botschaft Proteste
Waandamanaji wakipindua magari katika ubalozi wa Urusi, KievPicha: REUTERS

Mkataba kuhusu gesi bado

Rais Hollande na kansela Merkel pia walizungumzia kitisho cha Urusi kusitisha ugavi wa gesi kwa Ukraine kama serikali ya mjini Kiev itashindwa kulipa deni lake la mabilioni ya dola kufikia kesho Jumatatu.

"Wamesisitiza haja ya kufika makubaliano kulitatua tatizo hili la ugavi wa gesi ya Urusi kwa Ukraine," ikasema taarifa kutoka kwa ofisi ya rais wa Ufaransa.

Jana jioni waziri wa nishati wa Ukraine, Yuri Prodan, alisema mashauriano yataendelea leo asubuhi. "Kila upande umeelezea msimamo wake. Hakuna ufumbuzi uliopatikana," alisema Prodan.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP/DPA/REUTERS

Mhariri: Abdu Mtullya