1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cebit

Hamidou, Oumilkher4 Machi 2008

Maonyesho ya kimataifa ya Cebit yafungua njia kwa Ufaransa na Ujerumani kuweka kando hitilafu zao kuhusu malengo ya Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/DHlr
Kansele Merkel na rais Sarkozy kwenye maonyesho ya Cebit mjini HannoverPicha: AP


Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wamesema mjini Hannover ,jana,wamefikia "maridhiano" katika suala la "umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya kati"-mzizi mmojawapo wa fitina katika uhusiano kati ya Paris na Berlin.


"Tumefikia maridhiano katika suala la Umoja wa nchi za bahari ya Mediterenia ambao sote wawili tunaupigania na hakuna atakaetengwa" amehakikisha rais Nicolas Sarkozy wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari mjini Hannover.


"Tumekubaliana uwe mradi wa pamoja wa Umoja wa ulaya-"amesisitiza kwa upande wake kansela wa Ujeruma ni Angela Merkel.


Nicolas Sarkozy alikuja Hannover kufungua maonyesho makubwa kabisa  ya kimataifa ya teknolojia mpya ya mawasiliano-Cebit,akishiriki pia mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose-Manuel Barroso.


Mazungumzo na karamu ya chakula cha usiku pamoja na kansela Angela Merkel

 yamepelekea kuzungumziwa,zamu ya Ufaransa kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya kuanzia july mosi ijayo, na masuala mengine kadhaa ambayo misimamo ya Berlin na Paris haikua ikilingana.


Mzizi mkubwa zaidi wa fitina ulihusu mradi  ambao Nicolas Sarkozy alitaka kwa kila hali kuugeuza kipa umbele cha wadhifa wa nchi yake kama mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya,katika wakati ambapo Berlin ilikua ikizungumzia hofu mradi huo usije ukaugawa Umoja wa ulaya ,utakapozitenga zile nchi ambazo hazipakani na bahari ya Mediterenia.

Wakati wa mazungumzo hayo ,kansela Angela Merkel ameahidi kuisaidia Ufaransa itakapokabidhiwa zamu ya mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya.Kansela Angela Merkel amesema.


"Ujerumani na Ufaransa zikishindwa kukubaliana,inakua shida sana kufikia masikilizano ndani ya Umoja wa Ulaya.Na ndio maana,niaminivyo mie,jukumu letu ni moja.Kama sisi tulivyosaidiwa tulipokua na zamu ya kuongoza Umoja wa ulaya,ndivyo na sisi tutakavyoisaidia Ufaransa itakapokabidhiwa wadhifa huo ili kuupa msukumo Umoja wa Ulaya.Na nnaamini tunaweza kubainisha hali hii katika maonyesho haya ya Cebit."


Kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wamezungumzia pia mada nyengine tete inayohusu masilahi makubwa ya kiuchumi.Kansela Angela Merkel  amesema makubaliano yako njiani kufikiwa pamoja na Ufaransa kuhusu malengo ya Umoja wa ulaya ya kupunguza moshi wa magari.

Kwa upande wake rais Nicolas Sarkozy amezungumzia "msimamo wa pamoja wa Ufaransa na Ujerumani utakaofikiwa mnamo siku zijazo.


Wakati wa ziara yake ya saa nne,rais huyo wa Ufaransa ameisifu Ujerumani kua mfano wa maana kwa nchi yake.Sifa hizo zinaangaliwa kama ujumbe wa Ufaransa uliolengwa kutakasa mawingu yanayotanda katika uhusiano kati ya nchi mbili.

"Kuhudhuria maonyesho ya Cebit,si tukio la vivi hivi ni jukumu la kimoyo,ni jukumu la kiadilifu" kukutanabahisha wewe bibi Angela Merkel,na marafiki zetu wa Ujerumani,tunataka kushirikiana na nyie kirafiki kama tulivyokua tangu zamani" amesema rais Nicolas Sarkozy kwa moyo mkunjufu,wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Cebit ambayo Ufaransa ni muandalizi mwenza mwaka huu.



►◄