1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi ashinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka

28 Desemba 2015

Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka katika tamasha la Tuzo za Kandanda Duniani lililoandaliwa Dubai

https://p.dw.com/p/1HUfW
Leo Messi
Picha: picture-alliance/dpa/A. Garcia

Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye ni mchezaji bora wa mwaka mara nne na ambaye yuko katika orodha ya wachezaji watatu wanaowania tuzo ya FIFA ya Ballon d'Or mwaka wa 2015, aliisaidia timu yake kushinda Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi kuu ya kandanda ya Uhispania na Kombe la Mfalme licha ya kuwa mkekani kwa miezi miwili baada ya kuumia. Alisema "nna furaha sana. Kawaida inafurahisha kupewa tunzo hii. Hata ingawa umuhimu wake ni wa timu nzima, ni vizuri pia kupokea tuzo ya kibinafsi na nina furaha kubwa sana kuwa hapa"

Alipoulizwa ikiwa angeweza kuchagua tukio moja lililokuwa muhimu kwake mwaka huu, Messi alijibu kwa kusema ni vigumu. "ni vigumu kuchagua tuio moja tu. Ulikuwa mwaka uliojaa mengi kwetu. Tulishinda karibu kila kitu. Ulikuwa mwaka wenye mafanikio makubwa. Ukweli ni kwamba kuchagua tukio moja tu bora ni vigumu. Ninauona ulikuwa mwaka mzima wa matukio mengi kwa Barcelona" Tuzo ya timu bora ya mwaka pia iliwaendea mabingwa wa Ulaya Barcelona.

Marc Wilmots alipata tuzo ya kocha bora wa mwaka baada ya kuifikisha timu ya taifa ya Ubelgiji kileleni mwa orodha ya kimataifa ya viwango vya FIFA. Ubelgiji pia iliongoza katika Kundi lao na kufuzu katika michuano ya Mataifa ya Ulaya – UEFA Euro 2016

Fußball - UEFA Champions League Real Madrid vs Juventus Turin
Picha: Reuters/Juan Medina

Andrea Pirlo wa Italia na mchezaji wa zamani wa England Franck Lampard walipokea tuzo kwa mafanikio yao ya kucheza kandanda kwa muda mrefu. Kiungo Pirlo ameichezea timu ya taifa ya Italia mara 116, na alikuwa sehemu ya kikosi kilichonyakua Kombe la Dunia 2006 na kukisaidia kufika fainali ya Kombe la Ulaya Euro 2012. Pirlo alimaliza miaka kumi katika klabu ya AC Milan ambako alishinda mataji mawili ya ligi kuu ya Italia.

Sierie A na mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kisha akashinda mataji ya Sirie A katika kila msimu wa misimu yake minne na Juventus baada ya kuhama AC Milan mwaka wa 2011. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 sasa anachezea New York City FC ya Marekani.

Lampard, anashikilia rekodi ya kufunga magoli mengi katika klabu ya Chelsea na alikuwa nahodha wa klabu hiyo wakati ikishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka wa 2012. Alinyakua pia mataji matatu ya Premier League akiwa na Chelsea. Alihama Chelsea na kujiunga na New York City FC, na msimu uliopita alikuwa na Manchester City.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef