1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi atangaza kustaafu kandanda la kimataifa

27 Juni 2016

Chile wameshinda kwa mara ya pili mfululizo taji la Copa Amerika, baada ya kuwalaza wapinzani wao wakali Argentina kupitia mikwaju ya penalti baada ya mchuano kumalizika sare ya 0-0

https://p.dw.com/p/1JEUI
Chile - Copa America Finale 2015 - Chile vs. Argentinien, Lionel Messi
Picha: Reuters/R. Moraes

La Roja walifunga penalti 4 dhidi ya 2 za Argentina na kuhifadhi taji hilo la Copa America Centenario ambalo mwaka huu liliadhimisha karne moja tangu dimba hilo lilianzishwa.

Hata hivyo ushindi huo umegubikwa na habari zilizoushangaza ulimwengu wa kandanda. Nahodha wa Argentina Lionel Messi, ametangaza kuzitundika daluga zake katika timu ya taifa. Messi ambaye alipoteza penalti yake baada ya Arturo Vidal pia kupoteza yake, alibubujikwa machozi baada ya mchuano huo. Na ni kama miungu wa kandanda hawakuta akamilishe taaluma yake ya kimataifa kwa furaha maana hio imekuwa fainali ya nne kumponyoka mikononi..huyu hapa nyota huyo wa Barcelona "ndio basi tena. huu ndo uamuzi wangu. Nilipambana sana. nilifanya kila niwezalo ili nishinde. lakini ukweli ni kuwa ndo basi tena. Zimekuwa fainali nne. tayari nilikuwa nalifikiria. nilifany akila niwezalo. Haikuwezakana kushinda".

Argentina walishinda Copa America mara ya mwisho mwaka wa 1993 na wamepoteza fainali tatu katika miaka miwili. Na mwaka jana, walishindwa katika fainali kwa mikwaju ya penalti..dhidi ya nani? Chile. Aregtina pia ilipoteza fainali ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ujerumani.

Copa America 2016 Chile vs Argentinien | Chile Sieger
Chile imehifadhi taji la Copa AmericaPicha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Licha ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mara tato, Messi hukabiliwa na mbinyo kutoka kwa wakosoaji nchini mwake. Chile hata hivyo inaonekana kuwa kizazi cha dhahabu ambacho kinalenga kujiimarisha katika kandanda la kimataifa. Juan Antonio Pizzi ni kocha wa Chile "kwa bahati nzuri, tulifanikiwa kuunda kikosi cha wachezaji ambao tunastahili kuwashangilia, ambao tunastahili kuwapongeza. Natumai wataendelea kuimarika nasi na kuendelea kukua na timu hii ya taifa. Kadri michuano inavyochezwa, na muda unavyokwenda, timu hii inajituma zaidi ya uwezo wake na tunatumai kuwa tutaendelea kupambana ili kuendelea kupata mafanikio zaidi".

Lakini Messi sio mchezaji pekee ambaye anapanga kuondoka baada ya kichapo hicho. Javier Mascherano, Gonzalo Higuain na Sergio Aguero wote wanatathmini mistakabali yao. Kocha wa Argentina Gerardo Martino amekiri kuwa kuna hisia za huzuni kikosini "nakubali kuhusu machungu ya kutoshinda, hasa kwa sababu ya matarajio tuliyokuwa nayo na namba timu imekuwa ikicheza na kama utaanza kufikiria kuhusu siku zijazo leo, na hasa katika wakati kama huu, bila shaka ni vigumu. lakini mara nyingi wanamichezo wanaweza kujinyanyua na wamefanya hivyo kabla na nna uhakika watafanya hivyo tena".

Gumzo kuhusu tangazo la Messi kuiaga timu ya Argentina linaendelea kuvuma katika mitandao ya kijamii, na unaweza kunitumia maoni yako kwenye facebook na Twitter.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu