1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yatokota Mogadishu

12 Machi 2010

Waasi wapigana na wanajeshi wa serikali

https://p.dw.com/p/MRVA
Familia mjini Mogadishu yahama, mapigano yamekithiriPicha: AP

Mji huo wa Mogadishu umebadilika kuwa uwanja wa vita na raia kadhaa wameripotiwa kuuawa kutokana na mapigano hayo ya tangu mapema wiki hii.

Duru katika mji huo zinasema kwamba mapigano yalitokota siku ya Jumatano alasiri wiki hii kaskazini mwa Mogadishu ambapo wapiganaji wa kundi la waasi wanapania kuipindua serikali ya mpito inayoungwa mkono na nchi za magharibi.

Raia wengi wameuwawa katika ushambulianaji huo wa risasi. Meya wa Mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, Abdirisaq Mohammed Nur aliwaambia waandishi wa habari kwamba amependekeza wakaazi wote wauhame mji huo wakati wowote watakapoona vita vimechacha.

Serikali kupitia jeshi lake limekuwa likiripua na kushambulia maeneo wanakoshukiwa kujificha waasi wa la Al-Shabaab wanaoungwa mkono na Al-Qaeda tangu siku ya Jumatano wiki hii lakini Nur amesema huo sio mwanzo wa mashambulio ya jeshi la serikali unaopangwa kuanza wakati wowote.

Waasi wa Al-Shabaab wamekabiliana na wanajeshi wa serikali wanaoshirikiana na wale wa Umoja wa Afrika na madhumuni makuu ni kuwatoa nje ya mji wa Mogadishu wakitaka kudhibiti mji huo.

Wakaazi wanauhama mji wa Mogadishu tangu mwezi Februari ambapo duru za habari zilianza kudai kwamba kuna mashambulio makubwa yanayopangwa na sasa wengi wao wanapiga kambi katika eneo la Afgoye, magharibi mwa Mogadishu.

Shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema kwamba raia elfu thelathini na tatu wameuhama mji wa Mogadishu tangu mapigano yalipoanza mwezi Februari mwaka huu na wengine laki moja wameihama nchi hiyo tangu mwezi Januari.

Msemaji wa shirika hilo la wakimbizi, Andrej Mahecic akizungumza kutoka mjini Geneva,Uswisi, amesema hali nchini Somalia inaendelea kuwa mbaya kila uchao na kwamba inakuwa vigumu kutoa huduma kwa wakimbizi kutokana na kuzorota kwa usalama.

Somalia imekumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu kupinduliwa kwa mbabe wa kivita Siad Barre mwaka wa 1991.

Zaidi ya watu elfu ishirini wameuwawa katika mapigano ambayo yalianza kutokota tena mwaka wa 2007 baada ya wanajeshi wa Ethiopia kuingilia kati kuwasaidia wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia.

Kulingana na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi, takriban Wasomali milioni mbili wamehama nchi yao kutokana na vita na ni wakimbizi katika kambi za wakimbizi nchini Kenya na nchi nyingine jirani.

Mwandishi, Peter Moss/ DPA/AFP

Mhariri, Josephat Charo