1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Al Khalifa atangaza upinzani kushindwa

21 Machi 2011

Mfalme Hamad bin Isa al Khalifa wa Bahrain ameyashukuru majeshi ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba kwa kuzima njama za mataifa ya kigeni dhidi ya utawala wake baada ya wiki kadhaa za maandamano nchini mwake.

https://p.dw.com/p/10dC9
Maandamano dhidi ya utawala wa Bahrain
Maandamano dhidi ya utawala wa BahrainPicha: AP

Shirika la Habari la Bahrain limesema kuwa Mfalme Khalifa ametangaza kushindwa kwa njama hizo, wakati akizungumza na wanajeshi, na kusema kwamba iwapo njama kama hizo zingefanikiwa katika nchi mojawapo ya Ghuba, basi zingetapakaa katika nchi nyingine za eneo hilo.

Tangazo hilo la mfalme wa Bahrain limekuja siku moja baada ya nchi hiyo na Iran kufukuziana wanadiplomasia.

Iran imemtaka mwanadiplomasia wa Bahrain nchini humo kuondoka, ikiwa ni kulipiza kisasi cha kufukuzwa kwa mmoja wa wanadiplomasia wake nchini humo.

Wiki iliyopita Iran ilimuita nyumbani balozi wake katika kupinga mauaji ya watu yanayofanywa na serikali ya Bahrain ambapo siku moja tu baadaye Bahrain nayo ikamuita balozi wake nchini humo kwa madai kuwa, Iran imekuwa ikiingilia mambo yake ya ndani.

Bahrain ilimfukuza mwanadiplomasia wa Iran kwa kumtuhumu kuwa na mawasiliano na makundi ya upinzani.

Mwanamke wa Kibahrain akilia baada ya mashambulizi ya wanajeshi dhidi ya waandamanaji
Mwanamke wa Kibahrain akilia baada ya mashambulizi ya wanajeshi dhidi ya waandamanajiPicha: dapd

Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya Bahrain na Iran kutokana na Tehran kushutumu kwa nguvu hatua kali zinazochukuliwa na jeshi na kusababisha mauaji ya Washia katika taifa hilo la Kiarabu.

Na katika hatua nyingine chama kikuu cha upinzani nchini humo kimesema kuwa hakitaingia katika meza ya mazungumzo mpaka pale serikali itakapowaondoa wanajeshi mitaani na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa.

Kundi la upinzani nchini Bahrain linaloongozwa na chama cha Kishia cha Wefaq limebakia katika msimamo wake uliouweka mwezi uliopita ili kufanyike mazungumzo, ikiwemo kuundwa kwa serikali ambayo haidhibitiwi na wanachama kutoka familia ya kifalme inayoongozwa na Wasunni na kuanzishwa kwa baraza la uchaguzi kwa ajili ya kuandika upya katiba ya nchi hiyo.

Waandamanaji wanaopinga uingiliaji kati wa kijeshi mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia
Waandamanaji wanaopinga uingiliaji kati wa kijeshi mbele ya ubalozi wa Saudi ArabiaPicha: dapd

Kiongozi wa chama hicho Sheikh Ali Salman amesema Bahrain inahitaji makubaliano mapya kati ya watu wote pamoja na serikali. Amesema mfumo uliopo umeshindwa kufanya kazi.

Lakini katika hatua nyingine serikali ya Bahrain imesema imesikitishwa na majibu hayo yaliyotolewa na makundi ya upinzani, baada ya mtawala wa nchi hiyo kuahidi kufanyika mazungumzo kwa ajili ya kumaliza ghasia hizo.

Naye mbunge wa zamani kupitia chama hicho cha upinzani cha Wefaq, Hadi al-Moussawi amesema wanachama wao takriban 100 hawajulikani walipo kufuatia kamata kamata iliyofanywa na jeshi.

Amesema hawafahamu kitu chochote juu yao na wametoa taarifa katika hospitali na sehemu nyingi husika, lakini hawajapewa jibu lolote.

Wakati huo huo, Rais Barak Obama wa Marekani amemtaka mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, moja ya nchi mshirika mkubwa wa Marekani katika mashariki ya kati kujadili ghasia zinazoendelea nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza (AFP, Reuters)
Mhariri: Josephat Charo