1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Qatar azuru Ujerumani

Iddi Ssessanga
15 Septemba 2017

Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim Al-Thani ameitembelea Ujerumani, katika ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi tangu kuzuka kwa mgogoro kati yake na jirani zake wa Ghuba, ambapo amefanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/2k4Ns
Berlin Merkel empfängt Emir von Katar
Kansela Angela Merkel akiwa na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani baada ya kuzungumza na vyombo vya habari mjini Berlin Septemba 15, 2017.Picha: Getty Images/Sean Gallup

Katika kituo chake cha kwanza mjini Ankara Alhamisi usiku, Amir huyo wa Qatar alikutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye amekuwa muunganji mkono mkubwa wa Qatar wakati wa mzozo wa kidiplomasia uliodumu kwa miezi mitatu sasa, ambao umeiacha Qatar ikiwa imetengwa na jirani zake.

Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu zilivunja uhusiano na Qatar mwezi Juni kuhusiana na ukaribu wake na Iran na madai kwamba taifa hilo dogo tajiri linaunga mkono makundi ya itikadi kali. Qatar inakanusha kuunga mkono itikadi kali, ikisema mgogoro huo ulichochewa kisiasa.

Merkel, Al-Thani waeleza dhamira ya kumaliza mzozo

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habri mjini Berlin, Kansela Merkel na Mfalme wa Qatar wameelezea dhamira yao ya kuumaliza mgogoro kati ya Qatar na jirani zake kwa njia za kidiplomasia.

Emir Tamim von Qatar und Erdogan
Sheikh Tamim akiwa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara.Picha: Picture alliance/dpa/Turkish President Press Office

Kansela Merkel amesema haoni suluhu ya haraka kwa mgogoro huo lakini Ujerumani ingependa kusaidia katika utatuzi na kwamba wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na mfalme wa Kuwait kuutatua mzozo huo.

Kwa upande wake, Mfalme Al-Thani amesema yuko tayari kuutatua mzozo huo, na kuongeza kwamba ipo haja ya kuliangalia kwa undani suala la ugaidi. Ameishukuru Ujerumani kwa juhudi zake za usuluhishi. Wawili hao pia wamezungumzia uhusiano wa kimkakati wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Qatar.

Ujerumani imekuwa ikiunga mkono juhudi za kidiplomasia za kuutatuta mzozo huo, na waziri wa mambo ya nchi za nje  Sigmar Gabriel amesema idara ya uchunguzi ya Ujerumani itashiriki katika uchunguzi wa madai kwamba Qatar inayasaidia makundi ya kigaidi.

Tofauti za kisera kama kiini cha mgogoro

Mjini Ankara, viongozi hao wawili walisitiza haja ya kutafuta suluhu kupitia njia za kidiplomasia kulingana na ofisi ya Rais Erdogan. Lakini profesa wa masomo ya kanda ya Mashariki ya Kati katika chuo kikuu cha Qatar Mhajoob Zweiri ameelezea tofauti za kisera katika diplomasia za mataifa hayo kuwa kikwazo kikubwa katika kusuluhisha mgogoro huo.

"Saudi Arabia na UAE hiziridhishwi na sera ya kidiplomasia ya Qatar na zilijaribu kulaazimisha sera zao za kidiplomasia zinazowiana na maslahi yao kwa Qatar. huu ndiyo mzizi wa tatizo hilo," alisema msomi huyo.

Karte Mitgledsstaaten Gulf Cooperation Council ENG
Ramani inayoonyesha jiografia ya mataifa ya Ghuba.

Maslahi ya Ujerumani Qatar

Qatar, nchi ndogo yenye ukubwa sawa na jimbo la Hessen la hapa Ujerumani na jumla ya wakaazi milioni 2.6, ndiyo inaongoza duniani kwa uzalishaji wa gesi asilia, na inachangia asilimia 30 ya gesi yote inayouzwa kwenye soko la dunia.

Ina umuhimu mkubwa kwa Ujerumani kutokana na ukweli kwamba makampuni karibu 200 ya Ujerumani yana uwakilishi nchini humo na Ujerumani iliuza bidhaa za thamani ya euro bilioni 2.5 nchini Qatar katika mwaka wa 2016.

Qatar pia ni mwekezaji mkubwa katika mashirika kadhaa ya Ujerumani, ikiwemo benki kubwa zaidi ya ukopeshaji - Deutsche Bank, ambamo inamiliki asilimia 6.1 ya hisa kupitia wakfu wake wa uwekezaji wa nje QIA. Pia inamiliki asilimia 15 ya hisa katika kampuni kubwa zaidi ya magari barani Ulaya Volkswagen.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpad,ape.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman