1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Qatar ziarani Ujerumani

Klaus Jansen17 Septemba 2014

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel siku ya Jumatano anamkaribisha mfalme wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad At-Thani, mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika kanda ya mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/1DDhz
Katar Kronprinz Tamim bin Hamad al-Thani
Picha: Reuters

Ishara zake ni nzuri, wajihi wake ni tulivu. Bila kuonyesha hisia, ni vigumu sana kujua anachokiwaza Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani. Mfalme huyo wa Qatar anafahamu vizuri nini wanachostahili wafalme wa kiarabu. Kwa muda wa miaka 10 aliandaliwa kushika wadhifa wa kiongozi wa nchi, na miongoni mwa mambo mengine alipitia chuo cha kijeshi cha Sandhurst cha nchini Uingereza. Alirithi nafasi ya baba yake mwaka mmoja uliyopita, na sasa mfalme huyo mwenye umri wa miaka 34 ndiye mkuu wa serikali mwenye umri mdogo zaidi katika ulimwengu wa kiarabu, na mojawapo wa walio na ushawishi mkubwa zaidi.

Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani akiwa na mwanae Sheikh Tamim.
Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani akiwa na mwanae Sheikh Tamim.Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Ushawishi wake unatokana na utajiri usiyomithilika lililonao taifa hilo dogo la ghuba, unaotokana na hifadhi kubwa za mafuta na gesi. Ikiwa na wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja cha dola za Marekani 100,000, Qatar ndiyo nchi iliyokuwa kileleni duniani mwaka uliyopita. Serikali yake imenunua hisia katika makampuni makubwa duniani katika miaka iliyopita, na hata nchini Ujerumani.

Qatar inamiliki hisa katika baadhi ya makampuni makubwa ya Ujerumani kama vile Volkswagen inamomiliki asilimia 15.6, na kampuni kubwa ya ujenzi ya Hochtief ambako inamiliki asilimia 10. Zaidi ya hayo, nchi hiyo inawekeza katika kampuni ya Siemens na Deutsche Bank. Sheikh Tamim katika mazungumzo yake na Kansela Merkel, watajadili ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa mambo mengine.

Uwekezaji katika makampuni makubwa

Waqatar huwekeza mitaji yao katika makampuni ya kimataifa, ili kuongeza faida. Kwa sababu rasilimali katika eneo la ghuba zinaweza kuisha wakati wowote, taifa hilo linalenga kupanua uchumi wake. "Ikiwa Qatar itaishiwa pesa basi kunaweza kujitokeaza matatizo mengi ya kijamii, na kwa kuwa uchumi huu unategemea mafuta na gesi hilo ni tatizo kubwa," anasema Michael Stephens, mkurugenzi wa taasisi ya ushauri ya Royal United Services ya Qatar (RUSI).

Kwa hiyo huu ni mkakati wa muda mrefu kuwekeza katika mataifa mengi tofauti duniani, yakiwemo ya bara la Ulaya, na hilo wanatumai litaongeza utulivu nyumbani na kuwaimarisha zaidi kiuchumi na kisiasa katika muda mrefu, anaeleza mtaalamu huyo wa masuala ya mashariki ya kati.

Kansela Angela Merkel akiwa na mfalme wa Zamani wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani mwaka 2010 baada ya serikali ya Qatar kununua hisa katika kampuni kubwa ya Hochtief ya nchini Ujerumani.
Kansela Angela Merkel akiwa na mfalme wa Zamani wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani mwaka 2010 baada ya serikali ya Qatar kununua hisa katika kampuni kubwa ya Hochtief ya nchini Ujerumani.Picha: AP

Sera ya bidii

Baba yake Tamim, Shaikh Hamad bin Khalifa al-Thani aliongeza ukuaji wa uchumi wa taifa lake mara saba wakati wa utawala wake kuanzia mwaka 1995 hadi 2013. Alishiriki pia sera ya kigeni, kwanza kama mpatanishi katika migogoro kadhaa katika mataifa ya Kiarabu. Mwaka 2008 pande zinazohasimiana nchini Lebanon, zilikubaliana kwa msaada wa Qatar juu ya muafaka, ambao ulisafisha njia ya kufanyika uchaguzi mpya. Na mwaka moja baadaye, serikali ya Sudan ilisaini makubaliano ya amani na waasi wa jimbo la Darfur mjini Doha.

Kwa sera yake ya bidii, mfalme huyo wa zamani wa Qatar alijipatia maadui pia, kwa sababu Qatar ililiunga mkono kundi la Udugu wa Kiislamu wakati wa vuguvugu la mabadiliko katika ulimwengu wa Kiarabu. Baada ya uchaguzi wa kwanza huru uliyomleta Mohammad Mursi madarakani nchini Misri, Qatar ilitoa mikopo ya mabilioni kwa serikali mjini Cairo. Hata kituo cha Televisheni cha Aljazeera kinachomilikiwa na serikali ya Qatar kilitoa umuhimu wa kipekee kwa kundi la Udugu wa Kiislamu. Qatar ilikosolewa sana kwa sera zake hizo.

Wakati Sheikh Hamad alipofanya uamuzi wa kustukiza na kumkabidhi madaraka mwanae mwezi Juni mwaka 2013, wengi walitumai kuwa mfalme huyo mdogo angechukuwa mwelekeo tofauti. Lakini hadi sasa hajaweza kufanya hivyo, anasema mtaalamu wa masuala ya mashariki ya Kati Stephens.

Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani alipokutana na rais wa Misri aliepinduliwa Mohammad Mursi mjini Cairo Agosti 2011.
Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani alipokutana na rais wa Misri aliepinduliwa Mohammad Mursi mjini Cairo Agosti 2011.Picha: picture-alliance/dpa

Mabadiliko ya mwelekeo?

Hata katika baraza la ushirikiano wa mataofa ya Ghuba GCC, ambalo pamoja na Qatar linaundwa na mataifa ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Kuwait, Bahrain na Oman kumekuwa na malumbano. Mwanzoni mwa mwaka huu, mataifa matatu kati ya sita wanachama wa GCC yaliondoa mabalozi wake nchini Qatar, wakiituhumu kwa kuliunga mkono kundi la udugu wa Kiislamu. Saudi Arabi na Umoja wa Falme za Kiarabu wanaliona kundi hilo la Kiislamu kama tishio kwa tawala zao. Wakati huo huo, Qatar inaonekana kusalimu amri chini ya shinikizo, baada ya kuwaamuru viongozi kadhaa wa Udugu wa Kiislamu walioko mjini Doha kuondoka nchini humo mwishoni mwa wiki.

Kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Ghuba, Qatar pia inashikiri kampeni inayoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la wapiganaji wa Dola ya Kiislamu nchini Iraq, ambayo pia inaungwa mkono na Ujerumani. Kansela Merkel anataka kuzungumza na Sheikh Tamim juu ya hali inayoendelea nchini Iraq na Syria. Matajiri wa Qatar wanadhaniwa kuwa wanawafadhili wapiganaji wa Dola ya Kiislamu, na muungano dhidi ya Dola ya Kiislamu ulikubaliana kukomesha ufadhili kwa wapiganaji hao.

Mataifa 29 yaliyoshirki mkutano wa Paris uliyojadili kitisho cha Dola ya Kiislamu, yalikubaliano kuhamisha ufadhili ili kuyaimarisha makundi ya waasi yenye msimamo wa wastani nchini Syria. Kwa Qatar, hili linaweza kumaanisha kubadilisha mwelekeo, na fursa kwa Sheikh Tamim kujenga sera yake mwenye ya kigeni.

Mwandishi: Allmeling Anne.
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Oummilkheir Hamidou