1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfuko wa Dirk Nowitzki unajihusisha Tanzania

Maja Dreyer28 Septemba 2007

“Sisi sote tunajua kwamba duniani kuna watu wengi ambao hawana maisha mazuri kama yetu, kwa hivyo tunapaswa kutoa msaada.” Anayesema haya ni mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu, Dirk Nowitzki ambaye ni Mjerumani lakini anacheza kwenye ligi ya NBA huko Marekani. Licha ya kuwafurahisha mashabiki wake kwa kufunga mabao mengi – hata alishawahi kuchaguliwa mchezaji wa mwaka kwenye ligi ya NBA – Dirk Nowitzki pia anatumia mapato yake kuwawezesha watoto wengi maskini au wagonjwa kufanya mazoezi na kujiendeleza maishani.

https://p.dw.com/p/CHjA
Dirk Nowitzki
Dirk NowitzkiPicha: Ap

Mnamo mwaka 2001, mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu, Dirk Nowitzki, alianzisha mfuko wake wa kwanza huko Marekani ambapo anaishi pamoja na familia yake. Lengo la mfuko huu ni kuwasaidia watoto maskini duniani kupata elimu na afya.

Miaka miwili baada ya hapo, mchezaji huu pia ameanzisha mfuko mwingine hapa Ujerumani ambao ofisi yake iko mjini Würzburg mji alipozaliwa na alipoishi kama kijana Dirk Nowitzki. Akieleza juu ya mifuko hiyo, Dirk amesema: “Tunajaribu kuwasaidia watoto duniani kote. Tumeanzisha miradi kadhaa ambayo inaendelea vizuri kweli, baadhi yao hapa Ujerumani na pia tunajihusisha huko Tanzania kujenga shule.”

Kabla ya kusikia zaidi juu ya ushirikiano na mradi huu wa Tanzania tuangalie kwa ufupi kwa ujumla shughuli za mfuko huu huko Würzburg. Kwa vile umeanzishwa miaka michache tu iliyopita, kweli ni shirika dogo lenye mfanyakazi mmoja. Wengine wanaosaidia kuandaa mashindano na kuendesha ushirikiano fulani kawaida ni watu wanaojitolea. Kwa sasa, mfuko huu unachangia katika miradi mitano, baadhi yao ni hapa Ujerumani na mingine katika nchi za nje, mfano Nepal.

Fungamano na huko Tanzania bado liko kwenye ngazi ya kutayarishwa. Na kwa ajili hiyo, mkurugenzi wa utafiti na mipando ya mradi huu uitwao “Mtwara Sports Academy” amekuja Ujerumani kukutana na watu wa mfuko wa “Dirk Nowitzki”. Shule hiyo inalenga kuwasaida watoto walioko katika hali ngumu kupitia michezo.

Bi Anastacia Wambura ni mmoja kati ya waasisi wa Mtwara Sports Academy ambao mpaka leo wanagharamia wenyewe miradi wanayoiendesha. Sasa lakini kuna matumaini kuwa shule hiyo itasaidiwa kifedha kutoka mfuko wa Dirk Nowitzki.

Bi Jessica Wulf ambaye ni msimamizi wa ofisi huko Würzburg anaeleza kwa nini mradi huu utapata msaada´: “Mradi huu umetuvutia kwa sababu mazoezi yanapewa kipaumbele. Na yale tuliyozungumzia pia kwenye ziara ya Bi Wambura hapa kwetu ni kwamba huko Tanzania, michezo haiendelezwi sana. Michezo lakini ina manufaa mengi, kuanzia upande wa mtu binafsi, na pia kuhusiana na jamii. Kwa hivyo, kujenga shule ya michezo ili kuwafundisha watoto mapema ni ni kitu ambacho hakiko hadi leo na ndiyo maana mradi huu unatuvutia sana. Hususan kutokana na wazo hilo la waasisi juu ya manufaa ya michezo, kweli mradi huu unaenda sambamba kabisa na malengo ya wakfu wetu.”

Kama Bi Wambura alivyosema, Mtwara Sports Academy, inalenga hasa watoto walioko katika hali ngumu kupitia michezo. Michezo kweli ina manufaa makubwa. Kwa upande mmoja, bila shaka, michezo ni vizuri sana kwa afya ya kila mtu. Vilevile lakini michezo ni kama chombo cha kushirikiana, kukutana, kuheshimiana na kusaidiana. Ndiyo wazo la msingi la mfuko wa Dirk Nowitzki kuanzishwa. Kuambatana na fikra hizo, Mtwara Sports Academy si kituo cha kuendesha michezo, kama anavyoeleza Bi Anastacia Wambura hapo aliposema kuwa wanaendesha pia miradi ya kuwafundisha akinamama kazi ya kushona na kadhalika pamoja na kuwasaidia na vijana wasio na ajira.

Mfano mwingine wa mradi unaogharamiwa na mfuko wa Dirk Nowitzki ni huko Hamburg, Ujerumani, ambapo shirika lisilo la kiserikali linawaleta pamoja watoto kutoka mitaa mbali mbali kwa michezo na masomo ya muziki. Watoto hao wanatoka sehemu tofauti ya jamii, wengine ni wa familia tajiri, wengine ni maskini, baadhi yao ni Wajerumani wengine wazazi wao wamehamia Ujerumani. Bila ya mradi huu, watoto hao hawangekutana, kwa hivyo ni juhudi za kuleta maelewano kati ya watoto wenye maisha tofauti waheshimiane, kwanza katika michezo na halafu maishani kwa ujumla.

Mpendwa msikilizaji, huenda wewe mwenyewe unaendesha mradi kama huu au una wazo fulani au umewahi kusikia juu ya miradi ya aina hiyo pale mlipo. Kama anavyosema Bi Wulf wa mfuko wa Dirk Nowitzki, atafurahi sana kupata barua au maombi. Amesema: “Njia mwafaka kabisa ni kupitia tovuti yetu kwenye mtandao wa Internet. Bila shaka tunapata barua nyingi wakati tunapozidi kujulikana lakini tunaiangalia kila moja na kuzungumza na waendeshaji ili tuone vipi inavyoendelea na wapi tunaweza kuchangia.”

Pale ambapo shirika hili haliwezi kusaidia kifedha liko tayari lakini kusaidia kutafuta wafadhili wengine na kuuandaa mchanganuo unaohitajika. Bi Anastacia Wambura alipenda pia kutoa mwito kwa wananchi wenzake na wasikilizaji wengine wapaze sauti zao ikiwa wana wazo zuri.

Anwani ya mtandao wa Internet ya mfuko huu: ni www.dirk-nowitzki-stiftung.org