1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfumo wa kukinga makombora waekwa Korea Kusini

Yusra Buwayhid
26 Aprili 2017

Korea Kusini imesema sehemu muhimu za mfumo wa ulinzi wa Marekani wa kukinga makombora zimeshawekwa nchini humo, baada ya hasimu wake Korea Kaskazini kuonyesha nguvu zake za kijeshi. Ni hatua pia iliyoikasirisha China.

https://p.dw.com/p/2bwQr
THAAD Raketenabwehrsystem
Picha: picture alliance/ZUMAPRESS/B. Listerman

Marekani inaisisitiza China - ambayo ni mshirika mkuu wa Korea Kaskazini- kuchukua hatua zaidi za kuidhibiti nchi hiyo. Lakini taifa hilo kubwa barani Asia limeitikia wito huo kwa hasira, kutokana na hatua ya Marekani ya kuweka mfumo wa kukinga makombora unaojulikana kama THAAD katika ardhi ya Korea Kusini.

China ina wasiwasi  mfumo huo wenye nguvu kubwa unaweza kupenya katika ardhi yake na kudhoofisha usalama wa nchi yake, pamoja na usalama wa kanda hiyo. China inaupinga mfumo huo wa kukinga makombora katika kanda hiyo ya Asia.

Aidha, China imeichukulia Korea Kaskazini hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufu makundi ya ziara nchini mwake.

Akizungumza katika mkutano wake wa kila siku na waandishi habari, msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya China, Geng Shuang, amesema China inaitolea wito Marekani na Korea Kusini kuondoa mfumo huo wa kukinga makombora.

"Tunatarajia kwamba pande zote, ikiwa ni pamoja na Japan, zitashirikiana na China ili kulipatia suala hili azimio la amani la mapema. Tunatarajia kwamba pande zote zitachukua jitihada kama ilivyo wajibu wao," amesema Geng Shuang.

Donald Trump und Xi Jinping
Rais wa Marekani Donald Trump, akiwa na Rais wa China Xi JinpingPicha: picture alliance/AP Photo/A. Brandon

Marekani na mshirika wake Korea Kusini wanasema uamuzi wa kutuma wanajeshi, ulikubalika tokea mwaka jana, na una lengo la kuzuia  kitisho cha makombora ya Korea Kaskazini iliyo na silaha za kinyuklia.

"Na tunaendelea katika ngazi zote mbili kujijenga na kuwa tayari hata tukihitajika kupigana usiku wa leo. Kwa upande wa zoezi hili na katika kazi yangu hii ya miaka ishirini, sijawahi kuona zoezi la aina hii.. la kitaaluma zaidi na lenye uwezo zaidi wa mifumo ya silaha ambayo imejumuishwa pamoja na yenye uwezo wa kufyatua risasi kwa wakati mmoja .. kama nilivyoona katika zoezi hili hapa," amesema Luteni Kanali wa Kimarekani Matthew Harner, akiuzungumzia mtambo huo wa kukinga makombora.

Rais wa China, Xi Jinping alizungumza na Rais wa Marekani Donald Trump juzi kwa njia ya simu na kumtaka ajizuie katika suala hili la Korea Kaskazini.

Viongozi wa ulinzi wa Marekani pamoja na maafisa wengine a ngazi za juu, leo wanatarajiwa kuwa na mkutano wa siri na maseneta wote wa Marekani kuhusu suala hilo la Korea Kaskazini. Ni mkutano usio wa kawaida katika ikulu ya Marekani ya White House.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre/ape

Mhariri:  Yusuf Saumu