1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfungo wa Ramadhani waanza

10 Julai 2013

Leo ni Ramadhani Mosi kwa sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu, mwanzo wa mwezi mmoja wa waumini wa dini hiyo kujitakasa na kujikaribisha kwa Muumba wao, na pia kuhurumiana wao kwa wao.

https://p.dw.com/p/1955U
Gebet
10.07.2013 DW Deutschland Heute Ramadan

Waumini wa dini ya Kiislamu wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hii leo. Kuanzia alfajiri jua linapochomoza hadi magharibi jua linapozama kwa kipindi cha mwezi mmoja, waumini hao wanajizuia kula, kunywa na mambo mengine yanayotengua saumu zao, ikiwa ni sehemu muhimu ya ibada kwenye Uislamu. Ramadhan ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu.

Kufunga ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu. Kuanza na kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan hutegemea na kuandama kwa mwezi lakini kwa miaka mingi sasa kumekuwa na mgongano juu ya njia za kugundua kuandama kwa mwezi. Baadhi ya nchi hutaka mwezi lazima uonekane kwa macho na hukataa kutambua kuandama kwa mwezi kwa kutumia njia za kisayansi.

Mwandamo wa mwezi

Hata hivyo nchini Saudi Arabia, televisheni ya taifa ya Al-Ekhbariyah ilitangaza kuwa baraza linalohusika na kuthibitisha kuandama kwa mwezi limetoa taarifa kuwa leo ndio mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Vyakula vya kijadi kwa ajili ya kufungua saumu nchini Iran.
Vyakula vya kijadi kwa ajili ya kufungua saumu nchini Iran.Picha: MEHR

Barani Asia Waislamu wameanza mfungo huku wale waislamu wenye itikadi kali nchini Indonesia, nchi yenye idadi kubwa ya waislamu duniani, wakiapa kuvamia mabaa yenye kuuza vileo wazi wazi baada ya polisi nchini humo kukamata shehena za vileo na filamu za ngono, mambo ambayo ni kinyume na dini ya Kiislamu.

Wakosoaji wanasema waislamu hao wenye itikadi kali kama vile chama cha kutetea Uislamu cha Islamic Defenders Front (FPI) kimevunjwa moyo na kushindwa kwa serikali kufanya oparesheni dhidi yao na kuepusha mashambulizi hayo

Wakati huo huo, kumetolewa wito kwa misikiti nchini humo kupunguza sauti za vipaza sauti ili kuepuka kutatiza maisha ya yale wanaoisha karibu na miskiti hiyo.

Mauaji, umwagaji damu kwenye ulimwengu wa Kiislamu

Mataifa ya Kiarabu na yenye Waislamu wengi kama vile Misri, Syria na Libya yanaingia kwenye Ramadhani nyengine yakiwa na machafuko na mauaji. Nchini Misri ambako ni wiki moja tu tangu jeshi kumpindua Rais Mohamed Mursi, hali ni ya wasiwasi na ukosefu wa furaha, ambapo majeshi ya serikali na waasi nchini Syria wanaendelea kupambana na hivyo kumwaga damu ndani ya mwezi huu mtukufu.

Mashambulizi ya tarehe 9 Julai 2013 nchini Lebanon.
Mashambulizi ya tarehe 9 Julai 2013 nchini Lebanon.Picha: Reuters

Kipindi hiki cha mfungo, Waislamu wote kote ulimwenguni hutakiwa kujitenga na mambo yasiompendeza Mungu na yale yasiofaa katika jamii. Ni mwezi wa waumini wa dini hiyo kutumia muda wao mwingi zaidi kuomba msamaha kwa Mungu, kusali na kusoma kitabu kitakatifu cha Qur'an.

Mwandishi: Dalila Athmani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef