1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgawanyiko miongoni mwa Wapaalstina-Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza

Miraji Othman13 Januari 2009

Mgawanyiko baina ya Hamas na Fatah waondosha imani ya Wapalastina kwa viongozi wao

https://p.dw.com/p/GXi6
Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Palastina, PLO, marehemu Yasser Arafat,akielekea Paris, Ufaransa, ambako alifia.Picha: AP

Licha ya maombi ya Chama cha Wapalastina cha Hamas kwamba kufanywe michafuko ya mara ya tatu ya Intifada, watu wachache katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wanaonekana kuwa na hamu ya kuweko michafuko kama hiyo, ikijulikana kwamba kuna mgawanyiko mkubwa baina miongoni mwa wenyewe Wapalastina na watu kuvunjwa moyo na viongozi wao. Michafuko ya kwanza ya Intifada ilizuka katika ardhi za Wapalastina mwaka 1987, pale hasira kutokana na kukaliwa ardhi yao kwa miaka 20 na majeshi ya Israel zilipotokota baada ya wakaazi sita wa Ukanda wa Gaza kuuliwa na gari la kijeshi la Israel. Kama kweli Wapalastina mara hii watakuwa na udole wa kufanya michafuko ya Intifada.

Japokuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na operesheni za sasa zinazoendeshwa na Israel huko Ukanda wa Gaza inakaribia alfu moja, hivyo kuyafanya mashambulio hayo kuwa makali kabisa kuwahi kufanywa na Israel katika kijiardhi hicho kidogo, hakujakuweko malalamiko makali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, licha ya kutolewa maombi na kiongozi wa Hamas, Khaled Meshaal.

Pia, ukiwacha matokeo machache ya hapa na pale, hakujakuweko mashambulio dhidi ya vituo vya Israel. Bassam a-Salihi, kiongozi wa Chama cha Popular, ambacho zamani kilijulikana kuwa ni chama cha kikoministi, anasema wakaazi wa Kipalastina hawana tena imani na viongozi wao wa kisiasa, na ndio maana hakujakuweko vuguvugu kubwa la wananchi kuzipinga operesheni za Israel huko Gaza. Bwana Salihi anasema wananchi kuvunjwa moyo na viongozi kunatokana, kwa sehemu kubwa, na uhasama mkubwa ulioko baina ya Chama cha Hamas na kile cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas. Mapambano baina ya vyama hivyo viwili katika Ukanda wa Gaza hapo Juni mwaka 2007 yalimalizika kwa chama cha Kiislamu cha Hamas kuwafukuza mahasimu wao wasioelemea dini kutoka Ukanda wa Gaza. Bwana al-salihi anasema hali ya sasa inayowakuta Wapalastina inatokana na kugawika kwao na kukosekana mipango yeyote ilio wazi ya kuendesha upinzani dhidi ya uvamizi wa Israel.

Fikra zake zinakaririwa pia na Abdelrahim Maluh, afisa wa cheo cha juu wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Palastina, PFLP, akisema kwamba wanasiasa wanaoutumia nguvu zao katika mabishano baina ya Wapalastina ni jambo linalowavunja moyo wakaazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Migawanyiko hiyo haidhihirishi ukweli wa mambo ulivyo miongoni mwa Wapalastina, kwa ujumla. Anasema michafuko yeyote ya Intifada itakayotokea sasa itajiri kutokana na ukweli wa kijamii na sio kutokana na ombi au amri kutoka kiongozi huyo au yule.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Nader Izzat, profesa wa elimu jamii katika Chuo Kikuu cha Bir Zeit, mgawanyiko ulioko baina ya viongozi wa Kipalastina ni sura ya mgawanyiko mkubwa zaidi katika jamii, kwa ujumla, juu ya namna ya kukabiliana na hali duni ilivyo. Anasema katika Intifada ya kwanza ya mwaka 1987, kulikuweko makubaliano juu ya haja ya kufanya michafuko miongoni mwa wananchi. Lakini sasa Hamas inatenda kwa niaba yake wenyewe, wakati Chama cha Fatah kinafanya kile kilicho na faida kwake. Kumekuweko maisha tafauti baina ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, Ukanda wa Gaza ukiwa na fikra zaidi za kiasilia, na katika Ukingo wa Magharibi kuna fikra za kutoelemea dini. Tafauti hizi zimezidi katika miaka ya karibuni kutokana na vizuizi vingi viliovowekwa na wakuu wa Israel kuhusu kusafiri baina ya maeneo hayo mawili. Tangu Israel ilpoamuwa kuondosha majeshi yake kutoka Gaza mwaka 2005, watu wa Ukanda huo ulioko katika ukingo wa Bahari wamekuwa mbali na ndugu zao wa Ukingo wa Magharibi. Katika uchaguzi wa mwaka 2006, watu wengi wa Gaza walikichaguwa Chama cha Hamas, huku wengi kidogo wakibakia watiifu kwa Chama cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Mgawanyiko huo umezidi tangu kufa Yasser Arafat, kiongozi mkongwe Chama cha Ukombozi wa Palastina, PLO.