1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kifedha Cyprus wachacha

Tsuma Carolyne21 Machi 2013

Benki kuu ya Ulaya imesema itaendelea kuzipa benki za Cyprus msaada wa fedha wa dharura hadi Jumatatu ila itabidi kusitisha msaada huo ifikapo siku hiyo mpaka mpango wa kimataifa wa uokozi utakapoafikiwa.

https://p.dw.com/p/181DS
Benki za Cyprus zaathirika na mgogoro wa fedha
Benki za Cyprus zaathirika na mgogoro wa fedhaPicha: Reuters

Benki hiyo kuu imesema inaendelea kuziokoa benki za Cyprus ambazo zimekumbwa na msukosuko wa kiuchumi kutokana na hatari ya kufilisika lakini imesema itawalazimu kukatiza usaidizi iwapo hakuna mapatano ya jinsi nchi hiyo itakavyojikwamua kutoka kwa mzozo wa madeni.

ECB leo imesema kuwa baraza lake limeamua kuendeleza kiwango kilichoko kwa sasa cha usaidizi kutoka mfuko wa uokozi wa dharura lakini hilo litaendelezwa tu iwapo kutakuwa na mpango uliodhinishwa na Umoja wa Ulaya na IMF utakaoepusha benki za Cyprus kutotangazwa kufilisika.

Mpango mbadala wazungumziwa

Wanasiasa nchini humo hii leo wanajadili mpango mpya wa uokozi utakaopunguza asilimia itakayatozwa akiba za wateja wa benki,uuzaji wa mali za benki na mkopo mpya kutoka kwa Urusi na badala yake Cyprus kuipa gesi asilia.

Mpango huo mbadala unaotarajiwa kupigiwa kura na wabunge leo unanuia kuchangisha euro bilioni 5.8 ili kuiwezesha kupata mkopo wa euro bilioni 10 kutoka kwa Umoja wa ulaya na hazina ya fedha ya kimataifa IMF.

Wateja watoa pesa katika mtambo wa atm
Wateja watoa pesa katika mtambo wa atmPicha: Reuters

Mpango wa awali wa kutoza kodi akiba za wateja wa benki kwa aslimia 10 uliozua ghadhabu kutoka kwa raia na wanasiasa ulipingwa na bunge na kuzua hali ya taharuki miongoni mwa wawekezaji na wasiwasi kuwa benki za nchi hiyo zitaporomoka.

Mpango huo mpya inasemekana kuwa utapunguza kodi hiyo kutoka asilimia 10 hadi 3 kwa akaunti za wateja walio na euro laki moja na zaidi pekee. Benki nchini humo zimefungwa hadi Jumanne wiki ijayo ili kupunguza maafa zaidi kiuchumi hadi mpango makhususi utakapopatikana.

Shughuli za biashara zakwama

Mitambo ya ATM hata hivyo bado inatoa huduma kwa wateja licha ya taarifa kuwa vituo vya mafuta ya petrol hazikubali kadi za benki kwa malipo na kuna uhaba wa madawa kwani wafanyibiashara nao wamekataa malipo kwa kutumia kadi kutoka kwa wateja wao.

Mgogoro huo wa kifedha umekwamisha shughuli nyingi za kibiashara nchini humo na sasa Cyprus imegeukia mshirika wake wa muda mrefu Urusi wakitumai kupata msaada utakaowaepusha kufilisika. Waziri wa fedha wa Cyprus Michael Sarris yuko mjini Moscow ambako amesema atasalia mpaka apate ufumbuzi wa tatizo.

Waziri wa fedha wa Cyprus Michael Sarris
Waziri wa fedha wa Cyprus Michael SarrisPicha: Reuters

Rais wa Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso amesema mgogoro huo wa fedha wa Cyprus unamtia wasiwasi lakini anatumai kuwa suluhisho litapatikana hivi karibuni kwani Umoja huo umekabiliwa na matatizo makubwa katika kipindi cha nyuma kushinda hilo la Cyprus.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/ap/Reuters.

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.