1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Kifedha: Ugiriki ku moto, EU yagawika

15 Juni 2011

Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro wameshindwa kufikia makubaliano juu ya kuisaidia Ugiriki, huku Ugiriki kwenyewe maandamano yakipamba moto dhidi ya mpango wa Umoja wa Ulaya kuuokoa uchumi wa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/11aZ1
Maandamano nje ya Bunge la Ugiriki kupinga mpango wa EU
Maandamano nje ya Bunge la Ugiriki kupinga mpango wa EUPicha: dapd

Sasa mawaziri hao wameamua kukutana tena Luxemburg Jumapili ijayo baada ya kikao chao cha hapo jana (14.06.2011) mjini Brussels, kumalizika wakiwa wamegawanyika. Waliamua kutolitoa tamko la pamoja walilokusudia kuliwasilisha kwa lengo la kuyatuliza masoko ya fedha.

Mpango wa pili wa kuiokoa Ugiriki ulikuwa kati euro bilioni 90 hadi bilioni 120. Lakini imebainika kwamba mpango wa hapo awali hauwezi kufanikiwa katika nchi hiyo, ambayo tayari imeshazidiwa na madeni.

Licha ya kupata msaada mkubwa kutoka Umoja wa Ulaya (EU)na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Ugiriki inashindwa kujitoa kwenye dimbwi la matatizo na hadi mwaka wa 2012 haitakuwa na uwezo wa kupata fedha kutoka kwenye masoko ya fedha.

Askari wa Ugiriki wakimkamata muandamanaji
Askari wa Ugiriki wakimkamata muandamanajiPicha: dapd

Je, nchi zilizomo katika Jumuiya ya Sarafu ya Euro zinapaswa kufanya nini? Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Jean-Claude Juncker, ameleeza kwamba katika kukabiliana na matatizo ya Ugiriki, hakuna miiko yoyote itakayozingatiwa.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, alisisitiza pendekezo la nchi yake kwenye mkutano wa mjini Brussels juu ya kuishirikisha sekta binafsi katika juhudi za kuutatua mgogoro wa madeni wa Ugiriki.

Ujerumani, ambayo ni mfadhili mkuu wa mpango huo, iliungwa mkono na Uholanzi katika kuyataka mabenki na mashirika ya bima yashiriki katika kuiasiadia Ugiriki.

Schäuble amependekeza kwamba sekta ya binafsi yenye dhamana za Ugiriki, izibadili dhamana hizo na mpya zitakazokuwa na muda wa miaka zaidi ya saba kabla ya kuanza kulipiwa.

Lakini pia Schäuble alisistiza umuhimu wa kuimarisha ustawi wa uchumi katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Ugiriki.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki, George Papaconstantinou (kulia) akizungumza na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble
Waziri wa Fedha wa Ugiriki, George Papaconstantinou (kulia) akizungumza na Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang SchaeublePicha: dapd

"Jambo muhimu sana ni kuziimarisha njia za kuustawisha uchumi, kwa sababu bila ya Ugiriki kuelekea kwenye ustawi, haitawezekana kutimiza lolote. Na vile vile sehemu muhimu sana ya juhudi ni mchango wa sekta binafsi." Alisema Shäuble, ambaye pia alikiri kuwa kwa sasa hakuna kilichofikiwa.

Ujerumani inasisitiza juu ya mchango wa sekta binafsi, mabenki na makampuni ya bima, ili kuwaepushia mzigo walipa kodi. Waziri Schäuble amependekeza kwa mabenki yazibadili dhamana za Ugiriki walizonazo kwa mpya zitakazokuwa na muda wa miaka zaidi ya saba hadi kuanza kulipiwa.

Japokuwa hiyo ni njia rahisi ya kuubadili utaratibu wa ulipaji wa deni la Ugiriki, lakini siyo wote wanaokubalina nayo. Waziri wa wa Fedha wa Ubelgiji, Didier Reynders, amesema hayo yanaweza kufanyika kwa hiari.

"Kwangu mimi ni kosa kuwalazimisha wadau kuchukua hatua. Hayo yanaweza kusababisha ukosefu wa mikopo na pia yanaweza kusababisha matatizo makubwa katika eneo lote linalotumia sarafu ya euro."

Lakini pendekezo la Ujerumani litaipa Ugiriki muda zaidi wa kulishughulikia deni lake la Euro Bilioni 330. Kwa sasa kadiri siku zinavyopita, ndivyo wasiwasi unavyozidi kuwa mkubwa juu ya uwezekano wa Ugiriki kushindwa kulipa deni lake, jambo linaloweza kusababisha mgogoro mwingine mkubwa wa fedha barani Ulaya.

Mwandishi: Christoph Hasselbach/DW
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Thelma Mwadzaya