1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa madeni wa Ugiriki

27 Agosti 2012

Mgogoro wa fedha wa Ugiriki,mzozo wa Syria na kifo cha Neil Amstrong ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/15xII
Waziri mkuu wa Ugiriki Samaras (kushoto) na kansela Angela MerkelPicha: dapd

Tuanzie lakini Berlin na Paris ambako waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras alifika ziarani mwishoni mwa wiki kuwaomba viongozi wawe na subira kuelekea mgogoro wa fedha unaoikaba nchi yake.Wakati kansela Angela Merkel anawapa moyo wagiriki,washirika wake serikalini wananung'unika.Gazeti la Stuttgarter Zeitung linaandika:

Vipi wawekezaji wataweza kupata imani kama kweli Ugiriki itafanikiwa kuleta mageuzi,ikiwa waziri wa fedha wa taifa kubwa la kiviwanda barani Ulaya,anaashiria kwa njia moja au nyengine juu ya kushindwa juhudi za Ugiriki?Philip Rösler na katibu mkuu wa chama cha CSU,Alexander Dobrindt,pengine wanataka kujipendekeza kwa wapiga kura,lakini walichokisema hakilingani na nidhamu wala kuwajibika.Hakuna njia mbadala katika suala la kimsingi la dai na wajib.Wagiriki hawana budi isipokuwa kutekeleza mageuzi waliyoahidi.Lakini wakati huo huo juhudi wanazofanya lazma zitambuliwe ili waweze kupata moyo wa kuendeleza juhudi hizo.Yadhihirika kana kwamba baadhi ya wanasiasa wanashindwa kuitambua bali hiyo."

Alexander Dobrindt CSU Generalsekretär
Katibu mkuu wa chama cha CSU Alexander DobrindtPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:

Nidhamu inahitajika katika baraza la mawaziri .Nasaha ya kansela kwa mawaziri wake wajizuwie,haijasaidia kitu.Hata kabla ya maombi ya Ugiriki kutangazwa rasmi,katibu mkuu wa chama acha CSU,Alexander Dobrindt ameanza kulalamika.Eti CSU wamekusudia nini hasa?Yadhihirika kana kwamba hawajali zahma inayoweza kutokana na  soga lao .Kwao wao la muhimu zaidi ni uchaguzi wa jimbo lao la Bavaria mwakani.Ikiwa rais mpya wa Ufaransa Francois Hollande amedhihirisha anatekeleza makubaliano yake na kansela,kwa hivyo hata  akina Seehofer na wenzake, na wao pia wanabidi angalao wanyamaze kimya.Kujishughulisha kwa muda mrefu zaidi na yanayotokea katika jimbo lao la Bavaria,ungekuwa mchango wa maana."

Kämpfe im Libanon - Ausbreitung Syrien-Konflikt
Mapigano kaati ya wasuni na waalawi wa Syria nchini LibnanPicha: Reuters

Mada yetu ya pili magazetini inahusiana na hali nchini Syria.Gazeti la mjini Cologne,"Kölner Stadt -Anzeiger" linaandika:

Syria inaelekea katika janga la hatari.Baraza la usalama la umoja wa mataifa na jumuia ya kimataifa hawatokua na budi isipokuwa kuingilia kati haraka.Kila kukicha hofu  za kuzidi visa vya uhalifu zinazidi kuongezeka.Na hasa shehena ya silaha za kemikali zinazomilikiwa na Assad zitailazimisha jumuia ya kimataifa iingilie kati-pengine moja kwa moja wakati huu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe-pindi muimla huyo akitaka kweli kutumia silaha hizo za hatari.Au baada ya kuporomoka kwake,ili silaha hizo za maangamizi zisije zinaingia mikononi mwa wanajeshi walio watiifu kwake,Hisbollah au wanamgambo wa kigeni wa kiislam.Wizara ya ulinzi ya Marekani-Pentagon, inakadiria panahitajika wanajeshi 60 elfu kuweza kuwazuwia hatari ya kutumiwa silaha hizo za sumu.Itakuwa sawa na kuingilia kati kijeshi-kwa kiwango kama kile kilichoshuhudiwa nchini Iraq.

Mwandishi: Hamidou  Oummilkheir

Vyanzo: Stuttgarter Steitung, Landeszeitung,Kölner Stadt -Anzeiger,

Mhariri: Mohammed Khelef