1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa uchumi wadumaza juhudi za kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia

Charo Josephat 27 Aprili 2009

Idadi kubwa ya watu katika nchi zinazoendeelea kukabiliwa na umaskini

https://p.dw.com/p/HfHA
Nembo ya shirika la fedha la kimataifa IMF

Mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia umesababisha kuweko kwa hali ya hatari katika maendeleo itakayosababisha baadhi ya malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa kutofikiwa katika nchi nyingi ulimwenguni, hususan barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara na Asia Kusini.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa, IMF, juma lililopita, lengo la milenia la kupunguza umaskini kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2015 barani Afrika na Asia Kusini linakabiliwa na kipingamizi kikubwa kutokana na mgogoro wa kiuchumi.

Huku chumi za nchi zinazoendelea zikitarajiwa kufikia ukuaji wa asilimia 1.5 mwaka huu wa 2009, kati ya milioni 55 na milioni 90 ya raia wake wanatarajiwa kujiunga na tabaka la watu wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri. Ripoti ya benki ya dunia iliyopewa jina, "Hali ya hatari ya maendeleo" inasema pato jumla la kitaifa linatarajiwa kushuka katika nchi 50 maskini duniani, nyingi zikiwa barani Afrika.

Ripoti hiyo imeonya kwamba takwimu zitaongezeka iwapo mgogoro wa uchumi utaendelea kuongezeka na ukuaji uchumi katika nchi zinazoendelea utaendelea kuporomoka. Aidha ripoti hiyo imesema katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na Asia Kusini, ambako hali ya umaskini iko juu, kukwama kwa ukuaji wa kiuchumi kimsingi kunaondoa kabisa uwezekano wa kuendelea kupunguza umaskini mwaka huu.

Hali hiyo itasababisha athari kubwa na za mda mrefu katika sekta ya afya na elimu. Ripoti ya benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa imesema mgogoro wa kiuchumi utasababisha vifo vya watoto kati ya 200,000 na 400,000 kila mwaka kati ya mwaka huu 2009 na mwaka 2015, wakati ambapo malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa yanatakiwa kuwa yametimizwa.

Naibu mkurugenzi wa shirika la fedha la kimataifa, IMF, John Lipsky, amesema ingawa kunywea kwa uchumi kunaziathiri zaidi nchi zenye chumi imara, hali katika mataifa yanayoendelea inazorota kwa kasi kubwa. Kiongozi huyo amesema chumi zitafufuka kwa kasi ya kinyonga na hivyo kuvifanya vita dhidi ya umaskini kuwa changamoto kubwa na vya dharura zaidi.

Mkutano wa G20

Mapema mwezi huu viongozi wa kundi la nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi na zinazoinukia haraka kiuchumi walikutana mjini London Uingereza na kukubaliana kulipa shirika la fedha la kimataifa dola bilioni 750 kuzisaidia nchi zinazotaka mikopo kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi.

Kiwango kingine cha dola bilioni 250 kitatolewa kwa mpango maalumu wa mkopo kwa nchi zitakazokuwa na haki maalum. Kati ya kiwango hicho, dola bilioni 100 zitatolewa kwa nchi zinazoendelea.

G 20 Gipfelteilnehmer in London
Viongozi wa nchi za G20 mjini LondonPicha: AP

Nchi za G20 ziliunga mkono ongezeko la utoaji wa mikopo katika benki za maendeleo, ikiwa ni pamoja na benki ya dunia, kwa kiwango cha dola bilioni 100 kila mwaka katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Nchi hizo pia ziliidhinisha mipango ya benki ya dunia kuongeza kwa kwiango kikubwa mikopo yake kwa miradi ya ujenzi wa miundobminu, biashara ndogo ndogo na biashara za wastani na kusimamia mitandao ya usalama ya kijamii.

Benki ya dunia ilitangaza Ijumaa iliyopita kwamba itaongeza mara tatu fedha inazotoa kwa ajili ya kugharimia mifumo ya afya kufikia dola bilioni 3.1 na kuongeza maradufu fedha kwa ajili ya elimu mwaka huu kufikia dola bilioni 4.1 katika mwaka huu.

Malengo ya Milenia

Malengo ya milenia ya Umoja wa Mataifa yaliyoanzishwa na viongozi wa dunia kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2000 na kuidhinishwa tena mwaka jana, yanajumulisha malengo manane yanayotakiwa kutimizwa kufikia mwaka 2015.

Lengo la kwanza ni kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya watu wanaoishi katika hali ngumu ya umaskini na wanaokabiliwa na baa la njaa katika nchi zinazoendelea kufikia mwaka 2015.

Malengo mengine ni kuhakikisha watoto wanapat elimu ya shule ya msingi, kuendeleza usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake, kupunguza vifo vya watoto na akina mama wakatiw a uzazi kwa thuluthi mbili, kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ukimwi, malaria na magonjwa mengine makubwa.

Huku ufanisi ukiwa umepatikana katika kuyafikia malengo haya wakati wa sehemu ya kwanza ya muongo uliopita, kasi imekwamishwa kutokana na mchanganyiko wa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa nchi tajiri kutimiza ahadi zao za misaada zilizotoa wakati wa mkutano wa kilele wa nchi za G8 uliofanyika mjini Gleaneagles nchini Scotland mnamo mwaka 2005.

Shirika la Oxfam limesema ripoti ya benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF, inadhihirisha jinsi hali ilivyo mbaya na inatakiwa kuzipa changamoto nchi tajiri zitimize ahadi ilizotoa kwenye mkutano wa Gleaneagles na mkutano wa kundi la nchi 20 wa mjini London Uingereza mapema mwezi huu, ili kuongeza kwa kiwango kikubwa msaada kwa nchi zinazoendelea.

Mwandishi: Jim Lobe/IPS/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman