1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro washtadi Ukraine

Abdu Said Mtullya12 Aprili 2014

Rais wa muda wa Ukraine ameahidi kutowachukulia hatua za kisheria watu wanaoegemea Urusi, ambao kwa sasa wanayashikilia majengo ya serikali

https://p.dw.com/p/1Bfh4
Ghasia katika jimbo la Donetsk mashariki mwa Ukraine
Ghasia katika jimbo la Donetsk mashariki mwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Rais wa muda Oleksander Turchynov amesema hatachukua hatua za kisheria dhidi ya watu hao lakini lazima wazisalimishe silaha zao na waondoke kwenye majengo wanayoyashikilia.

Bwana Oleksander Turchynov amewaambia wabungewa nchi yake kwamba ikiwa watu hao watazisalimisha silaha zao na kuondoka kwenye majengo ya serikali wanayoyashikilia atahakikisha kwamba hawachukuliwi hatua za kisheria. Turchnov ameeleza kuwa yuko tayari kutoa amri ya Rais kwa ajili hiyo.

Watu wanaeogemea Urusi wanaotaka kujitenga na Ukraine wanayashikilia majengo ya serikali katika miji ya Luhansk na Donetsk mashariki mwa Ukraine.Serikali ya Ukraine imesema hatua za watu hao zinaweza kutumiwa na Urusi kama sababu ya kuivamia Ukraine.

Ukraine ipo tayari kufikia mwafaka

Rais wa muda wa Ukraine amesema kuwa serikali yake ipo tayari kulijadili suala la kuleta mageuzi ya serikali ya jimbo ili kutoa mamlaka zaidi ikiwa pamoja na haki ya kuanzisha mamlaka ya utawala wa ndani ya jimbo.

Kulingana na katiba ya Ukraine iliyopo sasa, magavana wa majimbo wanateuliwa na serikali kuu mjini Kiev. Serikali ya Ukraine mpaka sasa imekuwa inaipinga miito ya Urusi juu ya kuanzisha mfumo wa shirikisho katika nchi hiyo. Wapinzani wa serikali katika mji wa Donetsk wamelitangaza jimbo hilo kuwa ni Jamhuri huru ya umma na watu wanazipepea bendera za Urusi.

Juhudi za kimataifa

Wajumbe wa kidilpomasia wa ngazi za juu kutoka Urusi,Ukraine,Marekani na Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana mjini Geneva wiki ijayo ili kuujadili mgogoro wa Ukraine. Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia wanatarajiwa kukutana Luxemburg Jumatatu ijayo kutafauta njia za kukabiliana na mgogoro wa Ukraine.

Katika kadhia nyingine juu ya matukio ya nchini Ukraine Urusi imemlaani Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa Nato kwa kupiga ngebe za enzi za vita baridi wakati ambapo mivutano inaongzeka baina ya jumuiya hiyo ya kijeshi ya Nato na Urusi. Katika tamko lilotolewa leo, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imemkemea katibu mkuu huyo Anders Fogh Rasmussen na kumlaumu kwa kuigeuza Nato kuwa kikundi cha watu maalumu kinachotumia undumakuwili katika siasa za kimataifa.

Katika hotuba aliyoitoa mjini Paris hapo juzi Rasmussen aliitaka Urusi iwarudishe nyuma maalfu ya wanajeshi wake iliyowalundika karibu na mpaka wa Ukraine.Nato imesema Urusi inawatumia wanajeshi hao waliopo karibu na Ukraine kwa lengo la kuishinikiza serikali ya nchi hiyo na kwamba Urusi inafanya matayarisho ya kuivamia Ukraine.

Mwandishi: Mtullya Abdu/ ape

Mhariri: Josephat Charo