1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahojiano na mgombea wa Die Linke Janine Wissler

Saumu Mwasimba
24 Agosti 2021

Katika mahojiano maalumu na DW, mgombea mkuu wa chama cha mrengo wa shoto cha Ujerumani Janine Wissler amekosoa vikali uitikiaji wa serikali ya Ujerumani nchini Afghanistan, na kusema wamehatarisha maisha wa bindamu.

https://p.dw.com/p/3zRDx
DW Interview BTW Janine Wissler Die Linke mit Chimbelu und Romaniec
Picha: R. Oberhammer/DW

Hapa nchini Ujerumani zimebakia wiki chache tu ufanyike uchaguzi mkuu na hali haijawahi kuwa wazi kuhusu mwelekeo wa matokeo kama ilivyo wakati huu. Katika mfululizo wa kuzitazama siasa za Ujerumani kuelekea uchaguzi huo leo tunaangazia mazungumzo ya DW na mgombea ukansela wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke Janine Wissler.

Mgombea ukansela wa Die Linke Janine Wissler alihojiwa na waandishi wawili wa DW katika kipindi maalum cha televisheni mjini Berlin na katika suali la kwanza alitakiwa kueleza nini hasa anafikiri inapaswa kuwa dhima ya Ujerumani hivi sasa nchini Afghanistan. Mgombea huyo wa Die Linke ameulizwa suali hilo hasa kutokana na chama chake ambacho kina mrengo wa siasa za ujamaa miaka yote kuwa mstari wa mbele kupiga kura kupinga wanajeshi wa Ujerumani kupelekwa nje ya nchi. Bibi Wissler hili ndilo lililokuwa jibu lake.

Soma pia: Merkel ajibu maswali ya wabunge kwa mara ya mwisho

''Hii leo na katika siku chache zijazo kitu muhimu zaidi ni kuyaokoa maisha ya wau wengi kadri inavyowezekana, kuwaondoa watu wengi kadri inavyowezekana. Lakini lazima tuelewe kwamba miaka 20 ya vita Afghanistan na miaka 20 ya jeshi la Ujerumani kupelekwa nchini hmo, baada ya maelfu ya watu kuuwawa, nchi hiyo haijawahi kuwa salama wala kuwa na amani. Ni Kinyume chake, tunashuhudia janga. Na ndio sababu kupeleka wanajeshi nchini humo lilikuwa kosa tangu mwanzo.''

Mgombea huyo wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke ameendelea kutetea hoja yake hiyo kwa kufafanua kwamba ujumbe wa jeshi la Ujerumani,Bundeswehr peke yake uligharimu yuro bilioni 12.5 na anaamini fedha hizo zingeweza kusaidia kuimarisha kali ya kibinadamu nchini Afghanistan na ndio sababu chama chake miaka yote kimekuwa kikipinga juhudi za vita hivi.

DW Interview BTW Janine Wissler Die Linke mit Chimbelu und Romaniec l Making Off
Picha: R. Oberhammer/DW

Ama kwa upande mwingine amezungumzia msimamo wa chama chake kuhusu suala la nchi za magharibi,Urusi na China kuingia kwenye mazungumzo na Taliban akisema Ujerumani pia imo kwenye mazungumzo na Taliban na kwa mtazamo wake hilo ni kosa kubwa.Ingawa kuna tafauti baina ya kuwatambua Taliban kama serikali na kuzungumza nao lakini Wissler anasema tatizo ni kwamba Taliban lilishatambuliwa mapema kabisa pindi yalipofanyika mazungumzo ya amani mjini Doha, Qatar ambapo Marekani iliamua kuzungumza na Taliban na kuiacha nje serikali ya Afghanistan.

Soma pia: SPD yamchagua Olaf Scholz kugombea ukansela

Aidha Wissler ameulizwa pia kuhusu namna uongozi wake endapo atakuwa Kansela wa Ujerumani utakavyoshughulikia masuala ya kimataifa,suali hilo likiulizwa na mfuatiliaji wa DW kutoka huko nchini Kenya.

''Moja ya vitu,ni kwamba tunahitaji mfumo wa usawa wa kiuchumi duniani. Hatuwezi kuwa na nchi tajiri zinazofuja rasilimali za nchi masikini kabisa. Tunahitaji  utaratibu wa kiuchumi duniani. Tunapaswa kuacha kupeleka silaha kote duniani na kuwaunga mkono madikteta.Badala yake tunapaswa kujikita katika kuangalia ushirikiano wa kimaendeleo na kuimarisha hali ya kibinadamu. Tunahitaji juhudi za dunia nzima kukabiliana na njaa. Nafikiri hilo ndilo la muhimu zaidi. Na hiy pia ndiyo njia ya kuondoa baadhi ya sababu zinazochangia uhamiaji.Hilo pia linahusika na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi''

Ametoa pia mifano ya kuacha kuzipelekea silaha nchi kama Saudi Arabia,Misri au Qatar hatua ambayo anaamini itachangia kuifanya dunia kuwa salama zaidi,pale alipoulizwa ikiwa anafikiri Ujerumani inapaswa kujiondowa kabisa katika dhima ya kimataifa na kujielekeza tu kwenye msaada wa maendeleo.

''Lakini inamaanisha nini kujiondowa ´katika dhima ya kimataifa? Naweza kusema kwamba Ujerumani itakuwa na mchango mkubwa zaidi wa kubeba dhima ya kimataifa kwa mfano tungeacha kuwapelekea silaha watawala kama Saudi Arabia au Qatar na Misri.Hilo lingechangia kuifanya dunia kuwa salama.''

Kadhalika mgombea huyo wa Ukansela wa chama cha Die Linke nchini Ujerumani amegusia kuhusu Urusi baada ya kuulizwa ikiwa atapata nafasi ya kukutana na rais wa Urusi Vldmir Putin nini hasa anachopanga kuzungumza nae, kikubwa alichosema ni hali ya wapinzani, na haki za binadamu. Haungi mkono matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Urusi bali anapendelea zaidi sera ya kumaliza vita.

Chanzo: DW