1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo licha ya kufanyiwa marekebisho baraza la mawaziri nchini Ufaransa

Oumilkher Hamidou23 Machi 2010

Vyama vya wafanyakazi nchini Ufaransa vimeitisha mgomo mkubwa hii leo kuishinikiza serikali ifikirie upya msimamo wake kuhusiana na sekta za kiuchumi na kijamii

https://p.dw.com/p/MZmR
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: AP

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amelifanyia marekebisho baraza la mawaziri la nchi hiyo,jana, baada ya chama chake cha UMP na washirika wake kushindwa vibaya sana katika uchaguzi wa mikoa jumapili iliyopita.Licha ya kuahidi kuzingatia kwa makini zaidi madai ya umma,vyama vya wafanyakazi vimeitisha mgomo mkubwa hii leo nchini humo.

Mageuzi ya baraza la mawaziri yamelengwa zaidi kuileta pamoja kambi ya wahafidhina baada ya pigo walilolipata katika uchaguzi wa mikoa.

Waziri mkuu Francois Fillon,anaejivunia zaidi imani ya wananchi,ataendelea na wadhifa wake.Kigogo pekee aliyepokonywa wadhifa wake ni waziri wa kazi Xavier Darcos,aliyeshindwa vibaya sana katika uchaguzi wa jumapili kwa namna ambayo isingekua rahisi kwake kuongoza majadiliano ya sera za malipo ya uzeeni na umri wa mtu kustaafu.Nafasi yake amekabidhiwa waziri wa zamani wa bajeti ambae ni mtiifu kwa rais Sarkozy.

Mageuzi ya baraza la mawaziri yamepelekea kuingia serikalini wawakilishi wa mrengo wa kulia ambao si wafuasi wa Nicolas Sarkozy-yamekomesha wakati huo huo mtindo wa kuwafungulia milango wafuasi wa mrengo wa shoto serikalini.

Chama cha kisoshialisti hakijakawia kuyataja mageuzi hayo kua ni "kiini macho".Harlem Desir ambae ni kiongozi wa pili wa chama cha kisoshialisti amesema tunanukuu:"baada ya pigo la kihistoria la mrengo wa kulia,wananchi wanategemea mageuzi ya kina ya kiuchumi na kijamii."Mwisho wa kumnukuu.

Frankreich Regionalwahlen Martine Aubry
Mwenyekiti wa chama cha kisoshialisti Martine AubryPicha: AP

Mwenyekiti wa chama cha kijamaa-PS Martine Aubry anasema:

"Kwa kupiga kura na kwa wengi wengine kujizuwia kupiga kura,wafaransa wametaka kuonyesha upinzani wao dhidi ya siasa ya rais wa jamhuri na serikali yake.Nnafikiri wameikataa siasa isiyokua ya haki,zawadi nono za kodi za mapato kwa wenye kujiweza kifedha,dhidi ya nafasi za kazi,mapambano dhidi ya ukosefu ajira na dhidi ya kuinua shughuli za kiuchumi."

Katika wakati ambapo rais Sarkozy anasema ameuelewa mwito wa wapiga kura, mashirika yanayopigania haki za wafanyakazi yameitisha migomo kote nchini Ufaransa hii leo kudai nyongeza za mishahara,kazi na hali bora ya maisha kwa wastaafu.

Shughuli za usafiri wa jamii-metro zimevurugika na shule kufungwa.Mgomo huo unazihusu tangu sekta za serikali hadi za kibinafsi.Lengo ni kulalamika dhidi mpango wa serikali wa kurekebisha sekta ya malipo ya uzeeni na umri wa watu kustaafu pamoja pia na kufutwa maelfu ya kazi katika sekta za serikali.

Maandamano na mikutano ya hadhara imepangwa kufanyika katika kila pembe ya Ufaransa hii leo.

Mgomo huu wa siku moja ni kishondo cha kwanza kwa serikali iliyofanyiwa marekebisho jana.

Kiongozi wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini Ufaransa CGT,Bernard Thibault amemtaka hii leo rais Nicolas Sarkozy aitishe haraka mkutano wa kilele wa kijamii kuzungumzia masuala ya kiuchumi na kijamii.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/AFP

Imepitiwa na:Abdul-Rahman,Mohammed