1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo mkuu wa Wafanya kazi umeshika kasi Afrika Kusini

Othman, Miraji6 Agosti 2008

Maelfu kwa maelfu waandamana kupinga kupanda ughali wa maisha nchini Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/Era3
Rais Thabo Mbeki wa Afrika KusiniPicha: AP

Maelfu ya watu waligoma kwenda makazini leo kote nchini Afrika Kusini. Shughuli zilisita katika migodi ya dhahabu na viwandani . Sababu ni kwamba watu wanalalamikia juu ya kupanda ughali wa maisha ambao umeikumba nchi hiyo inayotajwa kuwa ni kama injini ya kiuchumi katika bara la Afrika. Maelfu ya watu walimiminika mabarabarani katika mji mkuu wa Pretoria wakielekea hadi ofisi ya Rais Thabo Mbeki, huku wakibeba mabiramu na wakitaka hatua zichukuliwe kuzuwia kupanda juu bei za bidhaa.

Vyama vya wafanya kazi vinasema usafiri wa umma ulisimama nchi nzima leo, huku kukiwekwa vizuwizi mabarabarani na matairi ya magari kuchomwa moto. Waandamanaji walisema bei za juu, hasa za vyakula na mafuta, zinawaumiza zaidi watu walio maskini nchini humo, ambako asilimia 40 ya karibu wakaazi milioni 48 wa nchi hiyo hawana kazi na milioni nne wanaishi katika hali ya hohe hahe. Kulikuweko ripoti kwamba wafanya kazi wachache walifika makazini, huku makampuni mengine yakifungwa. Gold Fields, kampuni kubwa kabisa la migodi ya dhahabu katika Afrika Kusini, lilisema wafanya kazi wake waliofika kazini leo ni baina ya asilimia saba na arbaini, na kiwanda cha kutengeneza magari ya Volkswagen kilifungwa. Milolongo mirefu ya ya watu walikua wanangojea kwa masaa mengi usafiri wa mabasi na taxi katika mji wa Johannesburg, huku watu wengine wakisema wanayaelewa malalamiko ya watu kupinga ughali wa maisha, lakini sio mgomo wenyewe.

Mgomo huo, ulioitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanya Kazi, COSATU, lenye wanachama 320,000, unaonesha umeitikiwa na wanachama milioni mbili wa vyama vinavoshirikiana na shirikisho hilo katika sekta za uchumi wa kibinafsi na wa umma. Waandamaji mjini Pretoria walisalimisha risala iliokuwa na matakwa yao kwa idara ya nishati, wakisema mgao wa umeme usiwe tu kwa watu walio maskini. Mfumko wa bei za vitu katika mwezi Juni huko Afrika Kusini ulipanda kwa asilimia 12.2. Sababu ya kupanda huko, Issac Khomu, mwandishi wa habari huko Johannesburg, aliniambia hivi:

Uchumi wa Afrika Kusini katika robo ya kwanza ya mwaka huu umepanda kwa asilimia 2.1 ukilinganisha na asilimia 5.3 katika robi ya mwisho ya mwaka jana.

Kama serekali ya Rais Thabo Mbeki ni ya kulaumiwa kutokana na hali hii, Issac Khomu, aliongezea kwa kusema:

Na mwanauchumi mmoja alisema pindi shida zinazowapata watu maskini zitadharauliwa, basi mambo yatakua hatari, kwani mgomo huu wa leo ni kilio cha walio maskini na wafanya kazi kwamba hatua za haraka zichukuliwe.