1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa madaktari Uganda wasababisha maafa

Iddi Ssessanga
8 Novemba 2017

Madaktari wa hospitali za umma nchini Uganda wamegoma kupinga mishahara duni na uhaba wa vitendea kazi, hali iliyopelekea baadhi ya wagonjwa kufariki, hali inayotishia kuzidisha hasira za raia dhidi ya serikali.

https://p.dw.com/p/2nIXe
Uganda Krankenhaus Symbolbild
Picha: AFP/Getty Images/I. Kasamani

Madhara ya mgomo huo yameanza kushuhudiwa miongoni mwa wagonjwa na jamaa na marafiki wa watu wanaoendelea kupoteza maisha yao ikiwemo watoto na akina mama waja wazito. Mtangazaji maarufu wa michezo nchini Uganda Peter Otai hapo jana jioni alimpoteza babake mzazi pale alipomkimbiza hospitali kuu ya Mulago lakini akakosa kuhudumiwa.


"Mimi binafsi ninasononeka sana kwamba babangu amefariki jinsi hii kwa sababu madaktari wamegoma. Siku zote nitasema babangu hakufa kutokana na saratani lakini hospitali ya Mulago ilimuua. Amekufa kwa uchungu mwingi," alisema  Otai.

Taarifa za hospitali kadhaa sehemu mbalimbali za nchi zaelezea kuwa wagonjwa wengi wameamua kurudi makwao au kwenda kwenye vituo binafsi vya afya baada ya kukosa matumaini ya kushughulikiwa na madaktari ijapokuwa wauguzi wanaendelea kuwahudumia. Chini ya shirikisho lao, wauguzi wameamua kutojiunga kwa mgomo huo.

Mkutano kati ya madaktari na kundi la mawaziri jana jioni haukuzaa matunda yoyote madaktari wakisisitiza kuwa watasitisha kwa muda mgomo huo iwapo serikali italipa mafao na posho zinazodaiwa na madaktari wakufunzi huku wakisubiri kukutana na rais Yoweri Museveni wiki ijayo tarehe 17 Novemba.

Uganda Krankenhaus Symbolbild
Mgomo wa madaktari umewaacha wagonjwa wakikosa huduma.Picha: AFP/Getty Images/M. Sibiloni

Hii ina maana kuwa wagonjwa na jamaa zao wanaotegemea vituo vya afya vya serikali wangali katika mashaka makubwa kuhusiana na masuala ya kupata matibabu. "Tunatoa kilio kwa serikali iwalipe madaktari mishahara stahiki," alisema Grace Nakato, aliyekuwa amempeleka mgonjwa hospitali ya Naguru akitaraji kwamba madaktari wangewahurumia na kuwashughulikia.

Mishahara duni

Mgomo wa mwisho kama huo kufanywa na madaktari ulikuwa zaidi ya miaka 20 iliopita. alisema Faustus Kavuma kutoka chama cha Madaktari Uganda, ingawa migomo midogomidogo hufanyika mara kwa mara. "Ukosefu wa dawa na vifaa katika hospitali laazima ukome," alisema na kuongeza, "malipo yetu ni duni sana."

Alisema madaktari wanakosa mahitaji muhimu kama vile glavu, dawa za kutuliza maumivu na kuzuwia mambukizi. Daktari wa ngazi ya kwanza katika sekta ya afya ya umma nchini Uganda hulipwa karibu shilingi milioni 1.1, sawa na dola 300 kwa mwezi. Daktari mwandamizi analipwa karibu shilingi milioni 3.4.

Baadhi ya watu waliozungumza na DW wakiwemo wanasiasa wa upinzani wameishtumu serikali kwa kupuuzilia maslahi ya madaktari na wananchi kwa jumla huku. Wanashangaa kwa nini serikali iliweza kupata kwa haraka pesa za kuwapa wabunge kwenda kushauriana na wananchi kuhusu muswaada wa kuondoa ukomo wa umri wa rais ili hali hazikuwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha kama ilivyo kwa upande wa afya ya wananchi.

Chama cha Madaktari kinataka mishahara ya wanachama wake ilipandishwe hadi milioni 8.5 na milioni 45 mtawalia, alisema Kavuma. Mgomo huo utachochea ukataji tamaa wa raia na utawala wa Rais Yoweri Museveni, ambao tayari unakumbana na ghadhabu zao kuhusiana na mpango wa kurefusha utawala wake wa miaka 35.

Uganda Proteste und Ausschreitungen in Kampala
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere wakiandamana kupinga kuondolewa kwa ibara inayoweka ukomo wa umri kwa nafasi ya rais nchini Uganda.Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Fedha zatumika kurefusha utawala wa Museveni

Museveni mwenye umri wa miaka 73 kwa sasa anazuwiwa kuwania muhula mwingine katika uchaguzi ujao wa 2021 kwa sababu katiba inaweka ukomo wa umri wa miaka 75 kwa wagombea urais. Chama tawala cha NRM kinataka kuondoka ibara juu y aukomo huo, kikiungwa mkono na rais.

Hatua hiyo imesababisha maandamano yaliokandamizwa kwa kutumia gesi za kutoa machozi na risasi na moto. Watu wasiopungua wawili wameuawa tangu kuanza kwa maandamano hayo.

Diana Atwine, katibu muu wa wizara ya afya, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali iko tayari kuongeza mishahara ya madaktari na kushughulikia masuala yao mengine lakini wanapaswa kuwa na subira.

"Tatizo hilo linahitaji mkakati mpana kwa sababu siyo madaktari wasiolipwa vizuri. Watumishi wote wa umma hawalipwi vizuri," alisema. Kamati iliundwa, alisema, kutathimini mishahara ya wafanyakazi wote wa umma na kutoa mapendekezo.

Mwezi uliopita, serikali iliwapa wabunge fedha za ziada kiasi cha dola 8,000 kufanya mikutano ya mashauriano kuhusu muswada wa kurefusha utawala wa rais Museveni. Wabunge tayari wanalipwa kiasi cha dola 5,900 kila mwezi.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga