1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa walimu nchini Kenya

6 Septemba 2011

Shughuli za masomo zimetatizwa leo katika shule za umma nchini Kenya kufuatia mgomo uliotishwa na chama cha kitaifa cha waalimu nchini humo.

https://p.dw.com/p/12Tha
Wanafunzi wa shule jijini NairobiPicha: picture-alliance/photoshoot

Mwandishi wetu Alfred Kiti kutoka Nairobi ametuandalia taarifa hiyo.

Kwenye mkutano ulioitishwa katika ofisi ya Waziri mkuu uliojumuisha maafisa wa wizara ya Fedha Wizara ya Elimu na chama cha walimu nchini, suluhisho halikupatikana na hivyo maafisa wa chama hicho wakiongozwa na katibu mkuu David Okuta wakaamua kuendeleza mgomo huo hadi serikali itakapotimiza matakwa yao.

Chama hicho kilitoa ilani ya mgomo huo wiki moja iliyopita na kuipa serikali muda siku saba kuytimiza masharti yao.

Miongoni mwa matakwa yaliyotolewa na chama hicho ni kuajiriwa kwa walimu wengine alfu kumi na kupewa kandarasi za kudumu walimu alfu 18 wanaohudumu kama vibarua.

Mwenyekiti wa chama kitaifa cha walimu nchini Kenya Wilson Sission anasema….

“Serikali iliacha kuajiri walimu mwaka 1998 kufuatia masharti ya Benki ya Dunia na iliporejelea mwaka 2001 iliajiri tu walimu kujaza mapengo yanayoachwa wazi na wale wanaostaafu au kufariki na hiyo ni kumaanisha serikali haijaajiri walimu wengine kwani idadi bado ni ile ya 235,000”

Serikali kupitia katibu wa wizara ya Elimu imeomba muda zaidi kufanya mashauri huku Wizara ya Fedha ikisisitiza kwamba hakuna fedha za kuajiri walimu wapya..

Katibu katika wizara ya Elimu Joseph Kinyua anasema..

“Kuongeza mzingo mwingine ni changamoto kubwa kwa serikali na hiyo itahitaji kutafuta mbinu mbadala bila kuwatwika Wakenya mzigo wa kodi ziada”

Hata hivyo katibu katika wizara ya elimu Prof. James Ole Kiyapi anasema..

“Katika muda wa wiki hii serikali itashauriana kutafuta ni jinsi gani tutakavyoweza kutatua tatizo hilo”

Tangu kuanza kwa mfumo wa elimu ya msingi bila malipo miaka minane iliyopita kumekuwa na uhaba wa walimu kufuatia ongezeko la idadi ya wanafunzi katika shule za umma. Serikali imekiri kwamba kuna upungufu wa walimu alfu 70 katika shule za umma kote nchini.

Mgomo huo bila shaka utatatiza masomo hasa kwa wanafunzi wanaofanya mtihani wao wa kitaifa mwishoni mwa muhula huu ulioanza hapo jana

Mwandishi: Alfred Kiti DW Nairobi.

Mhariri: Othman Miraji