1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wakwamisha huduma nchini Ugiriki.

Abdu Said Mtullya11 Machi 2010

Huduma mbalimbali za umma zimesimama nchini Ugiriki kutokana na mgomo wa saa 24.

https://p.dw.com/p/MQaD
Maalfu ya watu walioshiriki katika mgomo wa saa 24 nchini Ugiriki.Picha: AP

Wafanyakazi katika sekta ya  binafsi na watumishi katika sekta ya umma leo wameendelea na mgomo  nchini Ugiriki kote na  kutokana  na hayo huduma za usafarishaji zimesimama, shule  zimefungwa na ndege hazikuruka.

Sababu ya mgomo huo ni kupinga mpango wa kubana matumizi uliopitishwa na serikali ya nchi hiyo.

Katika mitaa ya mji mkuu wa Ugiriki, Athens leo vilisikika vipaaza sauti vilivyotangaza vidokezo juu ya kuwataka tajiri wa Ugiriki walipe deni kubwa linaloikabili nchi hiyo. Vipaaza  sauti  hivyo  vilitangaza vidokezo hivyo huku maelfu ya watu wakiandamana kupinga kukatwa kwa mishahara ya watumishi wa serikali, kupinga kupandishwa kodi, kutoongezwa kwa pensheni na kupinga kupandishwa kwa umri wa kustaafu.

Waandamanaji walisema kwa sauti za juu kwamba watu wa Ugiriki hawapo tayari kuwalipia  tajiri. Watu wameuliza jee  fedha zimeenda wapi?

Kutokana na shinikizo kutoka  kwa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya na kutokana na shinikizo la masoko,kuitaka Ugiriki ichukue hatua zaidi ili kuukabili mgogoro wake  wa madeni, serikali ya nchi hiyo  ilipitisha  wiki jana, mpango wa kubana matumizi ili kupata kiasi cha Euro bilioni  4 .8  kwa kukata matumizi na  kupandisha kodi.

Serikali ya Ugiriki itautekeleza mpango huo, licha ya mgomo huo mkubwa wa saa 24 unaoongozwa na jumuiya za wafanyakazi zenye wanachama milioni mbili na  nusu.

Hatahivyo ingawa Wagiriki   wengi wanakubaliana na serikali kwamba hatua ilizochukua ni za lazima,  kwa jumla inaaminika kwamba hatua hizo zinawabana wasiokuwa na hatia, katika  nchi ambamo rushwa imeshtadi na ukwepaji kodi umetanda.

Maalfu ya wafanyakazi kwenye viwanja  vya ndege, na katika sekta nyingine za usafirishaji walishiriki katika mgomo kwa kuandamana.

Palitokea ghasia ambapo  polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwakabili waandamaji waliokuwa  wanawatupia polisi hao mawe. Watu alfu 50 walishiriki katika maandamano ya leo mjini Athens.

Serikali ya Ugiriki ilitangaza mpango wa kubana matumizi ili kuthibitisha uhakika kwamba ina uwezo wa kulikabili deni lake la Euro bilioni 300.

Mwandishi: Mtullya Abdu/RTRE/ZA

Mhariri:  Josephat Charo