1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 10 madarakani; Rais Al-Assad wa Syria akosolewa kwa ukandamizaji wa haki.

13 Julai 2010

Syria ni kati ya nchi zinazokandamiza zaidi uhuru wa uandishi habari duniani.

https://p.dw.com/p/OINV
Rais Bashar al-Assad wa Syria ameimarisha uhusiano na makundi ya Hezbollah na Hamas.Picha: AP

Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameanza kulegeza masharti katika nchi yake yenye uchumi dhaifu lakini mabadiliko hayo hayapo katika siasa. Mwongo wake wa kwanza madarakani unaoadhimishwa mwezi huu, unamalizika kukiwa na ukandamizaji zaidi ya ulivyoanza. Hayo hayajazivunja moyo nchi za magharibi kujaribu kuisaidia Syria kutokana na miaka kadhaa ya kutelekezwa kutokana na ushawishi wake Lebanon, kuwaunga mkono maadui wa Marekani katika vita vya Iraq mwaka wa 2003 na kuyasaidia makundi ya kiislamu yanayopigana na Israel.

Syria bado inawaweka ndani wapinzani wake na hulaaniwa tu na Marekani na washirika wake wa Ulaya kwa maneno matupu, huku nchi za Kiarabu zikibakia kimya. Mahakama moja ya kijeshi ilitoa hukumu ya miaka mitatu gerezani dhidi ya wakili wa miaka 79, Haitham al-Maleh kwa kile kilichoitwa kudhoofisha motisha wa taifa.

Al-Maleh alikamatwa mwaka jana baada ya kurejea tena wito wa kutaka kuondolewe kwa sheria ya hali ya hatari ya mwaka 1963 inayopiga marufuku upinzani wowote dhidi ya chama tawala cha Baath.

Mwezi juni, wakili mwingine alitiwa gerezani kwa tuhuma kama hizo na mwandishi alikamatwa tena siku moja baada ya kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani. Wapinzani watano wa kisiasa waliachiliwa baada ya kuwa gerezani kwa tuhuma kama hizo na mbunge wa zamani, Raid Seif bado yuko gerezani.

Kutokana na hayo, Nadim Houry, mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadam, Human Rights Watch mjini Beirut, anasema rais Assad anatuma ujumbe kwamba hajali kuhusu haki za binaadamu na mabadiliko ya kisiasa nchini Syria na kwamba hadhanii jumuiya ya kimataifa inajali na inaweza kumwekea vikwazo kwa sababu ya hayo.

Hotel Ebla Cham Palace Damascus
Mahoteli ya kifahari mjini Damascus ni kati ya miundo mbinu inayong'ara mjini humo. Rais Al-Assad adaiwa kuipa kipau mbele biashara bila mabadiliko kisiasa na katika idara ya mahakama.Picha: IMPORT

Mji mkuu wa Syria, Damascus umekuwa uking’ara katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ukiwemo mahoteli ya kifahari na migahawa, majengo maalum ya ununuzi pamoja na mabenki ya kibinafsi na miradi ya ujenzi, lakini wachunguzi wanasema uhuru huo wa kibiashara umewafaidi wafanyabiashara wachache wenye uhusiano wa ngazi ya juu huku ufisadi ukikithiri. Wachunguzi hao wanatathmini ikiwa mabadiliko ya kiuchumi nchini Syria yanaweza kufaulu bila mabadiliko ya kisiasa na katika idara ya mahakama.

Ingawa ukosoaji wa umma kuhusu uchumi unavumiliwa, mengi yanasalia yalivyo, ukiwemo mfumo wa ulinzi ambao rais Assad alirithi kutoka kwa baba yake aliyetisha, marehemu Hafez al-Assad.

Joshua Landis, mtaalam kuhusu masuala ya Syria katika chuo kikuu cha Oklahoma, Marekani anasema serikali bila shaka inadhani kwa kuwadhibiti raia na kuweka mipaka fulani tu ya uhuru hatimaye itakumbwa na matatizo madogo .

Bw Landis alikiri kwamba Syria imezungukwa na nchi ambazo zimekumbwa na vita virefu vya wenyewe kwa wenyewe na uasi, zikiwemo Iraq, Lebanon, Uturuki, na pia mzozo kati ya Israel na Palestina na kwamba idara ya usalama wa Syria haiwezi kulegeza kamba. Baada ya kuingia madarakani mwezi julai mwaka wa 2000, rais Assad aliwaachia wafungwa kadhaa wa kisiasa na aliruhusu mjadala juu ya demokrasia na mabadiliko kisha akabadilisha mwelekeo miezi michache baadaye.

Miaka miwili iliyopita Bw Assad amekuwa na uhusiano wa karibu na Iran, Uturuki na Qatar na amerejesha uhusiano na Saudi Arabia na pia amefufua ushirikiano na Lebanon ikiwemo kuendeleza uhusiano na kundi la Hezbollah nchini humo na pia vuguvugu la Wapalestina la Hamas.

Kulingana na shirika la waandishi wa habari wasiokuwa na mipaka ‘Reporters without Borders’, Syria ni kati ya nchi zinazowakandamiza zaidi watumiaji wa mitandao ya Internet na Skype, Facebook na Youtube imepigwa marufuku na waandishi habari wanaotumia blogi kama majukwaa ya kukosoa huandamwa.

Tathmini ya uhuru wa uandishi habari ya mwaka wa 2009, iliitaja Syria kama nchi isiyotilia maanani uhuru huo ikiwa nafasi ya165 miongoni mwa orodha ya nchi 175.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed