1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 15 tangu wazungu awalipoamua ku´ngoa utawala wa kibaguzi Afrika kusini

Mohammed Abdul-Rahman16 Machi 2007

Leo hii Afrika kusini inajivunia demokrasia.

https://p.dw.com/p/CHI0
Nelson Mandela na FW.de Klerk, wanasiasa waliofikia maelewano na kuleta demokrasia Afrika kusini.
Nelson Mandela na FW.de Klerk, wanasiasa waliofikia maelewano na kuleta demokrasia Afrika kusini.Picha: AP

Miaka 15 iliopita, kura ya maoni ilioitishwa na Rais de Klerk kuwataka wazungu waamuwe juu ya pendekezo la kuin´goa sera ya ubaguzi, iliidhinishwa na asili mia 69 ya wapiga kura karibu milioni mbili waliolikubali pendekezo hilo. Matokeo hayo yakawa ndiyo mwanzo wa kumalizwa kwa utawala huo wa ubaguzi wa rangi.

Kilichofuata baada ya utaratibu uliosababisha kuachiwa huru mpigania uhuru na demokrasia Nelson Mandela baada ya kuwa gerezani kwa miaka 27, ni pamoja na mazungumzo rasmi na chama cha African National Congress-ANC, na hatimae kufanyika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasi 1994 na kupatikana utawala wa waafrika walio wengi.

Leo hii raia wa Afrika kusini kuitathimini vipi hali ilivyokua ? Bila shaka haikua sawa kisiasa kwamba jamii ya wachache walio wabaguzi iwe na usemi na mamlaka ya kuwatawala walio wengi. Mmoja kati ya waliopiga kura hao bado anakumbuka akisema :-

“ Mimi nilisema NDIYO. Ni miaka 15 mizuri, na ninafuraha kuona jinsi mambo yalivyokwenda na watu kuchanganyika na kufanya kazi pamoja kama jamii moja kubwa bila ya kipingamizi cha mtu binafsi au rangi.

Nafikiri mambo yanakwenda kwa pamoja na yanakwenda vizuri kabisa……vizuri zaidi kuliko ambavyo mtu angetegemea .”

Lakini raia huyu mzungu pamoja na kujikuta kwamba kulikua na wenzake katika jamii yake mwenyewe waliokua na msiamamo wa kibaguzi, anasema daima yeye na familia yake walikua na mtazamo na msimamo mwengine ……anaeleza kuwa:-

“Hatukupata kukipigia kura chama tawala cha National, daima tulikuza upinzani na wakati wote tuliuunga mkono upinzani kwa kila namna. Lakini yapaswa kukumbukwa tulikua tukiishi katika Afrika kusini ambako hakukua na chaguo jengine wakati ambapo sote tulikua ni waafrika kusini. Hata wakati ule hatukuunga mkono suala lolote la kibaguzi. Tulihisi mabadiliko yalihitajika na tulifurahi mno kuona mabadiliko, yalipotokea.”

Hayo ni maoni ya mwaafrika kusini mzungu aliyeamni kwamba sera ya ubaguzi ilikua ni kosa . Lakini bado wako ambao wanahisi vyengine na hawapendezwi na hali ilivyo. Mmoja wao ni huyu anayemiliki mkahawa mmoja nchini humo. Yeye ana maoni kuwa :-

“Ni mbaya kabisa, kwa sababu imani imebadilika kwa kila mtu. Hakuna uadilifu wa kitu chochote tena .

Lakini hatuwezi kuirejesha saa nyuma. Ni vizuri kwamba mabadiliko yametokea, lakini mambo yamegeuka haraka mno. Tatizo ni kwamba hakuna idadi ya kutosaha ya wenye ujuzi wa kutosha na kuna wengi wamewekwa katika makazi na nyadhifa bila ya kuwa na ujuzi wala uzoefu. Hilo ni tatizo moja wapo na pia uhalifu. Na ndiyo maana watu wengi wanahama.”

Matarajio kwa mtazamo wa wengi bado hayajafikiwa, kwa sababu mbali mbali. Moja wapo kubwa kwa mujibu wa raia huyu ni :-

“Rushwa kwa mfano. Mpango wa kuwapa nguvu kiuchumi waafrika unaelekea bado kuwanufaisha walio wachache na sio walio wengi. Na pia sasa wazungu hawana nafasi kubwa katika ajira. Mara nyingi si yule mwenye ujuzi anayekua na nafasi ya kupewa kazi.”

Kilio kikubwa cha waafrika walio wengi mbali na kuitaka serikali kupiga vita rushwa kivitendo, bado ni ukosefu wa ajira, maji safi na makaazi. Lakini pamoja na maoni tafauti juu ya mafanikio yaliopatikana tangu kura ya maoni ya wazungu juu ya kungolewa sera ya ubaguzi nchini Afrika kusini miaka 15 iliopita, wengi katika jamii hiyo wana matumaini juu ya hali ya siku zijazo katika Afrika kusini ya leo-Afrika kusini ya Kidemokrasi.