1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 20 ya Muungano wa Ujerumani.

Abdu Said Mtullya27 Oktoba 2010

Rais wa Ujerumani Christian Wulff asema Uislamu pia ni sehemu ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/PU7x
Rais wa Ujerumani Christian Wulff akisalimiana na wananchi.Picha: dapd

Rais wa Ujerumani Christian Wulff ametoa mwito wa kuwajumuisha katika jamii waislamu milioni nne wanaoishi nchini Ujerumani.

Rais Wulff alitoa mwito huo katika maadhimisho ya mwaka wa 20 wa muungano wa Ujerumani.Rais wa Ujerumani amesema waislamu sasa ni sehemu ya jamii ya Ujerumani.

Kiongozi huyo wa Ujerumani alikumbusha katika hotuba yake kwamba katika mchakato wa nchi 2 za kijerumani kuungana tena, wajerumani walisema kuwa wao ni watu wamoja,lakini ameeleza kuwa sasa kauli hiyo haina maana ya kuwaunganisha wajerumani wa mashariki na magharibi tu. Hayo yanawahusu wahamiaji pia wanaoishi nchini Ujerumani.

Hatahivyo Rais wa Ujerumani amekiri kwamba bado yapo mengi yanayopaswa kufanyika.Wulff amesema kuwa yeye siyo rais wa wajerumani tu bali pia ni wa waislamu wote wa nchini Ujerumani.

Katika hotuba yake rais Wulff ameitaka Ujerumani ifanye juhudi katika kuwatangamanisha na jamii waislamu milioni nne wanaoishi nchini Ujerumani.

Katika hotuba yake pia alizungumzia juu ya matatatizo yaliyopo katika mchakato wa kuwajumuisha waislamu hao katika jamii.Amesema pana haja ya kutoa fursa kwa ajili ya familia za wahamiaji na hasa katika kujifunza lugha ya kijerumani. Hatahivyo Rais Wulff amesisitiza kwamba Uislamu pia ni sehemu ya Ujerumani na amewataka wajerumani wawe watu wenye uwazi na stahamala.

Rais wa Ujerumani ameeleza kuwa Ujerumani pia inapaswa kuzitambua tofauti zilizopo. Rais wa Ujerumani ameeleza kwamba nchi zenye mustakabal mzuri ni zile zinazokubali tamaduni mbalimbali katika jamii.

Akizunguma kuadhimisha miaka 20 ya muungano wa Ujerumani naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kwamba wajerumani wameweza kuijenga upya nchi yao haraka kutokana na juhudi za pamoja za watu wa mashariki na magharibi.

Maadhimisho ya miaka 20 ya muungano wa Ujerumani yalianza kwa sala katika mji wa Bremen iliyoongozwa na Askofu wa kanisa katoliki Franz-Josef Bode kwa kushirikiana na kasisi wa kanisa la kiprotestanti, Renke Brahms.kilele cha sherehe kilifikiwa katika mji mkuu-Berlin.

Mwandishi Mtullya abdu/Dpa/ZPR

Mhariri/...Josephat Charo