1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 20 ya Muungano:Mafanikio na changamoto mpya

3 Oktoba 2010

Ujerumani imeadhimisha miaka 20 tangu eneo la Mashariki lilipoungana na Magharibi na kuwa nchi moja.Sherehe hizo zimefanyika mjini Bremen na zimehuhduriwa na viongozi kadhaa akiwemo Kansela Merkel

https://p.dw.com/p/PTLn
Rais wa Ujerumani Christian Wulff na Kansela Angela Merkel wakiwa mjini Bremen kwenye sherehePicha: dapd

 Rais wa Ujerumani Christian Wulff aliwapongeza walioshiriki kwenye harakati za kuutokomeza ukomunisti katika siku ya kuadhimisha miaka 20 tangu Ujerumani Magharibi na Mashariki ilipoungana na kuwa nchi moja.Katika hotuba yake ya kwanza muhimu,Rais Wulff aliikumbuka siku  na tukio hilo la kihistoria ambalo ni nadra kutokea,wakati ambapo Ujerumani ya Magharibi iliyokuwa ikiufuata mfumo wa kibepari na Mashariki iliyokuwa ya Kikomunisti ziliungana mwaka mmoja baada ya Ukuta wa Berlin kuangushwa.

‘Ninawasujudia wote walioupigania uhuru huu….ujasiri wenu uliutikisa ulimwengun mzima',alisema Rais Christian Wulff alipowahutubia viongozi muhimu waliohudhuria sherehe hizo za kilele akiwemo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy.Umati huo ulimpigia makofi ya kilo.

Dini na jamii

Hata hivyo Rais Wulff alizielezea changamoto zinazoikabili Ujerumani hususan suala zito linalozua mitazamo tofauti la kuwajumuisha pamoja Waislamu katika jamii hii.Suala hilo limezua mijadala mikali katika kipindi cha wiki chache zilizopita.Alisema,'Miaka 20 baada ya kuungana na kuwa kitu kimoja,bado tunakabiliwa na kibarua kigumu cha kudumisha umoja katika nchi ya Ujerumani ambayo ni sehemu ya ulimwengu unaobadilika''. 

Kuhusu suala la dini,Rais Wulff alifafanua kuwa,'Ukristo ni sehemu ya jamii za Ujerumani.Hiyo ni historia yetu iliyotokea kwenye misingi ya Kiyahudi na Kikiristo.Hata hivyo kwa sasa Uislamu ni sehemu pia ya Ujerumani''.

Wakati huohuo,aliwataka wote wanaoishi Ujerumani kuifuata misingi ya katiba ya nchi pamoja na mfumo mzima wa maisha vilevile kujifunza lugha ya Kijerumani.

Feier zum Tag der Deutschen Einheit in Bremen 2010 Flash-Galerie
Kansela Angela Merkel akielezea maisha ya MasharikiPicha: dapd

Kwa upande wake,Kansela Merkel wa Ujerumani aliyekulia eneo la Mashariki ya Ujerumani alikumbushia maisha yalivyokuwa wakati wa uongozi uliojikita katika mfumo wa kikomunisti.Alieleza kuwa endapo Ukuta wa Berlin haukuangushwa,pengine angelazimika kuwa mwanasayansi wa moja kwa moja.   

 Tamu na Uchungu

Bibi Merkel aliye na umri wa miaka 56,anayeaminika kuwa mmoja ya wanawake walio na madaraka makubwa ulimwenguni,alilielezea gazeti la Jumapili la Bild am Sonntag kuwa,ijapokuwa maisha katika Ujerumani ya Mashariki ya zamani yalikuwa na changamoto zake,''bado yalikuwa na mazuri yake pia'',alifafanua kuwa,''tuliweza kusoma vitabu,kusafiri hadi maeneo ya Ulaya ya Mashariki…..maisha katika Ujerumani mashariki yalikuwa magumu na vikwazo vyake, ila tuliyafurahia kadri ya uwezo wetu,'' alieleza Bibi Merkel aliyesomea udaktari.

Feier zum Tag der Deutschen Einheit in Bremen 2010 Flash-Galerie
Kansela Merkel akiwapa mkono waliohudhuria sherehe za miaka 20 za MuunganoPicha: dapd

Muda mfupi baada ya hotuba hiyo Rais wa Marekani Barack Obama aliipongeza Ujerumani na Wajerumani waliofanikiwa kuuangusha Ukuta wa Berlin kwasababu ya ujasiri na imani yao isiyotetereka.Hatua hiyo ilikihitimisha kipindi kigumu kilichowalazimu wengi kutengana kwa njia isiyokuwa ya kawaida.Urusi nayo iliipongeza Ujerumani vilevile naye Rais wake Dmitry Medvedev alisema kuwa,''Muungano huo una umuhimu mkubwa kihistoria si tuu kwa Wajerumani bali pia kwa wakazi wote wa Ulaya''.      

Baada ya vita vya pili vya dunia,mataifa yaliyoibuka washindi ya Marekani,Uingereza,Ufaransa na Muungano wa Kisovieti yaliigawanya Ujerumani kuwa vipande vinne.Muda mfupi kabla ya vita baridi kuanza,Urusi ililitenga eneo la mpaka wake kwenye eneo la Mashariki na mengine matatu ya Magharibi likiwemo eneo la Ukuta lililougawanya mji wa Berlin vipande viwili.

Kabla ya mwaka mmoja kupita baada ya ukuta wa Berlin kuangushwa kwenye mapinduzi ambayo hayakusababisha umwagikaji wowote wa damu,ilipofika tarehe 3 mwezi wa Oktoba mwaka 1990,makubaliano ya kuyaunganisha maeneo ya mashariki na magharibi ya Ujerumani yalianza kufanya kazi na ikawa nchi moja.Jambo hilo liliwafurahisha wengi.

Muungano ni jambo la msingi

Tangu wakati huo,siku hii huadhimishwa kwani ni siku ya kitaifa ya Ujerumani.Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni,asilimia 84 ya Wajerumani wanaamini kuwa muungano huo una manufaa zaidi na lilikuwa jambo la busara la kufanya ijapokuwa bado kuna tofauti za kiuchumi kati ya eneo la magharibi na mashariki.Maeneo hayo yalitengwa kwa muda wa miongo minne.

Kulingana na asilimia 14 pekee,hatua hiyo ya kuyaunganisha maeneo hayo ilikuwa kosa kama ilivyoeleza tathmini ya kura ya maoni yaliyofanywa na kituo cha televisheni cha kitaifa ZDF.    

Kwa sasa Ujerumani iko mstari wa mbele katika jukwaa la kimataifa la kisiasa na inaongoza kiuchumi barani Ulaya.Hata hivyo bado inakabiliwa na changamoto za kuyasawazisha maeneo ya Mashariki na Magharibi.

Feier zum Tag der Deutschen Einheit in Bremen 2010 Flash-Galerie
Picha za lango la Brandenburg:Nembo ya UmojaPicha: picture-alliance/dpa

Euro trilioni 1.3!

Eneo la Mashariki linakabiliwa na uhaba wa nafasi za ajira ulioongezeka maradufu kadhalika hali ya maisha kwa jumla iko chini ikilinganishwa na ile ya wakazi wa magharibi ijapokuwa limekuwa likipokea kiasi ya euro trilioni 1.3 kutoka kwa majirani wao. 

Sherehe hizo zimefanyika kukiwa na ulinzi mkali na usalama ulioimarishwa baada ya kiasi ya wanaharakati 1800 wa mrengo wa shoto kuandamana mjini Bremen hapo Jumamosi jioni.Ili kukihitimisha kipindi hicho cha historia isiyofurahisha ya Ujerumani,serikali ilililipa deni lake la mwisho la kiasi cha euro milioni 70 za fedha zilizotumika kufadhili vita vya kwanza vya dunia.

Shamrashamra hizo zitahamia katika mji mkuu wa Berlin ambako matamahsa kadhaa yameandaliwa kwenye barabara zinazoelekea kwenye majengo ya bunge pamoja na lango kuu la mji la Brandenburg.

Mwandishi:Wagener,Volker

Mtafsiri:Thelma Mwadzaya