1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 25 tangu ajali ya kemikali ya Bhopal

3 Desemba 2009

Mamia ya wakaazi wa mji wa Bhopal nchini India wanaamdamana leo katika kumbukumbu ya miaka 25 ya ajali iliotokea kwenye kiwanda kimoja cha madawa mjini humo. Watu wapatao 3.500 walikufa kutokana na kuvuja gesi kiwandani

https://p.dw.com/p/KpVq
Kiwanda cha Bhopal,IndiaPicha: AP

Waandamanaji katikati ya jiji la Bhopal la India, wanadai huduma za afya za muda mrefu na fidia ya kutosha kwa walioathiriwa na gesi iliyovuja kutoka katika kiwanda hicho miaka 25 iliyopita.Kiasi ya watu 3,500 walikufa papo hapo kutokana na gesi hiyo mnamo tarehe 3 Desemba mwaka 1984, katika tukio hilo la mauaji makubwa zaidi yaliyosababishwa na kemikali za viwandani.

Wiki zilizofuatia, watu wengine 15,250 waliovuta hewa au kunywa maji yaliyoathiriwa na gesi hiyo walikufa, ingawa kwa mujibu wa takwimu za vikundi vya haki za binadamu, idadi ya vifo ilifikia watu 25,000.

Fidia haitoshi

Vikundi hivyo vimekuwa vikidai fidia ya kiungwana na matibabu kamili, vikisema kuwa malipo ya kiasi cha dola milioni 450 kilichokubaliwa awali, hakitoshi kuhudumia maelfu ya watu walioathirika.

Kinder mit körperlichen Behinderungen in Bhopal
Mtoto aliyeathiriwa na gesi za sumuPicha: Pia Chandavarkar

Wanasema maelfu ya watu waliokuwa wanaishi jirani na kiwanda hicho wanaugua magonjwa ya pumu, saratani na wengine wengi wameathirika kisaikolojia.

Kikundi kimoja cha kinachopigania haki za binadamu jijini humo cha Bhupol Group of Infomation and Action, kimesema watoto waliozaliwa baada ya janga hilo, wameonesha dalili za saratani, pamoja na magonjwa mengine sugu.

Waathirika wa janga hilo pia wanadai hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika, na kusafishwa kwa mazingira machafu yaliyopo sasa kiwandani hapo.

Indien Ministerpräsident Manmohan Singh
Waziri Mkuu wa India Manmohan SinghPicha: picture-alliance/ dpa

Katika taarifa yake Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh, alitoa salamu za rambi rambi kwa jamaa wa marehemu na pole kwa wanaoendelea kuathirika kiafya kutokana na ajali hiyo ,alisema ,''Serikali imedhamiria katika kufumbua masuala yote yanayohusiana na janga hilo, ikiwemo maji safi ya kunywa, usafi katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho pamoja na utafiti wa tiba kuwasaidia wale walioathirika.''

Robo karne imepita sasa tangu dhahama hiyo ilipotokea, kiwanda hicho hakitumiki tena na kimetelekezwa, lakini nyuma ya milango mikubwa ya vyuma ya kiwanda hicho, kuna kile wanaharakati wa mazingira wanachokiita "janga ndani ya janga", ambapo kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni, hewa ya eneo hilo bado ina chembechembe za sumu ambazo zinaathiri maji ya kunywa kwa mamilioni ya wananchi wa India.

Sumu imehifadhiwa

Karibu tani 340 za kemikali zilizoharibika zimehifadhiwa katika maghala ndani ya kiwanda hicho, ambayo yanahitaji kuteketezwa.

Kampuni ya Dow Chemical imekana kuhusika na tukio hilo, ikisema kuwa ilikinunua kiwanda hicho miaka kumi iliyopita baada ya tukio hilo.

Serikali kwa miaka kadhaa imekuwa ikiyapinga madai kwamba vyanzo vya maji katika eneo hilo vina sumu ya gesi hiyo, ikisema kuwa tafiti mbalimbali za kiserikali zimeonesha hakuna uthibitisho wowote wa kuwepo sumu kwenye maji.

Mwandishi:Lazaro Matalange/RTRE/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman