1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 30 ya uhusiano wa kibalozi baina ya Uchina na Marekani

Miraji Othman7 Januari 2009

Ni miaka 30 sasa tangu Beijing na Washington kuwa na uhusiano wa kibalozi

https://p.dw.com/p/GTvz
Marehemu Richard Nixon, rais wa Marekani aliyesababisha kuanzishwa uhusiano kamili wa kibalozi baina ya nchi yake na Uchina.Picha: AP

Viongozi wa Uchina na Marekani wameupongeza uhusiano wa kibalozi baina ya nchi zao mbili uliodumu sasa kwa miaka 30, na kuuelezea kwamba ni moja ya uhusiano ulio wazi kabisa kupatikana katika karne ya 20. Lakini serekali za nchi hizo mbili zinasheherekea maadhimisho ya tokeo hilo kwa ukimya, bila ya mbwembwe. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, ameivunja ziara alioipanga kuifanya mjini Beijing kuhudhuria sherehe za maadhimisho hayo ili aweze kuushughulikia mzozo wa Mashariki ya kati unaozidi.

Kutokana na mzozo mkubwa kabisa wa kiuchumi ambao pande mbili hizo zimejionea tangu kuanzisha tena uhusiano wao hapo mwaka 1979, maadhimisho haya ni wakati wa kutafakari kwa pande zote mbili. Dai Bingguo, afisa wa cheo cha juu katika serekali ya Uchina, amesema katika kipindi kifupi cha miaka 30, na kwa juhudi za pamoja za vizazi wa viongozi wa Uchina, marais saba wa Kimarekani na wananchi wa nchi zote mbili, meli ya uhusiano baina ya Uchina na Marekani imesonga mbele, bila ya kujali kunanyesha mvuwa au juwa linawaka. Amesema uhusiano huo umeleta mafanikio mengi kwa watu wa nchi hizo mbili na umechangia sana kwa amani ya dunia na maendeleo.

Maadhimisho haya yanasheherekea ule uamuzi wa Marekani wa kuvunja uhusiano wake wa kibalozi na Taiwan, na badala yake kuanzisha uhusiano na Uchina Bara ya kikoministi hapo Januari Mosi, mwaka 1979. Mabadiliko hayo ya kibalozi yaliwezekana kutokana na ile ziara maarufu iliofanywa na Rais Richard Nixon huko Beijing mwaka 1972 na ile ya kulipizia iliofanywa na Deng Xiaoping huko Marekani.

Kuwa wa kawaida uhusiano huo kulisadifu na uamuzi wa Uchina kuanzisha marekebisho ya masoko huru. Chama cha kikoministi cha nchi hiyo kiliamuwa hapo Disemba mwaka 1978 kuruhusu kuweko ukulima wa kibinafsi, hatua ilioachana na ile fikra ya Mao Tse Tung ya kuwa na ukulima wa kijamaa.

Uhusiano huo umeisaidia Uchina kuibuka kama nguvu ya kiuchumi duniani. Hivi sasa Beijing na Washington zinafungamana katika masuala ya kisiasa na kiuchumi kwa kiwango ambacho hakijafikiriwa pale uhusiano baina ya nchi hizo mbili uliporejea kuwa wa kawaida mwaka 1979.

Lakini kukumbatiana huko sasa kunawafanya wanasiasa wa nchi hizo mbili wakune vichwa vyao wakati nchi zao zinakabiliana na matatizo ya kiuchumi. Katika hatua za mwanzo za uhusiano huo, Uchina ilikuwa ikiitegemea Marekani kwa ujuzi wa kiteknolojia na katika masuala ya fedha na usimamizi katika uchumi. Lakini lilivokuwa nchi hiyo sasa imeendelea, fedha za nchini zimechukuwa nafasi iliokuwa ikishikiliwa na rasil mali za kigeni kama kiini kikubwa cha uwekezaji.

Zaidi ni kwamba Uchina imekuwa sasa mkopeshaji mkubwa wa Marekani, ikiwa ni akiba kubwa ya fedha za kigeni zinazotokana na kuuza ngambo bidhaa zake za bei nafuu. Inakisiwa kwamba mnamo miaka kumi iliopita, Uchina imewekeza dola trilioni moja. Pindi Uchina itaamuwa kuuza sehemu tu ya uwekezaji huo, basi itasababisha kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya dola ya Marekani. Kuna watu wanaona kuna hatari kwa Marekani kuitegemea Uchina, na kuna hofu kwamba Uchina huenda ikaamuwa kutumia vitega vyake na rasil mali azke huko Marekani kama karata katika mashindano ya kibiashara na nchi hiyo.

Pia Uchina inaishiwa na subira kutokana na Marekani kukosa nidhamu katika siasa zake za fedha.

Lakini pande zote mbili zinatambuwa kwamba nchi hizo mbili zimefungamana sana kwa kiwango kwamba zinahitajiana. Karibu thuluthi moja ya bidhaa zinazosafirishwa ngambo na Uchina zinakwenda katika masoko ya Marekani.