1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya Bunge la Ulaya

Miraji Othman18 Machi 2008

Bunge la Ulaya leo linaadhimisha mwaka wa 50 tangu lianzishwe, taasisi ambayo kila miaka ilipopita imezidi kuwa na ushawishi. Lakini bunge hilo halifai livimbe kichwa kutokana na mafanikio yake.

https://p.dw.com/p/DQiz
Jengo la Bunge la Ulaya mjini Strassbourg, UfaransaPicha: AP

Bunge hilo lilianza miaka 50 iliopita kama klabu isiokuwa na mbwembwe, ambapo wawakilishi wa mabunge ya nchi za Ulaya waliketi kujadiliana. Leo lina wajumbe 785 waliochaguliwa moja kwa moja na raiawa Ulaya, likiwa ni bunge kubwa kabisa la kidemokrasia duniani. Katika miongo ya uhai wake limezidi kuwa na haki ya kushawishi mambo. Na pale Mkataba wa Lisbon utakapoanza kufanya kazi mwaka 2009, madaraka ya bunge hilo kushiriki katika ukataji maamuzi, katika mambo ya kisiasa au masuala ya siasa za kilimo, yatakuwa wazi.

Nii jambo zuri kuwa rai wapatao milioni 500 wa nchi za Umoja wa Ulaya wanawakilishwa na wabunge waliowachaguwa wenyewe moja kwa moja. Hata hivyo, lakini, mtu lazima atambuwe kwamba Bunge la Ulaya ni baraza la pili linaloshughulikia utungaji wa sheria. Hasa ushawishi mkubwa uko katika baraza la mwanzo, yaani lile baraza la mawaziri la nchi wanachama, ambapo serekali za nchi 27 za Umoja wa Ulaya zinawakilishwa. Bila ya baraza hilo kutoa uamuzi hamna kitu kinachoweza kufanyika. Haki ya kupendekeza kutungwa sheria mpya iko pekee kwa Tume ya Umoja wa Ulaya, hiyo ni kama uongozi wa utawala wa Umoja wa Ulaya. Bunge la Ulaya linaweza tu kushiriki katika kuamuwa kile ambacho hapo kabla kimewasilishwa. Wenyewe Wabunge wa Ulaya hawawezi kushikilia kutaka sheria ipitishwe. Wabunge wengi wanataka hali hiyo ibadilike, lakini wengine wanaonya kwamba mabadiliko yanaweza yakasababisha ushindani baina ya taasisi hizo tatu kubwa- yaani Tume, Baraza la Mawaziri na Bunge.

Licha ya hayo yote, pale mtu anapoipitia historia ya miaka 50 ya Umoja wa Ulaya, jambo moja muhimu linafaa litajwe, nalo ni vipi nchi zilizokuwa huru zimekubali kukabidhi baadhi ya madaraka yao kwa Bunge kubwa zaidi. Sehemu kubwa ya sheria ambazo sasa zinafanya kazi katika nchi wanachama zinafuata maagizo ya Tume ya Ulaya ilio na makao yake mjini Brussels. Huu ni mfano wa pekee katika historia. Yale malalamiko kwamba katika Bunge la Ulaya wanakaa wanasiasa wa daraja ya pili ambao wasingeweza kufanikiwa katika nchi zao, huenda yalikuwa ya haki hapo zamani. Lakini katika miaka ya karibuni kumezidi kuweko wanasiasa waliorejea nchini mwao kutokea Brussels ambaoko huko walipata umaarufu. Umuhimu wa bunge la Ulaya unaweza kuonekana kwamba kila miaka ikipita zaidi ya watu hukimbilia huko Brussles kutaka kushawishi namna fedha za Jumuiya zigawiwe. Kwanini watu wenye kushawishi wakimbilie huko Brussels ikiwa wabunge wa Ulayaa hawana ushawishi?

Lakini wapiga kura wa Ulaya hawaoneshi hamu kubwa kwa bunge lao. Sababu? Moja ni kwamba wabunge wa huko Brussels si maarufu na si wenye kuonekana sana hivyo hadharani kama walivyo wenziwao wa mabunge ya taifa. Na zaidi ni kwamba katika Bunge la Ulaya hakuna sakata za kisiasa au mizozano. Wabunge wa Ulaya hawaibebi serekali, hakuna makundi yanayounga mkono serekali au yanayounga mkono upinzani. Uamuzi unachukuliwa kutokana na wingi unaobadilika, kufuatana na mada inayozungumziwa. Tena ni kazi ngumu kuyafuata majadiliano yanayoendeshwa kwa lugha nyingi mbali mbali.

Lakini mabunge ya taifa yameshtambua kitambo kwamba wenziwao wa Brussels wana umuhimu zaidi. Ndio maana mabunge ya Ulaya yametaka yawe na ushawishi zaidi, na wameupata kutokana na mkataba mpya wa kuurekebisha Umoja wa Ulaya.

Katika miaka ijayo,bunge lina kazi mbili za kufanya; kwanza kuwa na uwazi kuhusu mishahara ya wabunge na vipato vya wafanya kazi wake, kwani kashfa za karibuni kuhusu mishahara mikubwa wanayolipwa wafanya kazi wa bunge hilo imechafua sifa yake. Na pili ni kwamba ni wiki moja tu katika mwezi ambapo bunge hilo hukutana katika mji wa Strassbourg wa huko Ufaransa, nyakati nyingine hukutana Brussels. Miezi hadi miezi inawabidi wabunge na wafanya kazi wa bunge hilo wasafiri huku na kule; hiyo ni kupoteza bure fedha za walipaji kodi. Hapa Rais wa Ufaransa, Nicolas Zarkozy, anatakiwa kuwa na ujasiri wa kukubali vikao vya mikutano huko Strassbourg vihamishiwe Brussels. Lakini wabunge wengi wanashuku kwamba jambo kama hilo halitafanyika mnamo miaka 50 ijayo.